The House of Favourite Newspapers

Magufuli Awapongeza Mwinyi, Maalim Seif – Video

0

 

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutanguliza maslahi ya nchi mbele na kuhakikisha amani inaendelea ili wananchi waendelee na shughuli zao na serikali itekelezE miradi ya maendeleo.

 

amesema hayo leo alipokutana na kufanYa mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, waliomtembelea nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

 

“Nawapongeza Rais Dkt. Mwinyi na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif kwa Sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyEa siku chache zilizopita, wamesherehekea kwa aina ya tofauti. Mapato yanayopatikana Zanzibar yanakwenda kuwasaidia wananchi.

 

“Nampongeza Maalim Seif kwa kuwa miongoni mwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Mwinyi. Maalim amefanya kazi na Mzee Mwinyi na leo anafanya kazi na mtoto, uzoefu wake ni mkubwa, sasa hivi ana miaka 77, atakapomaliza atakuwa na miaka 82, tunahitaji uzoefu wake.

 

“Rais Dkt. Mwinyi ninamfahamu kwa miaka 20, ana moyo mzuri, mnyenyekevu, ana heshima na ni mchapakazi, nilifahamu Zanzibar ya Hussein Mwinyi itakuwa ya tofauti. Nampongeza kwa hatua alizoanza kufanya hata mapato yameanza kuongezeka, mafisadi wanashughulikiwa.

 

“Tunatakiwa Watanzania tutangulize maslahi ya mataifa yetu kwanza. Maadui zetu wangefurahi sana kuona tunagombana na Zanzibar inachafuka lakini wameshindwa kwa sababu viongozi nyie hamkuwa na mawazo ya kuvunja umoja wa kitaifa.

 

“Maamuzi ya Maalim Seif ni ya kishujaa, yana mwongozo wa Mwenyezi Mungu, tumeona mataifa mengi duniani wanashindwa kuendelea sababu ya ugomvi, Watanzania wanahitaji maendeleo. Maalim Seif ameacha interest zake akatanguliza interest za Wazanzibari.

 

“Rais Mwinyi na Makamu wako Maalim Seif mmewafanyia lililo jema Wazanzibari, nafikiri hata mambo ya ubaguzi huyu Mpemba huyu Muunguja hayatakuwepo tena, kama yatakuwepo ninyi mkahubiri huo umoja. Zipo ndoa ambazo zilivunjika kwa sababu labda mwanaume alipigia ACT-Wazalendo na mwanamke akapigia CCM. Siku Maalim Seif alipoingia madarakani ndoa zile ziliungana.

 

“Na haya mambo ya vyama yasitusumbue, hata wewe Maalim Seif ukitaka kuja kuoa CCM hapa Chato nitakutafutia, hakuna tatizo, Watanzania tutangulize maslahi ya taifa letu kwanza, maadui zetu wangefurahi kuona tunagombana, Zanzibar inachafuka, lakini wameshindwa.

“Rais Mwinyi anatoka Unguja, Makamu wake wa kwanza Maalim Seif anatoka Pemba, Makamu wake wa pili anatoka Pemba, katika viongozi wakuu watatu wa SMZ wawili wanatoka Pemba, hii ina maana kubwa katika uongozi, Mhe. Mwinyi nakupoingeza kwa hilo umejenga upendo mkubwa.

 

“Maalim Seif kabla ya kuja Chato amepitia kukagua ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi linalogharimu Tsh bil 700, huu ndiyo Utanzania, pia wanakwenda kuangalia miradi kwenye soko la dagaa, Maalim Seif usishangae siku nikakualika kuja kufungua mradi wowote huku.

 

“Mhe. Rais Mwinyi umeanza vizuri sana, usiogope kutumbua majipu, wanaokwamisha maendeleo ya watu, fanya. Nikuombe Maalim Seif msaidie Mhe. Rais kuhakikisha mali za wanyonge zinasimamiwa kikamilifu. Kwa mwendo huu mlioanza nao, Zanzibar itakuwa Dubai nyingine, kwa sababu mahali palipo na amani wawekezaji watakuja.

 

“Mhe. Mwinyi ameniomba wawe na zoo au ranchi ili wafuge wanyama, sababu sheria zinaruhusu tutakuuzia wanyama kwa bei ya serikali ili watalii wakija Zanzibar waache hela huko huko. Hela ikiingia Zanzibar, imeingia Tanzania. Na madeni tunayoingia tutayalipa kama Tanzania,”  amesema Rais Magufuli.

 

Naye Rais Mwinyi amesema: “Leo tuko hapa tukiwa wamoja tuko kwenye serikali ya umoja wa kitaifa na siyo sisi tu viongozi tumeungana, Wazanzibar sasa wana mwelekeo wa kuwa wamoja zile tofauti zetu za kisiasa tumeziweka pembeni sote tunashirikiana kujenga nchi yetu.”

Pia Maalim Seif Sharif Hamad amesema: “Tumebadilishana mawazo juu ya nchi yetu na kushauriana namna bora zaidi ya kuwatumikia, mazungumzo yenye matumaini kuwa kiongozi wetu yuko pamoja na sisi hasa katika kuunganisha umoja, upendo na maelewano katika visiwa vyetu.

 

“Nimetembelea mradi wa daraja la Magufuli, siyo kwamba litaunganisha maeneo mbalimbali nchini bali litaunganisha nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati, hivyo nampongeza Rais Magufuli kwani mradi huo una manufaa makubwa.

 

“Tulikuwa na mazungumzo mazuri ya kidugu, mazungumzo ambayo yamenipa matumaini kwamba kiongozi wetu Rais Magufuli yuko pamoja na sisi hasa katika suala zima la kuimarisha umoja, upendo na maelewano katika Visiwa vya Unguja na Pemba.”

 

Leave A Reply