The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 46

0

ILIPOISHIA:

Huku Mtima akiwa hafahamiki alipo, Abdulrahman anamteka Destiny na kutoroka naye hadi kwenye maficho yake, wakiwa huko anagundua kuwa wanafahamiana na msichana huyo baada ya Destiny kujitambulisha na kumuulizia Mtima.

Teremka nayo…

ABDULRAHMAN alipigwa na butwaa, hakupenda kabisa kuamini huyo aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Destiny, msichana waliyefahamiana vizuri kipindi cha nyuma walipokuwa wakisoma pamoja nchini Uholanzi.

Lakini hata hivyo, hiyo haikuwa sababu ya kumfanya amuonee huruma. Chuki aliyokuwa nayo dhidi ya Mtima baada ya kutofautiana ilimsababisha ajikute akimchukia pia ghafla mwanamke huyo, akawaza kumuua na kupanga kulifanya zoezi hilo usiku wa siku hiyo.

Kwa upande wa Mtima, baada ya mgogoro mzito wa nafsi, majuto na  hata kutofautiana na rafiki yake kipenzi Abdulrahman alikuwa ameamua kuachana na suala zima la kuendelea kuwaua watu wasio na hatia. Wakati huo Mtima hakuwa tena kwenye maficho waliyokuwa wakiyatumia na Abdulrahman, baada ya kutofautiana aliamua kujitenga na kwenda kujichimbia kwenye mapango ya Kuchungu huko katika Kijiji cha Ibanda.

Akiwa kwenye maficho hayo, muda mwingi Mtima aliutumia akiwa amelala kwenye mawe huku akiwaza mambo mengi yaliyopita katika maisha yake, pale alipokuwa anahisi njaa alikwenda kwa kunyata kwenye mashamba ya watu na kuchuma mahindi, mihogo na maembe kwa ajili ya kuitibu njaa yake.

Hayo ndiyo yakawa maisha yake, kwa takriban mwezi mmoja baadaye alikuwa bado katika mapango hayo ambapo wakati mwingine alianza kujichanganya na wakazi wa kijiji hicho, baadaye alimpata rafiki aliyeitwa Manyama, jamaa huyo alikuwa anajishughulisha na uvuvi pembezoni mwa Ziwa Victoria. Baada ya urafiki wao kukomaa, Manyama alianza kumfundisha Mtima shughuli hizo za uvuvi.

Mtima akaendelea kubadilika taratibu hatimaye akawa mtu mpole na mstaarabu kuliko alivyowahi kuwa huko nyuma jambo lililomfanya Manyama na familia yake kumpenda hasa kutokana na historia yake aliyowasimulia.

“Vipi bwana mbona leo unaonekana una mawazo?” Manyama alimuuliza Mtima jioni fulani baada ya kumkuta  mpweke huku ameshika tama.

“We acha tu ndugu yangu!”

“Nini tena?”

“Najutia mno maisha niliyokuwa naishi huko nyuma.”

“Usijali Mungu amekwisha kusamehe.”

“Natumaini hivyo pia kwa sababu kuna shinikizo lililosababisha nifanye yale yote, lakini watu wanatakiwa kujifunza!”

“Kwa nini?”

“Kama siyo unyama waliomfanyia mama nisingeziangamiza roho za watu wasio na hatia.”

“Ni kweli, albino pia ni binadamu wa kawaida, ana haki kama walivyo watu wengine.”

Maisha ya Mtima kwa wakati huo yalikuwa yamejaa matumaini makubwa, tofauti na awali alijikuta akianza kuhisi kuhitaji mpenzi wa kumfariji, alimwambia Manyama ambaye alimuahidi kumtafutia msichana mbichi wa Kisukuma ili aoe baada ya kumpa chumba cha kuishi, jambo hilo lilimfurahisha sana Mtima.

***

Mipango ya kumuua Destiny aliyokuwa nayo Abdulrahman iliendelea vyema ambapo muda wa kufanya tukio hilo ulipowadia, alichukua bisu lake kubwa lililonolewa sawasawa, akamchukua Destiny na kumpeleka mahali ambapo alipanga kulifanyia tukio hilo.

Destiny alikuwa analia kwa uchungu ni kweli alikwishaapa kuwa yuko tayari kufa kwa ajili ya Mtima lakini hakuwahi kutarajia kama angekufa kinyama kwa kuchinjwa kama ambavyo Abdulrahman alikuwa anataka kumfanyia.

“Tafadhali Abdulrahman usiniue.” Destiny aliongea akigumia kwenye kwikwi na kilio.

“Ni lazima ufe!.”

“Kwa nini lakini unanitendea unyama kiasi hiki?”

“Ili nipoteze ushahidi.”

Destiny hakuwa na neno lolote lile la kuongeza zaidi ya kulia na kumuomba Abdulrahman amuachie nafasi ya dakika kadhaa afanye sala, Abdulrahman hakuwa na kipingamizi, msichana huyo alipiga magoti, akafumba macho na kuanza kusali kwa mara ya mwisho akimuomba Mungu wake kuiweka roho yake mahala pema peponi.

Wakati huo, Abdulrahman alikuwa anamtazama tu akijiandaa kuitenda dhambi hiyo lakini pale Destiny alipomaliza tu kusali na Abdulrahman kushika panga akijiandaa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili mara zilianza kusikika risasi zikirindima katika eneo hilo.

Abdulrahman alishituka na kutupa kisu pembeni kisha akaichomoa bastola yake kiunoni.

Je, nini kitaendelea? Usikose Jumamosi ijayo.

Leave A Reply