The House of Favourite Newspapers

Makocha, Manahodha Simba/Yanga Watambiana

0

MAKOCHA na manahodha wa Simba na Yanga leo Machi 7, 2020 wameelezea hisia zao kuelekea mchezo huo wa watani wa jadi utaochezwa kesho Jumapili saa 11:00 jioni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Kocha wa Yanga, Luc Eymael, amesema kuelekea mchezo huo hawakuwa na ratiba rahisi kutokana na kila baada ya siku tatu kucheza mechi ambayo ilikuwa inawalazimu kutofanya mazoezi ya kutosha na wachezaji wengine kuchoka kwani wametumika sana.

 

Eymal alisema hilo la ratiba ngumu lilitokana na mwingiliano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutoa ratiba yao mpya ambayo iliathiri ligi nyingi lakini kwa upande wao wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi kutokana na maandalizi ya kutosha ambayo wameyafanya.

 

“Nimefurahi kuonana na kocha mwenzangu ambaye tunatoka nchi moja lakini maandalizi tuliyoyafanya na wachezaji wangu naamini watakwenda kuyafanyia kazi ili kupata alama tatu ambazo ndiyo malengo yetu,” alisema Eymael ambaye ndiyo mechi yake ya kwanza kukutana na Simba.

 

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul, amesema wamefanya maandalizi ya kutosha yaliyokuwa na mbinu nyingi kulingana na wapinzani wao walivyo na yote hayo ni kuhakikisha wanapata pointi tatu ambazo ndio zitakuwa furaha kwa upande wao.

 

“Kikubwa kwetu maandalizi tumefanya ya kutosha ili kupata ushindi katika mchezo huo ambao tunafahamu ni mgumu na hautakuwa rahisi kwetu kupata ushindi tunafahamu hilo na tumejipanga nalo ili kukabiliana na wapinzani,” alisema Abdul.

 

Kocha wa Simba, Mbelgiji Sven Vandernbroeck amesema wanakwenda kucheza mechi ngumu na kubwa hapa nchini dhidi ya Yanga, na jambo kubwa anategemea kuliona pambano hilo ni ushindani mkubwa kutokana na uimara wa timu zote mbili.

 

“Tumefanya maandalizi ya kutosha na leo Jumamosi jioni tunakwenda kumalizia sehemu ndogo tu, jambo ambalo niwatoe hofu na kuwakaribisha mashabiki wa Simba wote nchini kuja kuipa nguvu timu yao kwani tutawapatia burudani ya kutosha huku tukihitaji ushindi,” alisema Sven.

 

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema: “Tumepokea maelekezo ya kutosha kwa benchi la ufundi na kama wachezaji tumeyapokea na tumejipanga kuyafanyia kazi ili kuwafunga (watani wetu) lakini sambamba na hilo tumejipanga kutoa burudani kwa mashabiki ambao watajitokeza kushuhudia mechi.”

 

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, alisema wamejipanga kuanzia uwanjani kwa maana ya mpangilio wa mashabiki na magari kuingia  na masuala mengine ya msingi.

 

“Kuhusu ujio wa Rais wa CAF, Ahmad Ahmad,  atafika nchini leo Jumamosi kwa ziara ya siku tatu ambayo ndani yake atazungumza na serikali kuhusu maendeleo ya soka nchini na atapata fursa ya kwenda kushuhudia mechi ya Simba na Yanga,” alisema Ndimbo.

Leave A Reply