The House of Favourite Newspapers

Mama Amfanyia Mbaya Mwanaye

0

MWANAMKE mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Emakulata amemfanyia kitu mbaya mtoto wake wa miezi miwili kwa kumtoroka usiku wa manane.

 

Taarifa zinaeleza kuwa mwanamke huyo mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam, alimwacha mwanaye (jina kapuni) hivi karibuni akiwa peke yake ndani ya chumba alichokuwa anaishi.

 

Jambo lililowasikitisha wengi ni pale walipomkuta mtoto huyo akiwa hana chakula na kwamba mama yake alimwachia ujumbe wa maandishi wenye maneno ya kuumiza kuwa:

“Mwanangu sijapenda kukuacha; sina uwezo wa kukulea”.

 

Jeshi la polisi mkoa wa Dar es Salaam, linaendelea kumsaka mwanamke huyo kwa udi na uvumba kwa kutelekeza mtoto ambapo jalada lake limepewa namba STK/RB/2791/20 KUTELEKEZA MTOTO.

Akizungumzia kwa kina tukio hilo Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Ukonga Mazizini, Shina Namba 6, Asha Msuya alisema, alimfahamu mwanamke huyo mapema kabla hajamtelekeza mtoto wake.

 

Asha alisema, miezi miwili iliyopita alimkuta Emakulata akizungukazunguka na mtoto huyo katika mtaa wake ambapo alimuuliza na kubaini kuwa hakuwa na makazi maalumu.

“Aliniambia kuwa yeye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma, amezaa na mume wa mtu anaishi na mke wake maeneo ya Matembele anaiyeitwa Benson Ezron.

 

“Nilipomuuliza kwa nini baba wa mtoto hamhudumii mwanaye aliniambia kuwa, mwanaume huyo hataki kutoa matunzo ya mtoto.

“Mimi kama kiongozi wa mtaa nikamchukua nikiwa na majirani zangu tukaenda kuripoti Kituo cha Polisi cha Stakishari, lengo ni kumsaidia apate haki ya mtoto.

 

“Tulipofika kule tulionana na askari wa Dawati la Jinsia, akatupangia Machi 3, mwaka huu kuwa ndiyo siku ya kujadili suala lake baada ya baba wa mtoto kupatikana na kupewa taarifa.

“Kwa kuwa alikuwa hana sehemu ya kuishi nikamchukua hadi kwangu, nikampatia chumba aishi na mwanaye wakati tunasubiri tarehe ya shauri lake ifike,” alisema mjumbe huyo kwa masikitiko.

 

Aliongeza kuwa, wakati Emakulata akiendelea kuishi pale, usiku mmoja mjumbe huyo alishangaa kusikia mtoto akilia bila kusaidiwa, alipokwenda chumbani kwa mwanamke huyo hakumkuta.

“Nilipoangalia kwa makini nikaona hiyo barua aliyoacha, nikajua ametoroka, roho iliniuma sana, ikabidi kutafuta njia ya kumsaidia mtoto maana alikuwa akilia kwa kiu na njaa.

 

“Kulipokucha ikabidi turudi Kituo cha Polisi Stakishari, tukaandikisha maelezo na kuelekezwa kuwa mtoto huyo tumpeleke Kituo cha Kulelea Watoto Msimbazi,” alisema mjumbe huyo.

Tukio hilo la kusikitisha limelaaniwa na wengi huku lawama za baadhi ya watu zikielekezwa kwa mwanaume aliyemzalisha mwanamke huyo na kugoma kutoa malezi ya mtoto.

 

“Nashauri wakati polisi wanamsaka huyo dada, mwanaume aliyemzalisha anatakiwa kukamatwa haraka ili achukuliwe hatua na kupewa jukumu la kumlea mwanaye.

“Haiwezekani mzigo wa malezi wapewe watu ambao hawahusiki wakati yeye yupo na ana uwezo, hata kama ni mume wa mtu,” alisema Said Hamza mkazi wa Ukonga alipozungumza na Gazeti la Amani.

Stori:Neema Adrian, Amani

Leave A Reply