The House of Favourite Newspapers

Majini yameiba viatu

0

Hii dunia bwana we acha tu, kuna mambo yanabadilika kila kukicha. Jambo ambalo jana ulikuwa ukikatazwa unaweza kukuta kesho unalazimishwa. Au jambo ambalo ulikuwa unalazimishwa wakati ulipokuwa mdogo, kesho yake unalitafuta.

Zamani zilee ukikuta mtu ana nywele fupi unajua huyu polisi au katoka gerezani, siku hizi kila anayekwenda saluni anataka anyolewe kama  katoka magereza. Kunyolewa kipara ilikuwa adhabu kwa watoto wakorofi, siku hizi fasheni.
Miaka michache iliyopita ungemwambia mtu kuwa utamuuzia maji ya kunywa kwenye chupa angekuona wewe mwongo kuliko waongo wote duniani. Zamani mwenye hela anahakikisha anaficha watu wasijue, siku hizi mtu anaweka picha WhatsApp akiwa kashika burungutu la mihela dah.

Lakini kali pia ni hii tabia ya wadada kutembea na nguo za kubadili, anaondoka nyumbani na nguo ya spea. Wiki iliyopita haya mambo ya nguo za ziada yamemtokea rafiki yangu mpaka sasa bado namcheka.
Jamaa yuko vizuri ana mke wake mrembo mstaarabu, ukiwaona pamoja utawaonea wivu. Full malavidavi. Lakini jamaa yangu akiwa peke yake tu bado anapenda visamsing au wengine wanaita nyumba ndogo, wengine wanaita, mpango wa pembeni, basi ndiyo hivyo tena.

Pamoja na uhuni huo anaogopa sana nyumba yake isiharibike, hivyo huwa anajitahidi sana kuficha makucha yake. Siku moja alirudi nyumbani kachelewa  baada ya kutoka kwenye misafara na kisamsing chake. Asubuhi yake wakaamka mapema na mkewe kuelekea kazini, njiani mkewe akamuomba asimame kwenye kaduka fulani anunue kitu.

Jamaa akapaki pembeni mama akashuka.             Wakati mkewe kashuka ghafla jamaa akaona viatu chini ya kiti cha mkewe, moyo ukataka kusimama, akajua ni viatu vya kisamsing cha jana kilisahau maana kilishuka kimelewa chakali, basi akavichukua viatu harakaharaka na kuvitupa mtaroni, kuficha ushahidi kabla mkewe hajaja.

Bibie aliporudi safari ikaanza, ghafla yule mama akauliza, ‘Jamani viatu vyangu vimeenda wapi? Niliviacha chini ya kiti nimevaa kandambili maana virefu mno sasa sivioni’. Jamaa yangu akalazimika kujidai mkali, ‘Sasa wewe unakuwaje na viatu na kandambili? Utakuwa umevisahau nyumbani’’ Mama akapinga akasema nimeingia navyo kwenye gari nilijua nitavivaa nitakapofika kazini, maana virefu mno. Jamaa kabaki kusisitiza, ‘Haya basi tuseme vimechukuliwa na majini.’

Leave A Reply