The House of Favourite Newspapers

MADAI YA KUBWIA UNGA, NDUGU WA DARASSA WAVUNJA UKIMYA!

Shariff Thabeet ‘Darasa’,

BADO gumzo lipo kila kona nchini, kwa mashabiki wa Muziki wa Bongo Fleva kutaka kufahamu wapi alipo mwanamuziki mwenye viwango vya juu kwenye tasnia hiyo, Shariff Thabeet ‘Darasa’, Ijumaa linakupa undani.

Ni takriban mwaka sasa, Darasa aliyetamba na wimbo wake wa Muziki, hajasikika kwenye media wala kuonekana kwenye mitandao ya kijamii na kinachoelezwa kumpoteza katika gemu ni madai ya kutumia dawa za kulevya ‘unga’.

 

Kwenye akaunti yake katika Mtandao wa Instagram, iitwayo ‘darasacmg’ yenye mashabiki zaidi ya laki mbili, mara ya mwisho kuposti picha ni Agosti 12, mwaka jana.

Lakini pia kuna moja ya akaunti ya mashabiki zake iitwayo ‘darasatz_cmg’ yenye mashabiki elfu ishirini na tano ilimposti Juni 28, mwaka huu na kueleza kwamba Darasa ameamua kuacha kila kitu na kushughulika na mwanaye na kwamba wazazi pekee ndiyo watamuelewa.

Moja ya shoo aliyofanya Darasa ukumbi wa Dar Live.

IJUMAA YAFANYIA KAZI TETESI ZA KUBWIA UNGA

Tokea madai hayo yaenee yapata mwaka mzima, magazeti ya Global yamewahi kuelezwa na vyanzo mbalimbali wakiwemo wanamuziki wenziye na Darasa kwamba jamaa kazama kwenye unga kiasi cha kuwa teja.

“Mnamuona Darasa siku hizi? Amechoka ile mbaya, unga umemmaliza,” chanzo kilieleza madai ambayo Ijumaa halikuyaamini.

Miluzi ya unga ilikuwa mingi kiasi cha kufikia hatua ya kutaja mpaka sehemu alipofichwa kwenye kituo cha kulelea waathirika wa dawa za kulevya ‘Sober House’ kwa ajili ya kutibiwa tatizo hilo.

GAZETI LA IJUMAA KAZINI

Baada ya kupewa ubuyu huo na vyanzo mbalimbali Ijumaa halina kawaida ya kunyamazia tetesi likaamua kumpigia simu ya mkononi Darasa kwa siku tatu kwa namba tofauti ili angalau kuupata ukweli wa madai hayo lakini mkali huyo wa vina simu yake haikuweza kupokelewa.

Ijumaa likaona mambo yasiwe mengi, Aprili mwaka huu likaamua kumuibukia maskani kwake Makongo jijini Dar alipokuwa anaishi wakati huo kwa lengo la kukutana naye ana kwa ana.

Lilipofika pale lilikutana na meneja wake anayefahamika kwa jina moja la Kimbe, ambapo baada ya kuulizwa kuhusu Darasa alisema yupo nje ya mkoa anafanya shoo.

 

Gazeti hili lilijaribu kumbana zaidi na kuweka wazi kwa meneja huyo juu ya madai ya kubwia unga, kutopokea simu za waandishi lakini na kuuliza juu ya shoo hizo za kimyakimya zilimaanisha nini, lakini meneja huyo hakutaka kufunguka lolote.

“Shida yenu si kumuona Darasa, akirudi nitawakutanisha naye,” aliahidi meneja huyo ahadi ambayo hakuitekeleza.

Mwezi mmoja baadaye Ijumaa lilirudi tena nyumbani kwa Darasa, waandishi waliishia kugonga mlango bila kujibiwa na mtu yeyote.

 

YUPO SOBER HOUSE?

Uchunguzi uliendelea; Ijumaa baada ya kunyaka taarifa kutoka kwa vyanzo kuwa msanii huyo yupo sober Bagamoyo, liliamua kutia timu huko mkoani Pwani kwenda kupeleleza.

Katika kituo hicho cha kulelea waathirika wa dawa za kulevya lilikutana na meneja wa kituo hicho ambaye alikanusha kuwepo kwa mwanamuziki huyo kituoni hapo.

MENEJA: “Mmeambiwa yupo hapa?

IJUMAA: “Ndiyo, kuna mtu ametueleza

 hivyo, kimsingi sisi hatumtafuti kwa ubaya tuna lengo zuri tu la kumsaidia kama rafiki yetu.”

MENEJA: “Hapana hapa hayupo angelikuwepo nisingekuwa na sababu ya kuwaficha.

 

IJUMAA LATOKA BAGAMOYO HADI KIGAMBONI

Baada ya kutoonekana kwa Darassa Bagamoyo Ijumaa lilifanyia kazi tetesi nyingine kwamba mwanamuziki huyo anapatiwa tiba ya kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya katika kituo kilichopo Kigamboni jijini Dar.

Msako uliendelea mpaka kwenye Sober ya Kigamboni, huko nako gazeti hili liliambulia patupu; hakukuwa na Darasa wala kivuli chake. Hata hivyo kazi haikuishia hapo, aliyetakiwa kupatikana ni Darasa na si vinginevyo.

 

IJUMAA LAAMBIWA YUPO ZANZIBAR

Iliposhindikana kumuona katika maeneo yaliyotajwa, ubuyu mwingine ukatua mezani pa dawati la Ijumaa kwamba Darasa kapelekwa Visiwani Zanzibar kutibiwa.

“Zanzibar panafikika, vyema mkafanya kila muwezalo kujua hicho kituo kiko wapi ili timu iwe na mwelekeo sahihi,” mkuu wa dawati la uchunguzi la Ijumaa alimuelekeza muongozaji timu ya upelelezi ambapo hata baada ya yote kufanyika Darasa hakuonekana Zanzibar kama ilivyodaiwa.

 

IRINGA YATAJWA

Mwishoni mwa Julai mwaka huu, taarifa nyingine zilidai kuwa Darasa yuko mkoani Iringa na kwamba anahifadhiwa huko kwa ajili ya tiba.

Hata hivyo hilo nalo halikuwa gumu, timu ya uchunguzi ilifanya yake na kubaini kwamba nazo zilikuwa ni tetesi zisizokuwa na ukweli.

 

LATINGA NYUMBANI KWAO KIWALANI

Darasa amekulia Kiwalani, sehemu moja inaitwa Migombani. Wiki mbili zilizopita Ijumaa liliamua kufunga safari na kwenda mpaka nyumbani hapo ili kuzungumza na mama yake.

Baada ya kufika hapo, lilifanikiwa kumkuta binti mmoja ambaye anamuita Darasa mjomba na shemeji yake Darasa ambaye ni mke wa mdogo wake.

 

Ijumaa, liliwachimba juu ya uwepo wa mama yake Darasa mahali hapo lakini watu hao walidai kwamba hakuwa akiishi tena mahali hapo bali alikuwa anaishi na Darassa, lakini wakati huo alikuwa amesafiri kwenda Tabora kwenye safari ya kifamilia. Kazi iliendelea na Darassa alizidi kusakwa nyumbani hadi studio alikopenda kuonekana bila mafanikio.

 

 IJUMAA LARUDI TENA NYUMBANI KWAO

Jumamosi iliyopita, Ijumaa liliamua kurudi tena nyumbani kwao Kiwalani, baada ya madai kuenea kwamba kwa sasa Darasa alikuwa pande hizo amefichwa chimbo kwa baba yake mkubwa. Baada ya kufika nyumbani hapo gazeti hili lilikutana na dada yake ambaye alikataa kujitambulisha jina lake halisi.

Alipoulizwa kuhusu Darassa alisema haya; “Ni kweli mimi ni dada yake mkubwa. Lakini sifahamu mengi kuhusu yeye kwa sababu ninaishi Morogoro, muda mrefu sijaonana naye na huku nimekuja kwa ajili ya harusi tu.

“Lakini kuhusu kuwepo Sober, hapana harusi imeisha juzi (Jumamosi) na Darassa ndiye amemfuata mama yake hapa na mimi ninamuona yupo vizuri tu,” alisema dada huyo.

 

Kwa upande wa ndugu yake mwingine na Darassa, aliyejitambulisha ni mdogo wake aitwaye Idrisa alisema Darassa yupo ‘fit’ na anajiandaa kuachia ‘projekti’ zake mpya.

“Ngoja niwaambie kitu waandishi mtahangaika sana kumtafuta Darassa lakini hamtompata. Lakini yupo fiti, nitakuonyesha ushahidi,” alisema ndugu huyo.

Baada ya maneno hayo akatoa simu yake na kuonyesha picha alizopiga na Darassa alipokuja kwenye harusi hiyo siku mbili zilizopita, akaonyesha picha na video wakiwa ‘lokesheni’ na Darassa alizodai kwamba ni za wimbo mpya ambao anakaribia kuutoa.

 

“Darassa hatumii dawa za kulevya. Labda majani, hapo angalau naweza nikaelewa. Dawa za kulevya hatumii.

“Mtu anayetumia dawa za kulevya yupo hivi? Angekuwa amepotea kabisa na lazima tu kwa uchunguzi wenu mngeweza kumpata.

“Lakini yeye ni mtu anayejielewa ambaye anaishi maisha yake ndiyo maana ameweza kuwa na uwezo wa kujichimbia na asipatikane,” alimaliza ndugu huyo.

 

IJUMAA LAPEWA NAMBA MPYA YA SIMU YA DARASSA

Baada ya kumalizana na ndugu huyo Ijumaa lilipewa namba mpya anayodaiwa kutumia hivi sasa msanii huyo ilipopigwa iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi (SMS) nao haukujibiwa.

 

NENO LA IJUMAA

Ni kweli ndugu walifunguka na kuonyesha baadhi ya ushahidi juu ya Darassa kuwa ‘fit’, lakini walikataa kutoa ushahidi huo ili jamii ione. Gazeti limejionea na kusikia maelezo yao, lakini bado kazi ipo palepale mpaka Darassa apatikane na mashabiki wake wamuone katika muonekano mpya! Endelea kufuatilia vyombo vyetu vya habari.

STORI: WAANDISHI WETU, IJUMAA

 

Darassa & ROMA Performance at DAR LIVE Dar es salaam 2016

Comments are closed.