The House of Favourite Newspapers

Mahakamani: Sabaya Akiri Kumiliki Silaha

0

MSHTAKIWA namba moja katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amekiri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa anamiliki silaha aina ya Glock-17 kwa ajili ya kujilinda kutokana na kutishiwa kuuawa.

 

Hayo yamejiri leo Alhamisi, Agosti 19, 2021 wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani hapo ambapo kwa sasa Sabaya na wenzake wawili wanajitetea.

 

Akijibu swali la wakili wa Serikali Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka leo Alhamisi Agosti 19, 2021 mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Odira Amworo, Sabaya amesema silaha hiyo alianza kuimiliki Machi 24, 2021.

 

Mahojiano hayo alikuwa hivi;

Wakili: Tusaidie katika ushahidi wako wa msingi umeieleza mahakama unamiliki silaha

Sabaya: ni sahihi

Wakili: Unamiliki silaha ya aina gani

Sabaya: Hakimu kwa sababu ni kifaa cha moto sijui kitatumikaje nikieleza kilivyo.

Wakili: Nataka kujua ni silaha

Sabaya: Kwa usalama wa silaha hiyo na kwa sababu nipo gerezani naomba nisieleze silaha gani. Ni silaha ndogo inaitwa Glock 17.

 

Wakili: Utakubaliana na mimi kwa Kiswahili inaitwa bastola.

Sabaya: Hapana

Wakili: Ulikua unaimiliki kwa shughuli gani.

Sabaya: Matumizi ya ulinzi binafsi

Wakili: Unapokuwa wapi

Sabaya: Ninapokuwa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro

 

Wakili: Hai ulikuwa una maadui

Sabaya: Ndiyo mheshimiwa hakimu

Wakili: Ulianza kumiliki lini?

Sabaya: Nilianza kuimiliki Machi 24, 2021

Wakili: Kwenye ushahidi wako wa msingi siku ukiondoka kuja Arusha Februari 9, 2021 uliacha silaha yako nyumbani Bomang’ombe. Ni sahihi siku ile ulikuwa ukimiliki silaha?

Sabaya: Sikuwahi kumiliki silaha ya moto kwa wakati huo nilikuwa na silaha ila haikuwa silaha ya moto

 

Wakili: Una watoto wangapi

Sabaya: Kwa sababu nimeshasema familia iko kwenye risk. Naomba nisitaje watoto wala idadi

Wakili: Lengai nikurudishe kwenye swali dogo wakati unatoka Hai saa 9 kuja Arusha na hiyo timu yako ulipita wapi

Sabaya: Nilipitia Kia barabara ya Mirerani nikaja Arusha

Wakili: Kwanini ulipita huko usipite barabara ya kawaida Moshi -Arusha

Sabaya: Napitia barabara yoyote kwa usalama wangu kwa sababu natishiwa kuuawa

 

Wakili: Kwanini ulikuwa unatishiwa kuuawa na wewe ni kiongozi wa watu

Sabaya: Kwa sababu ya aina ya majukumu niliyokuwa nafanya siasa za Arusha na Hai

Wakili: Umefika Arusha mlipokuwa mnaenea na timu yako alimkuta shahidi wa nne Hajirin Saad Hajirin, ulimuona?

Sabaya: Ndio nilimuoma hapa mahakamani

Wakili: Wewe unafahamaniana naye

Sabaya: Hapana

 

Wakili: Una ugomvi naye

Sabaya: Kama simfahamu siyo rafiki wala adui

Wakili: Na yule shahidi wa pili katoa ushahidi wake akasema alikuona Shahidi Store (dukani) una ugomvi naye au unamfahamu?

Sabaya: Simfahamu na hapo Shahidi Store sipafahamu.

 

Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura wanashtakiwa kwa makosa matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika duka la Mohamed Saad eneo la bondeni jijini Arusha Februari 9, 2021.

 

Leave A Reply