The House of Favourite Newspapers

Mambo 7 Ya Jakaya Kikwete Kuhusu Maisha Yake ya Sasa

0
Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Khalfan Mrisho Kikwete.

STORI: BRIGHTON MASALU, IJUMAA , HABARI

NI takriban miaka miwili sasa tangu Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Khalfan Mrisho Kikwete aondoke madarakani lakini shauku kubwa ya watu wengi ni kujua aina ya maisha anayoishi mwanasiasa huyo, Ijumaa limechimba na kuibua mambo 7 kuhusu maisha yake ya sasa, tushuke pamoja.
Katikati ya wiki hii, mwandishi wetu alijipa kazi maalum ya kuchimbua kwa ndani ili kuyajua maisha hayo mapya ya Mhe. Dk. Kikwete na katika kulifanikisha hilo, mwanahabari wetu alifanikiwa kuzungumza na mmoja wa watu walio karibu na familia ya Dk. Kikwete aliyeomba hifadhi ya jina lake na kuanika mambo kadhaa ambayo huenda huyajui.

JAMBO LA KWANZA

Kwa sauti ya kujiamini, mnyetishaji huyo aliweka wazi kuwa, jambo la kwanza na muhimu analolifanya Mhe. Dk. Kikwete kwa sasa ni kutoa ushauri wa kisiasa kwa familia yake, mkewe Mhe. Mama Salma Kikwete ambaye hivi karibuni ameteuliwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwa mbunge, pia kwa mwanaye Mhe. Ridhiwan Kikwete ambaye ni Mbunge wa Chalinze. “Mara nyingi amekuwa akiwaelekeza namna ya kuendesha siasa zao kutokana na uzoefu mkubwa alionao kwenye eneo hilo, kama unavyojua ametumika katika nafasi mbalimbali kabla ya kuushika urais, hivyo hilo ndilo jambo kubwa analolifanya,” alisema mtoa taarifa huyo.

JAMBO LA PILI

Jambo lingine ambalo Mhe. Dk. Kikwete analifanya mara kwa mara ni pamoja na kwenda mitoko katika sehemu mbalimbali ya kuhuisha akili (refreshing mind), akiwa na familia
yake hususan wajukuu ambapo hivi karibuni alionekana maeneo ya Mlimani City, akiwa mwenye furaha huku watu wakitumia mwanya huo kumpiga na kupiga naye picha mbalimbali za ukumbusho.

LINGINE P

amoja na mambo mengine ya kidunia, Mhe. Dk. Kikwete hasahau jambo moja muhimu maishani, kumkumbuka Mungu. Iliendelea kuelezwa na chanzo hicho kwamba kiongozi huyo amekuwa akitumia muda wake katika kufanya ibada ikiwa ni katika kujiweka karibu na Mungu wake. “Hafanyi ajizi na jambo la kuswali, tena anaweza kusahau mambo mengine kwa sababu ya umri kuanza kumtupa mkono, lakini linapokuja suala la kuswali, iwe kwenda msikitini au nyumbani, amekuwa mstari wa mbele kusisitiza, hata kwa wajukuu zake wanaopata mafundisho ya kidini chuoni, amekuwa akiwahimiza mno,” alisema mtoa habari huyo.

KUNA HILI PIA

Inatajwa kuwa tangu atoke madarakani, Mhe. Dk. Kikwete amekuwa akijumuika kwa asilimia kubwa kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuhudhuria misiba, sherehe, usafi wa mazingira, michango ya kimaendeleo pale kijijini Msoga (mahali anapoishi) na mambo mengine mengi ambayo wakati akiwa rais, alishindwa kuyashiriki kwa kiwango kikubwa.

CHUKUA HII

Jasiri haachi asili. Inatajwa Mheshimiwa huyo amekuwa akijihusisha na masuala ya kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo yale ya chakula na biashara, huku zao kuu ambalo anatajwa kujihusisha nalo ni Zabibu, huko mkoani Dodoma. “Mheshimiwa analima sana, anayo mashamba ya mazao
mbalimbali, lakini anapenda sana zao la Zabibu na muda mwingi anatumia kuwa mjini Dodoma, lilipo shamba lake, pia analo shamba la mananasi kule Kibaigwa-Bagamoyo na kilimo cha mazao mengine, bila kusahau kwamba anajihusisha na ufugaji, ambapo anao mbuzi, kuku na ng’ombe,” alizidi kuweka wazi sosi huyo.

JIFUNZE KWA HILI SASA

Duru zinaonesha kuwa, Mhe. Dk. Kikwete anapenda kuongeza maarifa kwa kujisomea vitabu mbalimbali kuhusu maisha, kusoma makala za magazeti ya ndani na nje ya nchi, kutazama video za hutuba za viongozi mbalimbali, wahamasishaji wa watu kujikomboa na umaskini. Pia hivi karibuni amekaririwa akiweka wazi mpango wake wa kuanzisha Taasisi ya Mfuko wa Jamii ya Kikwete, yote ni kuhakikisha anayafanyia kazi yale anayojifunza kuhusu maisha. “Huwezi kumkuta akiwa hana kitabu, gazeti au akisikiliza hotuba au mazungumzo yoyote ya kujielimisha,” alisema.

HILI KISIKUPITE “Ni mpenda mazoezi, mara zote anaamka asubuhi na kupasha misuli kwa kukimbia umbali wa mita kadhaa, kuruka kamba na kunyoosha viungo kwa namna mbalimbali, anaamini mazoezi hufukuza maradhi madogomadogo na uzembe,” alisema mgawa ubuyu huyu.

KUTOKA IJUMAA Usipoitesa akili yako ujanani, basi utautesa mwili wako uzeeni. Hakikisha unatumia vyema ujana wako, muda na ratiba zako za kimaisha kuhakikisha unatengeneza mazingira murua kabisa ya kufurahia maisha kwa baadaye kama ilivyo kwa mheshimiwa huyu ambaye wengi sasa hivi wanammisi

Leave A Reply