The House of Favourite Newspapers

Mbowe, Wenzake Wahukumiwa Jela au Kulipa Faini

0

Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo imewahukumu viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe katika kesi ya jinai iliyokuwa ikiwakabili kulipa faini jumla ya Tsh milioni 350 au kwenda jela miezi mitano.

 

Akisoma hukumu hiyo hii leo, Machi 10, 2020, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, aliwaondolea washtakiwa wote shtaka la kwanza la kula njama, na kufanya wabakie na mashtaka 12 katika kesi hiyo kabla ya baadaye kutiwa hatiani.

 

Hakimu Simba amesema katika shtaka la pili la uchochezi iliyokuwa ikiwakabili watuhumiwa wote, kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Tsh milioni 10 au kwenda jela miezi mitano.

 

Katika shtaka la 3 hadi 6, mahakama imeamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Tsh milioni 10 au jela miezi mitano. Hata hivyo shtaka la 9, 10 linamhusu Mbowe peke yake, hivyo kila kosa atalipa Tsh milioni 5 au jela miezi mitano na katika shtaka la 11 atalipa faini ya Sh 10 milioni.

 

Kwa ujumla

Hakimu Simba amewahukumu John Mnyika, Salim Mwalimu, Easter Matiko na Vicent Mashinji (ambaye kwa sasa amejiunga na CCM) kila mmoja kulipa faini ya shilingi milioni 30 au kwenda kutumikia kifungo cha miezi mitano jela kila mmoja.

John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee na Ester Bulaya wao walihukumiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 40 kila mmoja au kwenda jela miezi mitano huku Mbowe akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 70 au kwenda jela miezi mitano.

 

Washtakiwa hao walidaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui na Barabara za kawawa na Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni.

Kabla ya hukumu hiyo, jeshi la polisi lililazimika kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo, kwa lengo la kusikiliza hukumu hiyo ambapo askari waliokuwa kwenye sare zao wakiwa na silaha pamoja na askari kanzu, walitoa tangazo la kuwataka watu wote waliokuwa nje ya mahakama hiyo kutawanyika.

 

Waliokaidi agizo hilo walijikuta wakiishia kwenye mikono ya jeshi hilo, ambapo baadaye hali ilitulia mahakamani hapo na kesi ikaendelea kunguruma hadi majira ya saa 11 jioni hukumu ilipohitimishwa.

 

Kesi hiyo ilitakiwa kutolewa hukumu kuanzia majira ya saa 4:30 asubuhi lakini ikasogezwa mbele na kuanza kusomwa saa 7:30 mchana ambapo mahakama ilianza kufanya mapitio ya ushahidi wa pande zote mbili, kabla ya kuwatia hatiani washtakiwa wote katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili.

 

Kosa la 2 wote 10m

Kosa la 3 wote 10m

Kosa la 4 wote 10m

Kosa la 5 Mbowe 10m

Kosa la 6 Mbowe 10m

Kosa la 7 Mdee 10m

Kosa la 8 Heche 10m

Kosa la 9 Mbowe 5m

Kosa la 10 Mbowe 5m

Kosa la 11 Mbowe 10m

Kosa la 12 Mbowe Msigwa 10m

Kosa la 13 Mbowe Bulaya 10m

Au miezi 5 jela.

 

Leave A Reply