The House of Favourite Newspapers

JPM: “Wananchi Wanakufa, Aliyechoma Mradi wa Maji Akamtwe Sasa Hivi” – Video

Rais Dk. John Magufuli leo Jumapili Oktoba 6, 2019 ameanza ziara ya siku tatu mkoani Rukwa ambapo anatarajiwa kufungua barabara ya Tunduma – Sumbawanga yenye urefu wa Kilomita 223.21. Rais Magufuli yupo katika ziara ya siku tisa katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi.

 

Magufuli amesema ameanza ziara yake ya kikazi mkoani Rukwa kwa majonzi baada ya kuona fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi hazifanyi kazi iliyokusudiwa;

 

“Mbunge huyu alikuwa akinisumbua tangu nikiwa waziri, Daraja la Momba alinisumbua kweli, anapenda jimbo lake. Lakini binadamu ukiafanyia kazi atakusema vibaya, unamvusha kwenye mto anakwambia mgongo wako unanuka, una jasho. Ilikuwa aitwe kwenye kamati ya CCM afukuzwe, lakini alikuwa imara kuwatetea wananchi wake na leo matunda yanaonekana.

“Kuna bilioni zimetolewa hapa Laela akapewa mkandarasi. Wananchi hawajapata maji, mradi umechomwa moto kabla haujakamilika, sola 170 zimechomwa, miradi ya hovyo, polisi wapo, PCCB wapo, nataka wote wachunguzwe na kupelekwa mahakamani, waliompa miradi nao washikwe.
RPC na PCCB muanze kushughulikia hili la waliochoma mradi wa maji, mnachunguza miezi miwili? Wananchi hawapati maji wanasubiri uchunguzi wako? Huenda wengine wamekufa kwa kunywa maji machafu. Watuhumiwa wapo nje wanatembea? Tuma askari wako wakawakamate sasa hivi.
“Watu waliohusika kuchoma mradi wa maji Laela ndani ya siku 7 wawe wamekamatwa, suala hili nitalishughulikia mwenyewe. Waziri wa Maji, RPC, PCCB, TAMISEMI na wote mkae mtengeneze jinsi ya kuwakamata hawa watu, na katika suala hili sina mzaha nitaondoka na watu.
“Sikuchaguliwa kwa ajili ya kuonekana sura nzuri, huenda hata mke wangu ananiona sura mbaya, lakini tumechaguliwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. Hawa wananchi wasidhurumiwe, miradi inachomwa, pesa zinaliwa na wananchi hawafaidiki, sitokubali.
“Niwaombe ndugu zangu na watani zangu Wafipa hii barabara muitumie kiuchumi mmejitahidi sana kupiga hatua kimaendeleo na jukumu letu kama serikali ni kuhakikisha tunaboresha miundombinu.” amesema Rais Magufuli.

 

Comments are closed.