The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Awasili Nchini “Dunia Inawasalimia” – Video

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Septemba 25, 2021 amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akitokea jijini New York, Marekani alikoshiriki katika Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), alikohutubia kwa mara ya kwanza Septemba 23, 2021.
 
Rais Samia amepokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa kidini pamoja na wananchi mbalimbali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.
 

“Tumekwenda kwenye safari ambayo kwa miaka 6 tumekuwa tukiwakilishwa na ngazi ya Uwaziri na Ubalozi, lakini hatukwenda kama kiongozi wa nchi, mara hii tumekwenda, tumeshiriki na wenzetu na dunia inawasalimia.

 

“Katika mkutano ule tulikuwa na mambo manne makubwa, moja ni masuala ya uchumi na namna yalivyoathiriwa na maradhi ya UVIKO-19. Pili ni masuala yote ya UVIKO-19, kuhusu chanjo na kushirikiana jinsi ya kushinda janga hili.

 

“La tatu ni masuala ya utawala bora katika nchi zetu na utawala bora duniani. Pia tuligusia kuhusu masuala ya mazingira, kwa niaba ya Watanzania iliiahidi dunia kwamba Tanzania tutayafanyia kazi yote haya ili twende na dunia inavyokwenda.

 

“Nimepata fursa ya kuonana na Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Biashara Duniani, wafanyabiashara wa marekani waliowekeza Tanzania na wanaotaka kuja Tanzania, nimeonana na Marais wenzangu, orodha ni kubwa.

 

“Kwa miaka 60 sasa nchi yetu imekuwa ikijengwa kwa hatua mbalimbali, niwaombe kila mmoja wetu tuijenge nchi yetu kwa matofali na nondo madhubuti ili tulisimamishe vyema Taifa letu. Tumewahakikishia Umoja wa Taifa kwamba Tanzania tupo na na tupo imara, tutaendelea kufanya kazi na dunia,” amesema Rais Suluhu.

Leave A Reply