Mwinyi Aapisha Mawaziri, Awapa Maagizo Mazito – Video

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, amewashukuru mawaziri wote kwa kukubali uteuzi wake huku akisema hakuna hata mmoja kati yao aliyemwambia kama atamteua, hivyo kitendo hicho cha kuapa kimewafanya viongozi hao tayari wamepokea uteuzi huo na kuwa mawaziri, hivyo kazi inaanza mara moja.

 

 

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Novemba 21, 2020 visiwani humo  baada ya kuwaapisha mawaziri hao aliowateua hivi karibuni  na kuwapa maagizo mbalimbali ya utendaji katika wizara zao ili watimize majukumu yao ya kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo.

 

 

“Siku natangaza baraza niliulizwa, unawaambiaje mawaziri uliowateua?  Nikasema nitawaambia siku ninayowaapisha na maagizo ni haya yafuatayo, kila waziri ahakikishe anaijua wizara yake na taasisi zilizo chini yake haraka iwezekanavyo.

 

“Nataka kila mmoja wenu abuni mbinu mpya za kuleta ufanisi katika kazi. Nataka watu wawe wabunifu usingoje mimi nikuite kafanye hivi, kafanye vile, hakikisha wewe mwenyewe kwa kutumia wataalamu walioko katika wizara yako mnakuwa wabunifu.

 

Mawaziri mkazingatie Ilani ya Uchaguzi inasema nini juu ya wizara yako.   Hotuba yangu ya ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi inasemaje, ahadi zangu za kampeni, pia chukueni mawazo ya wadau, mfano huwezi kufanya kazi muhimu ya Wizara ya Elimu bila kukutana na Chama cha Walimu.

“Ndugu mawaziri nimewaapisha nendeni mkafanye kazi na mwajibike, wajibu unaendana na haki, hakikisheni mnawapa watu haki zao, haki za wafanyakazi wapeni posho na mishahara yao, simamieni haki za wananchi mfano Wizara ya Ardhi malalamiko mengi, kutaneni na watu wasikilizeni.

 

“Wizara ya ardhi kuna malalamiko makubwa, watu wananyang’anywa haki zao, rushwa ipo ni wajibu wetu kuiondoa, ubadhirifu upo, kuna semina zisizokwisha, safari za kikazi zisizokuwa na tija na matumizi mbalimbali ya mafuta, hakikisheni mnaondoa.

 

“Makamu wa Pili wa Rais amekwenda kuangalia mradi wa kutotoresha vifaranga vya samaki, alichokiona pale samaki watano, majogoo watatu, kaa mmoja haiwezekani, nahitaji ripoti ya kina, fedha zilizotumika na kwa nini uko namna ile. Nimetembelea baadhi ya maeneo, nimesikitishwa na kiwango cha miradi tunayoifanya, mkandarasi ameshalipwa fedha zote, nataka maelezo ya kina juu ya mradi ule,” amesema Mwinyi.

 

 

Toa comment