The House of Favourite Newspapers

Majaliwa Ateta na Staa wa Filamu India

0

 

Huenda waigizaji wa filamu nchini Tanzania wakajiimarisha na kufaidika zaidi na tasnia hiyo, baada ya Serikali kuwawekea urahisi wa kubadilishana uzoefu na waagizaji wa kimataifa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na muigizaji mashuhuri wa filamu za Kihindi kutoka nchini India, Sanjay Dutt ambaye ameahidi kushirikiana na Serikali katika kukuza tasnia ya filamu nchini.

Amekutana na msanii huyo leo Novemba 10, 2021 katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam ambapo amesema Serikali itampa ushirikiano wote kuhakikisha msanii huyo anatimiza malengo ya ziara yake nchini.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa filamu nchini kutumia ujio wa msanii huyo duniani kuimarisha uhusiano pamoja na kujifunza namna bora ya kuboresha kazi zao kupitia yeye na kuweka mipango ya kufanya kazi kwa pamoja.

Pia, Waziri Mkuu amemshukuru msanii huyo ambaye pamoja na mambo mengine ameahidi kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania katika kuendesha mafunzo ya masuala mbalimbali katika tasnia hiyo ikiwemo uandaaji wa filamu kwa kutumia teknolojia ya kisasa hususani kwa vijana.

Tasnia ya filamu inakua kwa kasi duniani na imekuwa sehemu muhimu kwa vijana wenye vipaji vya kuigiza kujiajiri na kuendeleza maisha yao.

Dutt amesema amevutiwa na fursa nyingi zilizoko kwenye sekta ya utalii nchini na kwamba ameahidi kuvitangaza vivutio hivyo na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kwenye ramani ya dunia katika masuala ya utalii.

Mbali na ahadi hiyo, pia msanii huyo amesema atashirikiana na wadau wa filamu nchini wakiwemo waandaaji pamoja na waigizaji kutoa mafunzo na mbinu bora zitakazowawezesha kuboresha kazi zao na hatimaye waweze kupata mafanikio zaidi.

Amesema kuwa katika ziara yake anatarajia kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ambapo atapiga picha kwa ajili ya kuvitangaza ili kuwavutia watu wengi waje Tanzania.

Miongoni mwa vivutio hivyo ni pamoja na mbuga ya wanyama za Serengeti na Ngorongoro.

“Jana nilikuwa Zanzibar nimeona fursa nyingi za uwekezaji hapa Tanzania ikiwemo uwepo wa fukwe nzuri. Nitakwenda kuwashawishi marafiki zangu nao waje kuwekeza. Naipenda sana Tanzania watu wake ni wakarimu na ninatarajia kuja kufanya filamu,” amesema Dutt.

Dutt anayesifika kwa filamu mbalimbali za Kihindi zikiwemo za Hathyar na Zinda anatarajia kutoa filamu nyingine tatu mwaka 2022 za K.G.F Chapter 2, The Good Maharaja, Shamshera

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema kupitia ujio wa Dutt, Wizara inategemea kuangalia maeneo ya kimkakati ambayo wanaweza kushirikiana na msanii huyo ikiwemo uandaaji wa filamu, kuongeza wigo wa masoko ya filamu na matumizi ya teknolojia katika kuikuza sekta ya filamu nchini.

Aliongeza kuwa kupitia Chuo cha Sanaa Tanzania (TaSUBa) Dutt ametoa ushauri wa namna bora ya kushirikina ikiwemo kutoa mafunzo kwa wasanii na waandaaji wa filamu.

“Lengo letu ni kuhakikisha wasanii wetu wanatengeneza filamu ambazo zitakuwa na viwango vya kimataifa na ameahidi kuwaleta wataalamu ili wawasaidie wasanii wetu,” amesema Bashungwa.

Leave A Reply