The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni-34

0

ILIPOISHIA

“Kwani wewe hunikumbuki mimi, si ndiye niliyewaingiza ndani ya pango hili hadi pale mlipochangukana?”
Nilipomtazama vizuri, nikakumbuka. Alikuwa ndiye yeye aliyetuingiza ndani ya pango lile.
SASA ENDELEA…

“Umetueleza mkasa wa ajabu sana. Ndani ya pango kama hili hakuwezi kukosekana majini lakini habari iliyotushitua ni ya wenzako kuuawa pamoja na habari ya huyo msichana uliyotueleza kuwa anaishi ndani ya pango hili kwa miaka minne,” mtu huyo akaniambia.

“Yupo. Ndiye aliyekuwa akitusaidiaa kwa chakula tangu tulipopotea humu ndani. Ameletwa na huyo jini na ametuambia jini huyo anaitwa Kaikush,” nikaendelea kuwaambia.
Kwa vile niliwaeleza pia kuhusu mwenzangu aliyeuawa dakika chache zilizopita na kunifanya nitoke mbio, watu hao walitaka nikawaoneshe huyo mtu.

“Lakini nataka kuwatahadharisha kuwa kama huyo jini bado yuko pale itakuwa jambo la hatari sisi kwenda,” nikawaambia.“Tunaweza kupata msaada kama kutatokea hatari yoyote. Huu waya unaouona ni wa simu,” mtu huyo aliniambia na kunionesha simu aliyokuwa ameishika mkononi ambayo ilifanana na radio call.
Akaendelea kuniambia.

“Tukipiga simu hii kuna watu watatufuata haraka na kutupa msaada.”
“Watajuaje mahali tulipo wakati hili pango lina njia nyingi?”

“Huu waya unaouona umeanzia nje ya pango. Wakiingia humu wataufuata waya huu. Huu waya ndiyo utakaowatambulisha tuko wapi. Faida mojawapo ya waya huu ni kutuongoza tusipotee. Kama tunataka kurudi tunaufuta ulipopita hadi tunafika nje ya pango. Bila waya huu tunaweza kupotea humu humu na tusijulikane tuko wapi.”
“Haya twendeni niwapeleke,” nikawaambia.

Tukaanza safari ya kuelekea pale mahali alipouawa yule mwenzangu wa mwisho.
Wakati tunatembea watu hao walinieleza kuwa walianza juhudi za kututafuta tangu siku tatu zilizopita.
“Leo ndiyo tumefanikiwa kufika hapa na kukuona wewe baada ya kubuni mbinu ya kuingia na simu pamoja na huu waya ambao unaonesha tulipopita. Hata kama tutakufa humu ndani, watu wanaweza kufuatilia huu waya na kujua tuko wapi,” mmoja wa watu hao akaniambia.

Tulitembea mwendo mrefu sana hadi tulipofika pale mahali. Ule waya ulikuwa ukizidi kujivuta kadiri tulivyokuwa tunakwenda. Inaelekea ulikuwa waya mrefu sana.

Tuliukuta mwili wa yule mwenzangu umelala chini ukiwa umetobolewa utosi. Tuliweza kumuona vizuri kutokana na mwanga wa zile tochi zilizokuwa kwenye kofia walizokuwa wamevaa wale watu.
Baada ya kuuona ule mwili, wenzangu hao sasa waliamini kuwa humo ndani hakukuwa salama.
“Na huyo msichana uliyetuambia yuko wapi?” Mtu aliyekuwa ameshika bunduki akaniuliza.
“Tufuate njia hii hii tutafika mahali anapoishi,” nikawaambia.

“Ngoja kwanza nipige simu niwaarifu wenzetu,” yule mtu aliyeshika simu akasema.
Alipiga simu. Simu yake ilipopokelewa alizungumza na mtu wa upande wa pili na kumueleza kuwa wameona mtu mmoja.

“Ametueleza kuwa wenzake wameuawa,” akasema.
“Wamekufa au wameuawa?” Sauti ya mtu kutoka simu ya upande wa pili ikasikika ikimuuliza.
“Ametumbia kuwa ameuawa na tumeshuhudia moja ya maiti za mwenzake aliyeuawa leo.”
“Wameuawa na nani?”

Kutokana na swali hilo mtu huyo akaeleza kuhusu mkasa wa Kaikush na Faiza ambaye bila shaka ulimshangaza mtu aliyekuwa akielezwa.“Ni maajabu ya mwaka! Yaani humo ndani ya pango kuna msichana anaishi kwa miaka minne?”
“Tumeelezwa kwamba yupo na huyo jini aliyemleta pia anakuja mara kwa mara.”

“Sasa ili msadikishe hayo maelezo awaeleze mahali alipo huyo msichana ili mumfuate.”
“Sawa. Tutafanya hivyo.”

Mtu huyo akakata simu na kuniambia.
“Sasa tupeleke kwa huyo msichana.”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply