The House of Favourite Newspapers

Magufuli Afuta Agizo Vyeti vya Kuzaliwa la Mwakyembe

Rais Magufuli akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana.

RAIS John  Magufuli amefuta agizo la Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, alilolitoa jana lililotaka wanandoa za kimila na kidini sharti wawe na vyeti vya kuzaliwa.

Akizungumza na wanahabari mkoani Dodoma, waziri huyo alitaka agizo hilo lianze kutumika Mei mwaka huu.
Magufuli ameagiza utaratibu wa awali uendelee kutumika kwa sababu wananchi wengi wa Tanzania hawana vyeti, hivyo wangekosa haki hiyo ya msingi ya kufunga ndoa.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amelifuta agizo lililotolewa waziri wa katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalowataka watu wote wanaotaka kufunga ndoa kuwa na cheti cha kuzaliwa kuanzia tarehe mosi mwezi Mei 2017.

Magufuli amefuta agizo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea Jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo amesema kuwa serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.

Amesema hadi kufikia sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ipo chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi wanaoishi vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.

”Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza waziri wa katiba na sheria Mhe. Harrison Mwakyembe apeleke bungeni kikarekebishwe” amesema Magufuli.

Wakati huohuo Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuzikagua vyema sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi.

Hata hivyo rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.

Comments are closed.