The House of Favourite Newspapers

Maajabu Yaliyofanywa na Kikosi Bora cha VPL 2019/20

0

 

SHAMRASHAMRA za tuzo za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2019/20 zilifanyika usiku wa juzi Ijumaa ambapo wachezaji, timu, makocha na viongozi mbalimbali waliibuka kidedea na kutwaa tuzo hizo kutokana na mchango mkubwa ambao waliutoa kwa kipindi chote cha msimu huu.

Tuzo hizo ambazo hazikuweza kufanyika mwaka jana kutokana na kutokuwepo kwa mdhamini wa ligi, zilirejea kwa kishindo ambapo kulikuwa na vipengele mbalimbali na zawadi lukuki kwa kila kipengele ikiwemo; tuzo na zawadi za fedha.

Miongoni mwa tuzo ambazo zilikuwa zikisubiriwa kwa hamu ni ile ya Kikosi Bora cha Msimu wa Ligi Kuu Bara ambacho huonyesha wanaume 11 waliofanya vizuri zaidi msimu huu.

Championi Jumatatu linaangazia mchango wa wanaume hao 11 waliochaguliwa kuonekana kuwa bora zaidi ya wenzao kama ifuatavyo;

AISHI MANULA

Ametwaa tuzo ya Golikipa Bora wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo, ndiye chaguo la kwanza la kocha Sven Vandenbroeck ndani ya kikosi cha Simba, naye hajamwangusha kocha wake kwani kwa msimu huu pekee ameweza kusimama langoni kwenye michezo 17 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa yaani ‘Clean sheets’.

NICHOLAS WADADA

Raia huyu wa Uganda alitwaa tuzo hiyo ya beki bora akiwashinda mabeki Bakari Mwamnyeto (Coastal Union) na David Luhende wa Kagera Sugar.

Wadada amehusika kwenye mabao nane kati ya 52 yaliyofungwa na Azam msimu huu, amefunga bao moja na kuasisti mengine saba.

DAVID LUHENDE

Huwezi kutaja mafanikio ya Kagera Sugar msimu huu na kuacha kuutaja mchango wa beki huyu wa kushoto, Luhende ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wametumika kwenye michezo yote 38 ya Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo amefanikiwa kutoa asisti nne za mabao.

SERGIE WAWA

Raia wa Ivory Coast ambaye ameendelea kuthibitisha ule usemi wa Kiswahili usemao ‘Ukubwa Dawa’ mara kadhaa amekuwa kiongozi wa safu ya Ulinzi ya Simba huku pia msimu huu akifanikiwa kuasisti mara moja.

BAKARI MWAMNYETO

Nahodha wa zamani wa Coastal Union ambaye tayari amekamilisha usajili wake wa kujiunga na kikosi cha Wanajangwani, alikuwa na msimu bora sana ambapo ameiongoza safu ya ulinzi ya Coastal kuwa miongoni mwa klabu ambazo zimeruhusu mabao machache zaidi msimu huu.

Ukiacha suala la kutimiza majukumu yake ya kuifanya safu ya ulinzi ya Coastal kuwa bora, Mwamnyeto pia ameisaidia safu ya ushambuliaji ya timu hiyo baada ya kuweka kambani bao moja.

ZAWADI MAUYA

Mkata umeme wa zamani wa klabu ya soka ya Kagera Sugar ambaye pia amekamilisha usajili wake wa miaka miwili kuitumikia Yanga msimu ujao, Mauya amepata nafasi ya kuingia kwenye kikosi bora cha msimu kwa kumshinda kiungo wa Simba, Jonas Mkude ambaye pia alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye kikosi hicho.

LUIS MIQUISSONE

Anatajwa kuwa ndiye mchezaji ghali zaidi kwenye Ligi Kuu Bara katika usajili ambao Simba iliufanya kipindi cha dirisha dogo la mwezi Januari ambapo Simba ilimsajili nyota huyu kutoka Klabu ya Mamelodi Sundowns inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Miquissone kwenye ligi kuu msimu huu ameifungia Simba mabao manne na kuasisti mara moja huku bao alilofunga dhidi ya klabu ya Alliance likiwa miongoni mwa mabao matatu bora msimu huu.

LUKAS KIKOTI

Ubora wa kikosi cha Namungo msimu huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubora aliokuwa nao Kikoti katika eneo la katikati ya uwanja, uwezo wake wa kuituliza timu na kupiga pasi zenye macho, unajidhihirisha kwenye furushi la takwimu bora alizozikusanya na hii ni baada ya kuhusika kwenye mabao 11 ya Namungo, amefunga mabao manne na kuasisti mengine saba.

MEDDIE KAGERE

Ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo, tangu ajiunge na Simba msimu wa 2018/19 Kagere ameifungia Simba mabao 45 kwenye Ligi Kuu Bara pekee huku msimu huu pekee akihusika kwenye mabao 28, akiweka kambani mabao 22 na kuasisti mara sita.

CLATOUS CHAMA

Kwa maneno machache unaweza kusema huu ulikuwa mwaka wake kwani ukiacha suala la kutajwa kuwa kwenye kikosi cha timu bora ya msimu huu, Chama mpaka sasa amefanikiwa kukusanya tuzo nne kubwa, tuzo hizo ni; Mchezaji Bora wa Michuano ya FA, Mchezaji Bora wa SportPesa, Kiungo Bora wa Msimu na Mchezaji Bora wa Msimu.

Ili kupata tuzo hizo ilimbidi chama achangie mabao 16 kwenye michuano yote msimu huu akifunga mabao matano na kuasisti mengine 11.

JOHN BOCCO

Nahodha wa Simba anayeshikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kwa miaka zaidi ya kumi aliyocheza ligi kuu amefunga zaidi ya mabao 100, msimu huu kwa mara nyingine tena ameiongoza Simba kutwaa kombe la tatu mfululizo ambapo yeye pekee amechangia mabao 12 ya Simba akifunga mabao tisa na kuasisti mengine matatu.

KWA maneno machache unaweza kusema huu ulikuwa mwaka wake kwani…

 

MAKALA| JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply