The House of Favourite Newspapers

Muziki Sio Uhuni, ni Fursa,

0

MUZIKI ni ala zilizounganishwa ili kutengeneza kitu ambacho kinaitwa burudani.

Muziki wa Tanzania kwa upande wa Bongo Fleva na Hip Hop, ulianza miaka ya 1990 baada ya kuibuliwa na waasisi mbalimbali waliokuza muziki huo akiwamo Mike Mhagama aliyekuwa mtangazaji wa redio one Tanzania.

Muziki ulipoonesha njia ya ajira uliamsha hisia za wafuatiliaji kiasi cha kuwafanya vijana wengi kujiingiza na kuanza kurekodi kazi zao.

Kwa kipindi hicho, wapo wasanii ambao walianza na kutambulika kwa kuachia ngoma kali ambazo zilikubalika kwa mashabiki wao kiasi cha kuendelea kufuatiliwa.

 

Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya, wapo walioanza mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kukubalika.

Wasanii kama Dully Sykes, TID, Jay Moe, Ngwair, Daz Nundaz, Madee, Mandojo na Domo Kaya, Mr. Blue, Dudu Baya, Juma Nature, Ali Kiba, A.Y., G.K., Q Chillah, Mwana FA, Lady Jaydee, Ray C bila kuwasahau Sister P, Zay B na wengine wengi.

Mmoja wa waanzilishi wa Hip Hop ya Tanzania ni Joseph Mbilinyi ‘Mr. II’ pia anajulika kama Sugu ambaye alitoa kibao chake cha kwanza maarufu cha Bongo Fleva, Ni Mimi mnamo 1995.

 

Mr. II bado yupo hadi leo na rekodi yake ya mwisho ni Coming of Age, aliyoitoa mnamo 2007.

Ndani ya Hip Hop wapo wasanii ambao nao waliamini kuwa mwana Hip Hop, lazima uwe mgumu na si kufanana na ‘wabana pua’, hivyo walijiingiza kwenye mambo ambayo yalionyesha dhahiri ni uhuni ikiwemo kuimba mashairi yenye sentesi tata ndani yake.

Lakini tukirudi kwa wasanii wenyewe, wapo ambao waliamini kuwa, msanii ili utoboe na kufika mbele zaidi ni lazima uwe na mtazamo wa kihuni na kubadili aina ya maisha.

Wapo ambao walihamia kwenye ulevi kwa lengo tu la kutafuta stimu na wengine sasa wakatopea kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.

Baadhi ya wasanii kama Rashid Makwiro ‘Chid Benz’, Abubakar Katwila ‘Q Chillah’, Rehema Chalamila ‘Ray C’, Isack Waziri ‘Lord Eyez’, Ferooz na wengine kibao, ambao walipitia wakati mgumu na kuupoteza muziki wao kwa kipindi hicho.

Wengine waliamni kuwa usanii ni kuchora tatoo, kuvaa milegezo au nguo za utupu ili muziki wako utoke, kumbe muziki ni kipaji, ubunifu na kujituma.

 

Si kwa hapa Bongo tu hata mataifa ya nje, nako wapo wasanii wanaoamini njia kubwa ya kutoboa ni kuendekeza uhuni, kama hivyo kuchora tatoo mwili mzima, staili ya maisha na hata ulevi hasa wa madawa ya kulevya.

Nani anamkumbuka mwanamama aliyekuwa na kipaji kikali kutoka nchini Marekani, Whitney Houston ambaye alisikika sana miaka ya nyuma na ngoma zake kama I will always Love You, I have Nothing, Try on My Own na nyingine kibao, lakini sasa hayupo duniani kutokana na madawa ya kulevya.

 

Wapo wasanii wengi tu wa nje ambao mpaka sasa bado wanaamini kutoboa kwenye muziki lazima kuendekeza uhuni kumbe sivyo.

Turudi Bongo sasa, wapo wasanii ambao walitoboa bila hata kupita kwenye masu­ala ambayo ni kinyume na maadili na bado mpaka sasa wa­naendelea kupep­ea.

 

Jaydee ndiye msanii wa kwanza kurekodi albamu yenye gharama kubwa mno kuliko zote tangu kuanza kwa muziki wa kizazi kipya kwa kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ndiye aliyeanza kupiga video na Benchmark Production kwa kipindi hicho jambo ambalo haikuwa rahisi sana kufanya kazi na kampuni hiyo.

 

Jaydee na A.Y. ni wasanii wa mwanzo kabisa kuthubutu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania katika kufanya muziki na wasanii wa nchi za nje.

Hapo ndiyo tujue kuwa muziki ni biashara na si uhuni kama watu walivyojijengea fikra hizo.

Ninajaribu kujenga hoja kuwa, muziki ni kazi kama kazi nyingine, ni biashara kama zilivyo biashara zingine na ndiyo sababu mpaka sasa katika kizazi cha miaka hii kwenye muziki, wapo waliotajirika kupitia muziki na bila hata kupita kwenye njia mbovu.

 

Msanii kama Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz amefanikiwa kuupeleka mbali muziki wa Tanzania nje ya nchi kwa kiasi kikubwa.

Kupitia Lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), ameweza kuzalisha hata vipaji vingine vikali ambavyo vinautangaza vizuri muziki wa Bongo kama vile Ray­van­ny, Mbosso Khan, Queen Darleen, Lava Lava na sasa Zuchu ambaye amekuwa akisifika ku­piga mbizi za kutosha na hata kuliteka anga la kimataifa.

Si yeye tu wapo wasanii wengi wa muziki wa kizazi cha sasa ambao wamekuwa wakisifika kufanya kazi kali kama vile Harmonize, Rayvanny, Zuchu, Mbosso, Aslay, Nandy, Maua Sama, Lulu Diva, Linah na wengine kibao.

Katika kipindi hiki, rundo la wasaniii wa muziki wa Bongo Fleva wali­batizwa kama ‘wabana pua’, waliongezeka na kuigana kupita kiasi. Watayarishaji wa muziki huu waliongeza maradufu ubunifu na Bongo Fleva, ilianza kuchukua miundo mbalimbali ya muziki mingine kama vile Kwaito, Zouk Rhumba, Singeli, Raggae, muziki wa Nige­ria hasa waliiga na kadhalika.

NINI KIFANYIKE?

Wasanii wanatakiwa waelewe kuwa, muziki ni biashara tena ni mtaji mkubwa wa kuendesha maisha na sio uhuni kama jinsi dhana hii ilivyojijenga kwenye vichwa vya watu walio wengi hasa wasanii.

Biashara hii inahitaji kujituma, kujitoa, kujichanganya, kuchangamka, ubunifu, kukubali kukosolewa na mengine mengi.

Wasanii fanyeni kazi ambayo mmeona ndiyo vipawa vyenu hayo mengine ni ya ziada tu.

Kibiashara!MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply