The House of Favourite Newspapers

Mbowe Amtuhumu Spika Ndugai Kugomea Mil. 43 za Wabunge Kumtibu Lissu

0
Mbowe akizungumza na wanahabari.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametua nchini akitokea nchini Kenya anapomuuguza Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na kufunguka kwamba Spika Job Ndugai amezuia Sh. Milioni 43 zilizochangwa na wabunge kusaidia matibabu huku akivituhumu vyombo vya ulinzi na usalama kwamba vinahusika kumpiga risasi mbunge huyo, anaandika Hellen Sisya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mbowe amesema licha ya fedha hizo kuchangwa na wabunge wote wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , mpaka sasa hazijatolewa kwa ajili ya kugharamia matibabu ya Lissu.

Amesema licha ya kuzungumza na Spika Ndugai na kukubaliana naye kwamba ampatie utaratibu wa kuzituma moja kwa moja hospitalini nchini Kenya anapotibiwa Lissu, lakini bado hilo halijafanyika mpaka sasa.

Mbowe ambaye alirudi nchini jana jioni, amesema kuwa siku Lissu alipopigwa risasi mjini Dodoma, alifanya kikao na spika pamoja na Waziri wa Afya, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kumsaidia Lissu.

Hata hivyo, Waziri Mwalimu pamoja na spika walitaka Lissu akatibiwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kama itashindikana ndipo apelekwe nchini India.

Mbowe amesema baada ya kuona hali ya Lissu ilivyo alitaka apelekwe nchini Kenya, jambo ambalo lilipingwa na spika pamoja na waziri na wakasema kama ni hivyo wao hawatahusika na gharama za matibabu hayo.

Akifafanua mbele ya waandishi wa habari, Mbowe ameongeza kuwa ni jambo la ajabu kuona fedha zilizochangwa na wabunge, spika ameendelea kuzikalia badala ya kuzitoa ili zisaidie kufanya kazi ya kumtibu Lissu.

“Michango ya wabunge wote Tsh  43 milioni ambazo Bunge walikata posho zetu ikiwamo ya Tundu Lissu hatujapewa hadi leo…. Spika Ndugai aliniambia niandike barua Lissu apelekwe India, kweli mbunge anaumwa unasema chama kitume maombi, huu utaratibu umeanza lini?”, alisema Mbowe.

Kuhusu tuhuma za nani aliyehusika kumpiga Lissu risasi, Mbowe aliweka bayana kwamba mtuhumiwa namba moja ni vyombo vya ulinzi na usalama ingawa hakumtaja mtu kwa jina.

Aidha, kuhusiana na kauli ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma aliyoitoa jana kwamba suala la Lissu viachiwe vyombo vya dola, amesema yeye hana utalaam huo na kwamba bora akae kimya asubiri masuala ya kisheria ambayo yanamhusu.

Hata hivyo , aliwataka Watanzania kutoamini baadhi ya taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na kwamba wanaozitoa hawajaonana na Lissu na kuzungumza naye.

Kuhusu kauli ya serikali iliyotolewa na Waziri Ummy  kusema ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu popote duniani endapo familia ya Lissu itatuma maombi, Mbowe amesema kuwa hilo halitawezekana kwani hata nchini Kenya serikali ingeweza kusaidia na akatibiwa huko.

Mbowe ameahidi kwamba siku Lissu akirejea nchini, ataanika kila kitu kilichompata ili Watanzania wapate ukweli na undani wa tukio lote lilivyotokea mjini Dodoma.

 

Mbowe: Ndugai Hajatoa Tsh. 43M Michango ya Wabunge Kumtibu Lissu

Leave A Reply