The House of Favourite Newspapers

Maalim Seif: Tusiingize Siasa Kwenye Corona

0

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad amewataka viongozi wa kisiasa nchini, kuweka mambo ya kisiasa kando na kuwaelimisha wananchi kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona na homa ya COVID19.

 

Hatua hiyo imekuja wakati maambukizi ya virusi hivyo yakizidi kushika kasi ambapo hadi kufikia Machi 19 mwaka huu tayari wagonjwa sita walikuwa wamebainika hapa nchini.

 

Kufuatia hali hiyo, Maalim Seif ambaye ambaye alifanya ziara katika ofisi za Global Publishers na kuzungumza na wahariri wa kampuni hiyo, alitoa wito kwa Watanzania kutofanya utani kwa sababu virusi hivyo vya Corona ni hatari.

 

Alisema tayari baadhi ya nchi zimepata athari kubwa kama vile China, Italia, Iran na Korea Kusini.

“Baadhi ya nchi wamefunga mipaka yao, anayeruhusiwa kwenda ni raia tu wa nchi ile wengine wote wanazuwiwa, hata Oman wametanga hata yule raia aliyepo nje haruhusiwi kuingia.

 

“Wananchi wachukue tahadhari sana, wafuate maelekezo wanayopewa na wizara ya afya, hii si siasa… hapa hapana siasa ni uhai wa mtu, uhai wa taifa letu. Hatutaki watu wapotee wafuate maelekezo wasiwe wakaidi na serikali ichukue hatua za kuwahami Watanzania, wala wasiogope kulaumiwa.

 

“Serikali italaumiwa watu wakifanya mambo ya hovyo, wasipochukua tahadhari kujikinga italaumiwa, cha msingi ichukue hatua sahihi kuhami Watanzania,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wanachama wa ACT Wazalendo pamoja na wa vyama vingine vya siasa kuwa kila moja ajihadhari na Corona.

 

“Kila mmoja achukue hatua ambazo atajinusuru kuambukizwa na maradhi haya mabaya sana.

“Wala wasidanganyike kwamba kuna dawa, hakuna dawa, wito wangu kwamba wote wanachama wa ACT, Chadema, CCM na kadhalika, wote tufuate maelekezo ya wataalam wa afya,” alisema.

 

Kauli hiyo ya Maalim Seif imekuja siku chache baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kusitisha mikutano yote ya ndani na ya hadhara ikiwa ni njia za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema ziara zote za viongozi wa chama, ambazo walikuwa wazunguke nchi nzima zimesitishwa hadi serikali itakapotoa maelezo zaidi.

“Vikao vya chama vilivyokuwa kwenye kalenda, ambazo si mkusanyiko kama Halmashauri Kuu, hivi vitaendelea,” alisema.

 

Polepole alisema CCM inajihadhari kwa kuweka dawa maalum ambayo itasambazwa nchi nzima kwenye ofisi za chama ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona.

Pia alitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa katika kipindi hiki, huku akiwaasa viongozi wa vyama vingine kuiga mfano wa CCM.

 

Tayari Rais John Magufuli alitoa wito Machi 16 alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua miradi wa barabara ya Morogoro wa kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 kwa kuwa ni hatari kwa sasa duniani.

STORI: GABRIEL MUSHI

Leave A Reply