The House of Favourite Newspapers

Liverpool vs Man city… Hii ni Kwa Wakubwa tu, Watoto Kaeni Mbali

0

FEBRUARI 7, mwaka huu ubao ulisoma Liverpool 1-4 Manchester City ikiwa ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya England ‘Premier League’, kesho Jumapili timu hizi zinaenda kukutana tena katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo.

 

Liverpool watakuwa Anfield kuwasubiri Manchester City katika mchezo wa raundi ya saba kwa timu zote, bonge la mechi kwa wikiendi hii.

 

Majogoo wa Liverpool chini ya Kocha Jurgen Klopp wanaingia uwanjani wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kwenye ligi kati ya sita waliyocheza ambapo wameshinda minne na sare mara mbili.

 

Man City wakiongozwa na kocha Pep Guardiola watakuwa Anfield wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo uliopita kwa mabao 4-1 lakini rekodi zao za msimu huu wameshinda mechi nne wamepata sare moja na kufungwa moja.

 

Safu ya ushambuliaji ya Liverpool ikiongozwa na Mohammed Salah mwenye mabao matano inaonekana kuwa imara zaidi ukilinganisha na wapinzani wao kwani ina wastani wa kufunga mabao 2.50 kwa mechi na hadi sasa wachezaji wao wametengeneza nafasi 20 za mabao na wana umakini wa pasi zao kufika ni 84%.

 

Kwa upande wao Man City, wanaonekana hawamtegemei mmoja katika ufungaji kwani kwenye listi yao ya ufungaji mwenye mabao mengi ni Gabriel Jesus na Ferran Torres ambao kila mmoja ana mawili na baada ya hapo wanafuata wenye mojamoja.

 

Rekodi zao za kufunga kwa mechi ni mabao 2.00 pia wametengeza nafasi 17 na wana umakini wa pasi zao kufika kwa 90%.

 

REKODI ZINAIBEBA CITY, LIVERPOOL NI MFUPA

Miaka ya nyuma Liverpool ilikuwa inajipigia tu Manchester City hadi Waarabu walipoinunua klabu hiyo kibao kimekuwa kiki geuka, sasa mechi yao ni ngumu kutabirika.

 

Ukiangalia takwimu zao za miaka yote za Premier, Liverpool ameshinda mechi 20 dhidi ya 11 za City kati ya 48 walizokutana huku wakitoka sare mara 17.

 

Kwa upande wa mabao Liver wamefunga 74 na City 64, kwa miaka ya karibuni timu hizi ndizo ambazo zimekuwa zikishindania ubingwa na utaona kwa miaka minne iliyopita wao ndio wametwaa uchampioni wa Premier.

 

Angalia pia msimamo hadi sasa, Liver wako kileleni na pointi 14 chini yake wako City na pointi 13 wote wana GD ya +11.

 

Wakati Liver akitambia ubora wa safu yao ya ushambuliaji kumbuka beki yao imeruhusu mabao manne wakati City wao wameruhusu moja tu, hapa ni vita kati ya Salah na mbabe Rúben Dias.

 

WAZEE WA KUBET

Wale wa betting ukiangalia odds ambazo amepewa Liverpool kushinda mechi ya leo ni 2.90 wakati sare ni 3.50 na ushindi kwa City ni 2.40

 

Mechi sita zilizopita za michuano yote baina ya timu hizi inaonyesha kuwa zimekuwa zikitoa mabao mengi. City imeshinda nne, Liverpool moja huku zikitoka sare mara moja. Hapa unaweza kutupia GG.

 

MWAMUZI WAO HUYU HAPA

Paul Tierney, 40, anatarajiwa kuchezesha mchezo huu na msimu huu tayari amechezesha mechi tano ambapo ametoa njano 19, hajatoa nyekundu ila ametoa penalti moja.

 

Amechezesha big match tatu, Spurs 0-3 Chelsea, Leicester City 0-1 Man City na Arsenal 0-2 Chelsea.

Mwamuzi huyu atasaidiwa na Lee Betts na Constantine Hatzidakis. Kule VAR watakuwepo Stuart Attwell, akisaidiana na Marc Perry na mwamuzi wa nne ni Mike Dean.

 

3,309: Pasi walizopiga Liverpool msimu huu kwenye Premier

3,746: Idadi ya pasi walizopiga Man City kwenye Premier

 

KULE HISPANIA NAKO MOTO

Wakati England kukiwa kugumu, leo Jumamosi kule Hispania nako miamba ya soka nchini humo Atletico Madrid watakuwa na kazi ngumu mbele ya Barcelona kwenye Uwanja wa Wanda saa 4:00 usiku kwa saa za Bongo.

 

Atletico walio nafasi ya nne kwenye msimamo wamecheza mechi saba wameshinda nne, sare mbili, wamepoteza mmoja, wamefunga mabao tisa na kufungwa sita.

 

Barca wao katika mechi sita walizocheza wameshinda tatu na sare tatu hawajapoteza mchezo wowote. Wamefunga mabao 11 na wamefungwa matano.

 

Ukiangalia matokeo yao katika mechi sita zilizopita za michuano yote, Atletico ameshinda mara mbili sawa na Barca sare zipo mbili.

 

Makocha Ronald Koeman wa Barca na Diego Simeone watakuwa na kazi kubwa za kuhakikisha wanawaongoza vijana wao ili wazipe alama tatu timu zao.

Wazee wa kubet hapa kulingana na kiwango cha Atletico msimu huu wameipa nafasi ya kushinda ya odd 1.95 na Barca wana 4.00.

 

MECHI ZAO ZILIZOPITA

EPL: Liverpool 1 : 4 Man City

EPL: Man City 1 : 1 Liverpool

EPL : Man City 4 : 0Liverpool

EPL : Liverpool 3 : 1 Man City

ECS Liverpool 1 : 1*Man City

 

MECHI ZAO ZILIZOPITA

Barcelona 0 : 0 Atletico

Atletico 1 : 0 Barcelona

Barcelona 2 : 2 Atletico

Barcelona 2 : 3 Atletico

Atletico 0 : 1 Barcelona

LUCY MGINA, na mtandao

Leave A Reply