The House of Favourite Newspapers

Mwanamuziki Anayeishi Kimateso, Aanza Kusaidiwa

0

MWANAMUZIKI wa Shikamoo Jazz, Idd Said Nyangala ‘Baba Sauda’ ambaye gazeti hili la UWAZI toleo namba 1202 la Juni 23 mwaka huu, lilitoa habari kuumwa kwake na kumfanya aishi mazingira magumu, amelishukuru UWAZI pamoja na Global Tv, ambayo ilirusha habari yake hewani na kuwafikia wasamaria wema ambao wameanza kumsaidia.

 

Mwanamuziki huyo amesema baada ya taarifa zake kuruka hewani, hata ndugu zake waliokuwa hawajui kuwa anaumwa kwa kiwango hicho, walifunga safari wengine kutoka mbali na kwenda kumjulia hali.

“Nalishukuru sana gazeti la Uwazi na Global Tv kwa kusaidia kurusha taarifa zangu ambazo zimewafikia ndugu na jamaa ambao wameanza kuja kunijulia hali.

 

“Kikubwa zaidi nawashukuru wasamaria wema ambao wameanza kujitokeza na kunisaidia pesa ambazo zimeanza kunisaidia baadhi ya mahitaji ikiwemo kupunguza kodi ya nyumba na kununua dawa.

Nawaomba wazidi kunichangia ili niweze kwenda kwenye hospitali kupata matibabu zaidi,” alisema Nyangala.

 

Akiwataja waliomchangia pesa hizo, Nyangala amesema mmoja wa Tanzania aliyeko nchini Uingereza ambaye amemchangia shilingi 33,000/ na Mchungaji mmoja aliyeko nchini humo na mwingine ni raia wa Burundi anayeishi nchini humo ambaye ameahidi kumsaidia.

 

Amemshukuru pia msamaria mwema mwingine kutoka Mwanza ambaye amemtumia kiasi cha shilingi laki moja na kusema anamuomba Mungu awabariki sana”, alisema mwanamuziki huyo.

Akiwa ameanza kusaidiwa, Nyangala amewaomba wasanii wenzake, Diamond Platnumz, Ally Kiba na wengineo kumsaidia.

 

Pamoja na wanamuziki hao, amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumsaidia ili afya yake irudi kwenye ubora wake ili aweze kuendelea na ujenzi wa taifa.

Leave A Reply