The House of Favourite Newspapers

Madai: Dogo Apukutisha Utajiri wa Super Sami, Mke Atishiwa Maisha – Video

MAPYA yameibuka kufuatia kifo cha aliyekuwa mfanyabiashara  na tajiri wa mabasi ya Kampuni ya Super Sami, Samson Josiah almaarufu Super Sami, mkazi wa Magu mkoani Mwanza,  baada ya mke wa ndoa, Lilian Limbe,  kudai kuwa mali za mumewe zimeteketezwa na mdogo wa marehemu.

 

Akizungumza na Global TV Online, Lilian amedai kuwa baada ya msiba, ukoo wa Josiah ulikaa na kumteua shemeji yake huyo kusimamia mali za marehemu, lakini haikuchukua muda mali hizo akaanza kuzifuja,  jambo lililosababisha ukoo kumnyang’anya mali hizo na kuteua wasimamizi wengine wawili.

 

Mama huyo anadai baada ya hapo alipata taarifa kuwa ndugu wa marehemu wamepeleka maombi ya mirathi mahakamani,  jambo lilomlazimu kwenda mahakamani kupeleka pingamizi mali hizo zisigawiwe ili watoto wake wapate haki zao.

 

Mbali na hayo, Lilian anadai alipopeleka maombi hayo, kesi iliendeshwa na mahakama ikamteua yeye kusimamia mirathi hizo, ambapo anadai alianza kutumiwa ujumbe wa vitisho na ndugu wa marehemu kisha kukamatwa na kuwekwa ndani pasi na utaratibu wowote, hivyo anaiomba Serikali imsaidie ili apate haki yake kwani aliyekuwa ameteuliwa kusimamia mirathi hizo mpaka sasa hajampatia nyaraka yoyote ya mali za marehemu.

 

Mfanyabiashara huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku kadhaa, kabla mwili wake kuonekana katika Mto Ndabaka wilayani Bunda mkoani Mara ukiwa umefungwa kwenye kiroba na kuharibika vibaya.

VIDEO: MSIKIE: LILIAN AKIFUNGUKA

Comments are closed.