The House of Favourite Newspapers

Samia: Bunge la Kenya Linasimisimua, Mna Demokrasia – Video

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atahutubia Bunge la Kenya lililo na mjumuiko wa wabunge wa Seneti na Bunge la Kenya.

 

“Nina furaha kubwa kupata nafasi ya kuhutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na la Kitaifa Nchini Kenya, Tanzania tuna Bunge moja. Kwangu, ndio mara ya kwanza kuhutubia Bunge lenye chemba mbili. Sio jambo dogo na ni heshima iliyoje.

 

“Tumeguswa sana na Heshima na Ukarimu mliotuonesha. Sisi #Tanzania tutalipa wema huu. Namshukuru Kaka yangu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupiga simu na kutufariji tulipofiwa na Dkt Magufuli. Hatutasahau kitendo chake cha kutukumbusha kuheshimu Dini za wengine.

 

“Nilikwenda #Uganda kusaini Mkataba lakini haikuwa ziara rasmi. Ziara yangu rasmi tangu kushika Uongozi nimeanzia Kenya. Nimeanza #Kenya sio kwasababu ni karibu kijiografia lakini ni kwasababu ya Umuhimu wa Kenya ndani ya Tanzania.

 

“Busara inaelekeza kuwa ukiwa mpangaji mpya lazima ujitambulishe kwa majirani. Nami nimekuja Kenya kuitikia mwito wa Rais Uhuru Kenyatta. Nimebaini sehemu kubwa ya ujumbe nilioambatana nao wanajua vichochoro vya Nairobi, wanajua nyama choma inapatikana wapi.

“Namshukuru Kaka yangu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupiga simu na kutufariji tulipofiwa na Dk Magufuli. Hatutasahau kitendo chake cha kutukumbusha kuheshimu Dini za wengine.

“Rais Uhuru Kenyatta ni mtu wa kutimiza ahadi. Ili kuondoa mitazamo hasi tumepanga kukutana mara kwa mara, kwa maana ndugu wanaotembeleana undugu na uhusiano wao unaimarika. Umbali hujenga mashaka na ukaribu huondoa mashaka.

“Ushirikiano wa Tanzania na Kenya sio wa hiari. Wanyamapori wanakuja kupata mimba Kenya wanarudi kuzaa Tanzania. Kama Wanyama wana udugu sisi wanadamu tunatengana wapi? Ushirika na ujirani vinatufanya tuwe pamoja. Tupendane au tuchukiane hatuwezi kukwepa kuwa pamoja.

“Iwe kheri au shari, iwe neema au dhiki tunategemeana. Panapotokea ukame Tanzania, njaa inabisha hodi Kenya. Panapotokea uzalishaji ukasimama Kenya bidhaa zinakosekana Tanzania. Hivyo, hapana budi tupatane, tushikane ili tuishi kwa neema na furaha.

“Binafsi huwa nashangazwa sana na wale ambao wanadhani kuwa eti #Kenya na #Tanzania ni washindani na kwamba uhusiano wetu unapaswa kuwa wa kukamiana. Mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake.

“Wafanyabiashara nendeni mkashirikiane na sio kushindana, mna bahati kwamba katika Nchi zetu hizi mbili upande mmoja kuna Uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna Suluhu ya kuondosha vikwazo vya biashara, hapo mshindwe nyinyi tu.

“Wanaoamini Tanzania na Kenya ni Washindani ni wenye choyo, wana maono mafupi na akili mbovu. Bahati mbaya wapo kwenye pande zote #Kenya na #Tanzania na wapo kwenye Serikali zetu na Wanasiasa, bahati nzuri sio wengi ndio maana uhusiano wetu unadumu.

“Tunavyo vituo vya pamoja mipakani ambavyo vimerahisisha shughuli katika mipaka ya Kenya na Tanzania. Katika ushoroba wa Pwani tuko mbioni kukamilisha kipande cha Pangani Bagamoyo na Uhuru ameniambia yuko mbioni kukamilisha mazungumzo ya kupata fedha ili tumalizie.

“Vyovyote itakavyokuwa, lazima tushirikiana na majirani zetu wakiwemo Kenya. Tuna miradi mikubwa inayotaka ushirikiano kati ya Mataifa haya mawili. Yeyote anayedhamiria kuleta uhasama kati yetu, aelewe tulikuwepo, tupo na tutaendelea kuwepo.

 

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na yenye kuamsha matarajio makubwa sana kwa Nchi zetu mbili. Kwa yale tuliotofautiana, hayakuwa na misingi ila tu ni mitazamo tofauti ya watu. Uchungu wowote uliojitokeza ulikuwa uchungu wa uzazi na sio wa maradhi.

 

“Dunia inakabiliwa na janga kubwa la Corona ambalo limeathiri kwa ukubwa ukuaji wa Uchumi wetu. Leo #Corona imebadili mfumo wa maisha yetu na kutufanya tufunge midomo na pua kama tulivyokuwa tukiwafunga Mbuzi tukiwapeleka kwenda kula.

“Sisi Tanzania sio Kisiwa, tunaishi kama sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa hivyo kupitia Kamati ya Wataalamu niliyoiunda tumeanza mchakato wa kutafakari mbinu zaidi za kukabiliana na janga hili huku tukisubiri mapendekezo na hatua zaidi za kuchukua.

“Badala ya kunyang’anyana idadi ya watalii, busara itumike tumshawishi mtalii aongeze siku za kukaa Kenya na #Tanzania. #Kenya ikiwa salama, Tanzania iko salama, pia Tanzania ikiwa salama na Kenya iko salama.

“Chini ya uongozi wangu, tutafanya kila tunachoweza ili kuimarisha uhusiano wetu. Dira ya Serikali yangu ni kudumisha ya Awamu iliyopita na kuendeleza mapya. Kama kuna ambalo linalega au uhusiano wetu unasuasua nimekuja kuyanyoosha yale yaliyojipinda pinda.

 

“Kama ambavyo Ikolojia yetu inavyoingiliana ndivyo na Vivutio vyetu vya Utalii vinavyoingiliana. Hivyo hakuna haja ya kushindana. Mwl. Nyerere alisema tukipoteza muda mwingi kunyang’anyana kibaba, tutapoteza muda mzuri sana wa kuvuna kikubwa zaidi.

“Mabunge yenu ya Kenya yanatusisimua kwa mengi, tunafurahia upana wa #Demokrasia yake, uzito wa mijadala na hamasa ya Wabunge. Tulifurahishwa zaidi na uamuzi wenu wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili Bungeni, na-enjoy Kiswahili chenu kina vionjo vingi.

 

NA EDWIN LINDEGE

 

Leave A Reply