The House of Favourite Newspapers

Machi 17 Yateka Akili ya Wasomaji

Mwandishi wetu | CHAMPIONI|  Dar es Salaam

MACHI 17, mwaka huu ambayo ni siku ya kuchezeshwa droo ya pili ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba awamu ya pili, imeteka akili za wasomaji wengi wa magazeti ya Global Publishers wakikumbuka jinsi wenzao watano

walivyoibuka na zawadi zilizobadili maisha yao katika droo ya kwanza iliyofanyika Februari 8, mwaka huu, katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar. Wasomaji mbalimbali waliopiga simu katika chumba cha habari cha gazeti hili, walisema wanategemea droo itakuwa ya wazi kama ilivyo kawaida ya Global Publishers na wao wamejipanga kuhakikisha hawapotezi hata nafasi.

“Najua ni bahati nasibu, lakini kujitabiria ushindi siyo jambo baya, maana ukisubiri mtu akutabirie mazuri utakaa sana, sasa naendelea kununua magazeti na kuhifadhi kuponi, kila ninapopata nafasi ninazipeleka mwenyewe ofisini Global, sitakaa mbali siku hiyo ili kushuhudia,” alisema Dedeki Jopi, wa Bunju jijini Dar es Salaam.

Tarik Mbashau, kutoka Tanga, naye alisema japokuwa atakuwa mbali siku ya kuchezwa kwa droo hiyo, ana uhakika wa kushinda kwani uzoefu unaonyesha wanaoshinda zawadi siyo wote huwa wa Dar es Salaam, kwani katika droo iliyopita, mshindi wa pikipiki alikuwa ni mwenyeji wa Muheza mkoani Tanga.

“Ingawa kuwepo mwenyewe eneo la tukio ni jambo zuri, lakini sisi tunawaamini sana Global, kama ni kuponi yako ndiyo imeshinda, zawadi zako utapata tu, hivyo tunaisubiri hiyo siku kwa hamu na sisi tutakuwa tunaomba dua tu tuibuke washindi,” alisema msomaji huyo.

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, alisema jana kuwa zoezi hilo la kufanya droo ndogo litaendelea kila mwezi ili kuhakikisha wasomaji wengi wa magazeti ya Ijumaa, Championi, Uwazi, Risasi, Amani na Ijumaa Wikienda wanapata zawadi. “Huu ni mwendelezo wa droo ndogo za Shinda

Nyumba kama tulivyoahidi hapo awali, tutazifanya kila mwezi na tumeboresha aina za zawadi pamoja na thamani zake, sasa wasomaji wetu watajikuta wakiondoka na zawadi nzuri zaidi tofauti na Bahati Nasibu iliyopita, niwasisitize tu wasomaji wetu waendelee kujaza na kutuma kuponi zao kwetu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuweza kuibuka mshindi,” alisema Mrisho.

Droo ndogo ya kwanza ilifanyika Februari 8, mwaka huu katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem ambako washindi watano walijishindia zawadi za pikipiki, televisheni, simu za kisasa, vyombo vya jikoni na vitu vingine vingi.

Washindi hao walikuwa ni Andrew Mtunguja wa Muheza mkoani Tanga, Ambrosi Ligonja wa Mang’ula Morogoro, Evans Stanley wa Kunduchi, Said Mohamed na Gasto Peter wote wa Kimara jijini Dar es Salaam. Bahati Nasibu hiyo kubwa kabisa kuwahi kuchezwa na kampuni ya magazeti, inadhaminiwa na Kilimanjaro Institute of Technology and Management iliyopo Mwenge kwa Mama Ngoma na Afrika Sana na British School ambayo ipo karibu na kituo cha daladala cha ITV, karibu na Kanisa la Lutheran.

Comments are closed.