The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu-28

0

A spear in My Heart
ILIPOISHIA…
Catarina amekutana na Craig Andreson mzungu kutoka kampuni ya uanamitindo ya Fonex Modeling ya Afrika Kusini na amevutiwa na uzuri wa msichana huyu na kumweleza kwamba kwa muonekano wake angeweza kushiriki mashindano ya uanamitindo na alikuwa tayari kumsaidia jambo linalomfurahisha Catarina kupindukia.

Mzungu huyo anakwenda mbele zaidi na kumweleza kama angekubaliana na kile alichomweleza mkataba maalum ungeandaliwa na Catarina kuweka saini yake jambo linalozidi kuichanganya akili ya Catarina, anaamini kwamba ndoto aliyokuwa nayo akiwa mtoto mdogo sasa ilikuwa ikienda kutimia.

Anawaeleza wazazi wake nao wanakubaliana na kuomba kuonana na Mzungu huyo ambaye anaongea mengi huku akiwahakikishia usalama wa mtoto wao ndipo mkataba unasainiwa na Catarina anajiandaa kwa safari. Wiki moja kabla ya kuondoka anakwenda kumtembelea Kevin shuleni kwao kisha kumweleza habari hizi ambazo anazipokea kwa furaha akitaka Catarina aachiwe afanye alichoona kinampa furaha.

Wakiwa katika maongezi wasiwasi unamwingia Kevin haamini kama Catarina atarejea kwani alikuwa mzuri mno jambo ambalo Catarina mwenyewe anamhakikishia kwamba hakuna mwanaume ambaye angeweza kumtoa kutoka kwake. Wanakumbatiana na wote wanalia kwa uchungu, kutengana kuliwasikitisha.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…

INGAWA Kevin alimuunga mkono Catarina, jambo ambalo halikutarajiwa na wengi, moyoni mwa Catarina kulikuwa na huzuni, kitendo cha kutengana na mvulana aliyempenda kiasi kile kiliuumiza sana moyo wake, hakutaka iwe hivyo, angekuwa na namna nyingine ya kuitimiza ndoto yake akiwa nchini angeichukua lakini haikuwepo, ilikuwa ni lazima aondoke Tanzania kwenda kufukuzia ndoto ya maisha yake nchini Afrika Kusini.
Kitu pekee kilichompa wasiwasi Kevin ni umbali kati yao, msemo wa Kisichokuwepo machoni na moyoni hakipo, ulimsumbua sana, kuna wakati alihisi mpenzi wake waliyeahidiana kuzitunza bikra zao pengine angekutana na wanaume wengine nchini Afrika Kusini, matajiri na wenye ushawishi, ambao wangekuwepo kwenye ulimwengu alikuwa anakwenda kuishi na mwisho kabisa angeamua kumuacha.
Maisha bila Catarina kwake yalionekana ni kitu kisichowezekana, alishamruhusu msichana huyo kumwingia moyoni mpaka kwenye kina cha chini kabisa, safari ya mapenzi waliyosafiri pamoja ambayo walikuwa na umri mdogo ilikuwa na kumbukumbu nyingi zilizowafunga pamoja, ambazo hakuna hata mmoja kati yao angeweza kuzisahau.
Fikra za kuachwa na Catarina zilimuumiza mno Kevin, mara zote akibishana na moyo wake kuwa msichana aliyempenda kiasi hicho asingeweza kumtendea ubaya wa aina hiyo, hiyo ndiyo ikabaki imani yake, kwamba Catarina alikuwa anakwenda Afrika Kusini katika Jiji la Johannesburg kutafuta maisha tu na mambo yakimwendea vizuri angefanya mpango ili Kevin aungane naye, hivyo ndivyo walivyokubaliana.
Taratibu za safari zilipokamilika, wiki mbili baadaye, Catarina alisindikizwa na wazazi wake hadi Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere ambako aliagana na familia yake na kupanda ndege akiwa na Graig Anderson, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda ndege akisafiri nje ya nchi yake, tena akiwa ameketi kwenye daraja la wafanyabiashara ambalo kwa kiingereza huitwa Business Class.
Waliongea mengi wakiwa angani, Graig Anderson akimweleza Catarina juu ya kazi aliyokuwa anakwenda kufanya, vishawishi vyake hasa matumizi ya dawa za kulevya ambazo wanamitindo wengi walizifanya ni ulevi na kuharibu kabisa maisha yao ya baadaye, pia ufuska na mabilionea wa dunia ambao huwa tayari kulipa kiasi chochote cha fedha ili mradi tu wafanye ngono na mwanamitindo maarufu.
“Thank you Graig! Why are you so nice to me?”(Ahsante Graig! Kwa nini unakuwa mwema kiasi hicho kwangu?)
“I like you! You are so beautiful Catarina, if you utilize your beauty well, for sure you are going to die a very rich woman!”(Nakupenda! Wewe ni mzuri Catarina na kama utautumia uzuri wako vizuri, basi hakika utakufa mwanamke tajiri sana!)
“Really?”(Kweli?)
“Yes!”(Ndiyo!)
“Are you sure I am going to sign the agreement?”(Una uhakika nitasaini mkataba?)
“Count that one done!”(Hesabu hilo limekwishafanyika!)
“How can I believe?”( Nawezaji kuamini?)
“I have a lot of influence in the organisation!”(Nina ushawishi mkubwa ndani ya shirika!)
“I will be happy, you know I said goodbye to my friends, all they know is I am going to be an International Super Model, I therefore, will not take anything for an answer except signing the agreement” (Nitafurahi, unajua nimewaaga marafiki zangu, wanachojua ni kwamba ninakwenda kuwa mwanamitindo wa kimataifa, kwa hiyo sitakubaliana na jibu lolote isipokuwa kutia saini mkataba!)
“I have told you to count that done!” (Nimekwishakuambia uelewe hilo limekwishafanyika)
“Thank you, are you married Craig?”(Ahsante, Graig una mke?)
“No! I am single!”(Hapana! Sijaoa!)
“Why?”(Kwa nini?)
Badala ya kujibu swali hilo Craig aliinamisha kichwa chini, aliponyanyuka kumwangalia Catarina, machozi yalikuwa yakimbubujika, akachukua kitambaa na kuanza kujifuta huku Catarina akionyesha mshangao na kuomba msamaha kama swali alilouliza lilikuwa limemkwaza.
“She died!”(Alikufa!)
“Who?”(Nani?)
“My wife, just after our honeymoon!”(Mke wangu, muda mfupi tu baada ya fungate letu!)
“What happened?”(Nini kilitokea?)
“A terrible motor accident!”(Ajali mbaya ya gari)
“Ooh sorry! I didn’t mean to hurt you, was just trying to be a little curious!”(Ooh samahani! Sikumaanisha kukuumiza, nilikuwa najaribu kuwa mdadisi kidogo!)
“It is okay, I loved her so much!”(Hakuna shida, nilimpenda mno!)
Kwa mara ya kwanza maishani mwake Catarina alimuwekea Craig mkono begani akimbembeleza mpaka akaacha kulia na kuendelea kuelezea kuhusu maisha yake baada ya kufiwa na mkewe, kwamba aliamua kuzunguka huku na kule duniani akifanya kazi yake ya kutafuta walimbwende ambayo ilimuondolea kumbukumbu za mke wake aliyekuwa na miaka mitano kaburini siku hiyo.
Alimweleza Catarina juu ya utajiri aliokuwa nao na heshima aliyopewa kote duniani sababu ya kuwasaidia warembo wengi kutimiza ndoto zao, alipomtajia idadi ya warembo wa kimataifa waliopitia mikononi mwake na kufikia mpaka hatua ya kutambulika kila kona duniani wakitengeneza mamilioni ya dola, Catarina alibaki mdomo wazi na kujiona ni mwenye bahati kupindukia kukutana na mwanaume huyo aliyemzidi umri mara mbili.
“I will help you to achieve your goal in life!”(Nitakusaidia kutimiza lengo lako maishani!)
“Thank you Craig! For sure you are an angel sent from heaven specifically for me!”(Ahsante Craig! Kwa hakika wewe ni malaika uliyetumwa kutoka Mbinguni kwa ajili yangu!)
“Mention not!”(Usijali!)
Saa tatu baadaye wakiwa bado wanaendelea kuongea mambo mbalimbali, Catarina akiwaza uanamitindo tu na namna ambavyo angefanikiwa maishani mwake bila kumfikiria Kevin, ndege ilianza kushuka taratibu wakitangaziwa kufunga tena mikanda tayari kwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa O.R. Tambo, Catarina alipotupa macho nje kupitia dirishani alianza kuona majengo marefu ya Jiji la Johannesburg, hakuamini kirahisi kwamba alikuwa ni yeye.
“Am I dreaming?”(Ninaota?) alijiuliza mwenyewe bila kupata jibu.

Je, nini kitaendelea? Nini kitatokea Afrika Kusini kati ya Catarina na Craig? Je, mafanikio anayoyafikiria atayapata au amejiingiza kwenye matatizo? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply