Mapokezi ya Diamond Dar…mafuriko!

Musa Mateja

USIPIME! Mapokezi ya ‘kichaa’ wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alipotua jijini Dar, juzi na tuzo tano alizojitwalia nchini Marekani yamesababisha mafuriko ya watu na kufungwa kwa baadhi ya barabara na shughuli kusimama, Risasi Jumamosi lilikuwa kwenye msafara.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Diamond alitwaa tuzo tatu za Jarida la African Music (Afrimma) 2015 zilizotolewa Dallas, Marekani kisha akazifuata nyingine mbili za AfricaNafca kutoka Hollywood nchini humo, moja ikiwa; Mwanamuziki Anayependwa Afrika, nyingine; Wimbo Unaopendwa Afrika (Nana).

TUANZIE UWANJA WA NDEGE

Ilikuwa mishale ya saa 8:00 mchana ambapo mashabiki wengi walikuwa wakimsubiri nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar (JNIA) kabla ya kutokea akiwa amezishika tuzo zake hizo tano.
Baadhi ya mashabiki wa nyota huyo, wakiwemo bodaboda kibao, walisababisha mshangao mkubwa uwanjani hapo kutokana na idadi yao huku wakiimba; ‘rais…rais…rais wetu Diamond’. Wengine walikuwa na mabango ya kumsifia na mengine ya kuwakejeli wapinzani wake.

MAFURIKO KAMA LOWASSA, MAGUFULI

“Hivi watu hawa wote wametokea wapi? Wamejuaje kuwa Diamond anatua muda huu? Kweli dogo (Diamond) ni kipenzi cha watu,” alisikika mmoja wa wafanyakazi uwanjani hapo.
Mwingine alisema: “Huu kweli ni mwaka wa tofauti, eti hata Diamond naye ana mafuriko! Mimi nilijua ni Lowassa (Edward) na Magufuli (John) tu.”

Baada ya kusalimiana na mashabiki wake kisha mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’, uongozi wake wa Wasafi Classic Baby (WCB) na ndugu zake wengine, Diamond alizungumza na vyombo vya habari akishukuru mashabiki kwa kumpa sapoti hadi akanyakua tuzo hizo.

MSAFARA WAANZA

Baada ya kuona msongamano mkubwa, Diamond aliamrishwa na mashabiki wake atembee ambapo alitii kisha wakaingia barabarani kuanza msafara.

Msafara huo ulikuwa ukielekea kwenye Ukumbi wa Escape One, Mikocheni jijini Dar kwa kupitia Barabara ya Nyerere kabla ya kuzuiliwa na askari waliomwamuru apande kwenye gari ili kuepusha msongamano.
Baada ya kutii agizo hilo, Diamond aliendelea na msafara wake kupitia Barabara za Mandela, Uhuru, Lumumba, Morogoro, Kawawa kisha msafara ulikata kushoto kuelekea nyumbani kwao, Tandale.

Baada ya Tandale, alielekea Escape One ambapo alizungumza tena na wanahabari kisha kupiga picha na mashabiki wake akiwa na tuzo hizo.Kwenye barabara hizo zote kulikuwa na mafuriko kiasi cha baadhi ya watu kuuliza ni mgombea gani anayefanya kampeni barabarani muda huo!

NDANI YA ESCAPE ONE

Ndani ya Escape One, mashabiki waliendelea kusherehekea ushindi wa Diamond kwa kunywa, kula na kuserebuka na muziki hadi muda mbovu.

TUZO NYINGINE YANUKIA
Akiwa Escape One, Diamond alisema kuwa kuna tuzo nyingine inanukia ya MTV Europe Music ambapo alipigiwa simu na kuelezwa kwamba ameteuliwa kushiriki akiwa msanii pekee kutoka barani Afrika zitakazofanyika jijini Milani, Italia, Oktoba 28, mwaka huu.

Kufuatia siku kubaki chache, Diamond aliwaomba mashabiki wake wampigie kura kwa wingi ili achukue tuzo hiyo muhimu itakayomkutanisha na mastaa wengi wakubwa duniani.

“Fursa ya kuwepo kwenye tuzo hiyo itaniwezesha kukutana na mastaa wakubwa wa Marekani ambao nao wanashiriki. Nitahakikisha nazungumza na mmoja wa mastaa hao juu ya muziki wa Tanzania na ikiwezekana nifanye bonge la kolabo ili nizidi kuitangaza zaidi Bongo,” alisema Diamond almaarufu Dangote au baba Tiffah.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Loading...

Toa comment