The House of Favourite Newspapers

LULU AIBUA MAZITO JELA! MKUU WA GEREZA AONGEA NA IJUMAA

0
Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Wakati mwanadada mrembo kwenye tasnia ya filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, akielekea kumaliza wiki mbili gerezani Segerea, Dar, anakotumikia kifungo cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia staa mwenzake wa filamu, Steven Kanumba, binti huyo ameibua mazito jela, Ijumaa linakupasha.

 

Tangu Lulu ahukumiwe kifungo hicho, mtaani kumekuwa na mijadala mbalimbali juu ya kifungo chake ambapo wapo wanaodai kuwa atatumikia mwaka mmoja kwa madai kwamba gerezani siku inahesabiwa usiku na mchana kuwa ni siku mbili.

“Lulu hawezi kukaa gerezani kwa muda wa miaka miwili, ninachofahamu huwa wanahesabu usiku na mchana kuwa ni siku mbili kwa maana hiyo kwa kifungo chake cha miaka miwili atatumikia mwaka mmoja tu,” alisema jamaa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Said Juma wa Mwenge, Dar huku kundi la watu likiwa limemzunguka ambapo wengine walimpinga na wengine kukubaliana naye.

 

Kwa upande wake, John Koloswa ambaye alikuwa katika kijiwe hicho aliibua jambo jingine na kudai kwamba Lulu anaweza kutoka gerezani kwa msamaha wa Parole ambao ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada ya kukidhi vigezo.

“Ninavyojua kesi ya mauaji bila kukusudia ina msamaha hasa mtu asipohukumiwa kifungo cha maisha. Tena ikiingilia Bodi ya Parole, Lulu anaweza asikae hata hiyo miaka miwili aliyohukumiwa,” alisema jamaa huyo.

 

MKUU WA MAGEREZA AONGEA YA KUSHANGAZA

Kutokana na mijadala hiyo kupamba moto, juzi, Ijumaa lilizungumza na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Dk Juma Malewa ambapo aliibua mambo mawili mazito juu ya jambo hilo.

Alipoulizwa kama kweli Lulu hatakaa gerezani kwa miaka miwili kama alivyohukumiwa, Dk Malewa alikuwa na haya ya kusema: “Ni kweli Lulu anaweza asikae gerezani kwa muda wote wa miaka miwili kama ambavyo hukumu yake
inasema kwa sababu katika sheria za magereza kuna kitu kinaitwa moja ya tatu (theluthi).

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Dk Juma Malewa.

“Huu ni utaratibu ambao unampunguzia mtuhumiwa moja ya tatu ya muda wake wa kukaa gerezani.” Akaendelea kufafanua: “Kwa hiyo kwa upande wa Lulu unaona sheria hiyo inamgusa moja kwa moja, hivyo basi, ukipiga hesabu ya miezi 24 aliyohukumiwa kukaa gerezani, ukitoa theluthi yake kwa maana ya miezi nane, basi atakaa gerezani kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne.

 

“Lakini pia sheria hii haiwahusu watu wanaokabiliwa na kesi za ubakaji ambao wamehukumiwa kukaa gerezani kwa miaka 30 au waliohukumiwa kunyongwa, kifo au kifungo cha maisha.” Hata hivyo, tamko la Dk Malewa litakuwa limeleta furaha kwa familia na ndugu wa Lulu kwa kuwa anaweza kutumikia jela mwaka mmoja na miezi minne tu kisha akarejea uraiani kuungana nao tena.

 

Jambo jingine alilozungumza kumhusu Lulu gerezani liloonekana la kushangaza ni juu ya Parole ambapo Dk Malewa alisema: “Parole ni sheria inayompa mfungwa kutumikia kifungo cha nje, lakini inamhusu zaidi mfungwa aliyehukumiwa kuanzia miaka minne na kuendelea. Kwa mujibu wa sheria hii Lulu hana haki ya kupata Parole, kwa kuwa yeye amehukumiwa miaka miwili.”

 

MREMA NAYE ANENA

Akizungumza na Ijumaa, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustine Lyatonga Mrema alifafanua sheria za bodi yake kwa kusema; Moja; awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwenendo wa kurekebishika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya kifungo chake kwa masharti maalum.

 

Alisema masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote hadi atakapomaliza kifungo chake, kuzingatia masharti ya Parole anayopewa kikamilifu pamoja na kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato halali katika jamii.

 

Pili; awe ameonesha kujutia kosa, kurekebishika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani. Tatu; mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii. Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani.

 

“Utaratibu huu ni wa kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu kuanzia miaka minne ambao ndiyo wengi waliopo magerezani,” alisema Mrema kwa msisitizo. Aidha, alisema Parole ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika urekebishaji wa tabia ya mfungwa kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni zao katika jamii. Hata hivyo, Lulu kwa kuwa amehukumiwa kifungo cha chini ya miaka minne jela, hahusiki na ‘huruma’ ya Parole.

Leave A Reply