The House of Favourite Newspapers

Mafuriko Yaua 6 Tanga, Barabara Zafungwa

WATU  sita wameripotiwa kupoteza maisha huku kaya kadhaa wilayani Korogwe zikikosa makazi baada ya nyumba zao kuanguka na zingine kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia saa 2 usiku wa Oktoba 8 hadi majira ya saa 9 alasiri Oktoba 9.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, SACP Edward Bukombe,  mvua hiyo iliyonyesha katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe katika milima ya Usambara ilisababisha barabara kuu ya Arusha -Segera -Dar eneo la Msambiazi Korogwe Mjini kutopitika na kufungwa kwa muda kwa tahadhari za kiusalama.

 

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa, alithibitisha barabara hiyo kufungwa kwa muda wa saa mbili na baadaye kuendelea na safari zake kwenda Tanga, Dar es Salaam, Lushoto, Moshi, Arusha na Nairobi kupitia Namanga mkoani Arusha.

 

Akizungumzia vifo vya watu sita, Kamanda Bukombe amesema watu hao ambao majina yao bado hayajajulikana ni kutoka kijiji cha Dindira ambako  mwanamke mmoja na watoto wake wawili waliangukiwa na nyumba usiku.

 

Aidha, Bukombe alisema, msichana mmoja anayejulikana kwa jina la Asha Yahaya Ambanyonge alikuwa amelala na wadogo zake wawili ambapo nao wameangukiwa na nyumba na kufariki papo hapo.

 

Wilayani Muheza katika Barabara ya Amani -Muheza, Kata ya Mbaramo eneo la Msangazi mawasiliano ya barabara yalifungwa kwa muda kutokana na mafuriko yaliyoziba njia.

Comments are closed.