The House of Favourite Newspapers

Namungo: Tulichofanyiwa Siyo Fitina Za Soka, Ni Uhalifu

0

UONGOZI wa Namungo umesisitiza kuwa kile kilichofanywa na wenyeji wao nchini Angola, Clube Desportivo 1º de Agosto, si fitina za soka bali ni uhalifu wa kupangwa ambao unapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

 

Licha ya hapo mwanzo kupanga kurejea nchini juzi Jumapili, lakini Namungo mpaka jana asubuhi walikuwa bado hawajaondoka nchini Angola, walipokwenda kwa ajili ya mchezo wa mtoano Kombe la Shiikisho Afrika dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto.

Mchezo huo ulipaswa kuchezwa juzi Jumapili, lakini ulifutwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya wachezaji wa Namungo kufika Angola na kukumbana na matukio mbalimbali yaliyotafsiriwa si ya kimichezo huku ikidaiwa wachezaji wao watatu wana maambukizi ya corona.

 

Akizungumza na Spoti Xtra kuhusiana na sakata hilo, Ofisa Habari wa Namungo, Kindamba Namlia, alisema: “Ni kweli tulipaswa kusafiri siku ya Jumapili ili kurejea nyumbani Tanzania, baada ya mchezo wetu dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto kufutwa na CAF, lakini tulilazimika kubadili ratiba hiyo.

 

“Hii ni kutokana na kuchelewa kuwasili kwa wenzetu wanne, ambao ni wachezaji, Lucas Kikoti, Hamis Mgunya, Fredi Tangaru na Ofisa Mtendaji Mkuu, Omary Kaya ambao waliwekwa chini ya ulinzi kutokana na madai ya kugundulika kuwa na virusi vya Corona.“

 

Kiukweli kitu walichokifanya wenyeji wetu sio fitina za mpira kama ambavyo watu wengi wanalichukulia, bali kilichotokea ni uhalifu wa kupanga ambao umeshirikisha mamlaka mbalimbali za nchi ya Angola.”

STORI: JOEL THOMAS, DAR

Leave A Reply