The House of Favourite Newspapers

Namungo Wawekwa Karantini Angola, Wanyang’anywa Passport

0


MSAFARA wa watu 32 wa Klabu ya Namungo ya Tanzania umezuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda nchini Angola baada ya mamlaka za nchi hiyo kudai kuwa wachezaji watatu na kiongozi mmoja wamepimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

 

 

Mpaka tunaenda hewani, timu ilikuwa bado ipo uwanja wa ndege huku utata ukitawala kutokana na mamlaka za nchi hiyo kutaka msafara mzima ama urudi Tanzania au uwekwe karantini. Lakini mwisho wa siku imeamriwa msafara mzima wa klabu hiyo kuweka karantini kwa siku tatu.

 

 

Namungo ipo Angola kuchuana na Clube Desportivo 1º de Agosto katika mechi ya Kombe la Shirikisho ambayo ilipangwa kupigwa kesho Jumapili, Februari 14.

 

 

Mwenyekiti wa Namungo FC Hassan Zidadu Kungu amesema tangu wameingia Angola wanasumbuliwa kwa kisingizio cha Corona.

 

“Baada ya hapo wakataka kutupeleka karaantini tukakataa kwa sababu sisi hatuna maambukizi. Wakaja askari wasiopungua 60 (wanajeshi) wakatulazimisha kuingia kwenye basi wakatuambia wanatupeleka kwenye hoteli ambayo serikali imelipia.

 

“Wametutoa mjini tumetembea umbali wa saa 2:30 tupo nje kabisa ya mji. Tumeletwa kwenye hospitali ya jeshi, timu tunayoenda kucheza nayo ni ya jeshi. Baada ya kufika hapa (hospitali ya jeshi) walitulazimisha kuingia kila mmoja kwenye chumba chake tukae kwa muda wa siku tatu, tukakataa kushuka kwenye basi. Askari wakaamuru basi tulilopanda lifungwe halafu wao wakaondoka.

 

“Kwa hiyo tupo ndani ya basi tumefungiwa na wao wameondoka, kibaya ni kwamba tangu tumeingia hatujanywa hata maji na hatujui tutapata wapi chakula!

 

“Kinachotushangaza ni kwamba, tumesafiri na wahudumu wa ndege watano  ambao pia wamepimwa na walipaswa kuwa huku lakini wao wamewaruhusu wamekwenda kupumzika hotelini kwamba hawana shida yoyote. Shida ipo kwetu haturuhusiwi kwenda popote wala kufanya chochote,” amesema Zidadu.

 

Wanaodaiwa kukutwa na Corona ni wachezaji watatu (Lucas Kikoti, Fred Tangalu, Hamisi Mgunya) na CEO wa Namungo, Omary Kaya. Mwenyekiti anasema wamejaribu kuongea nao ili wawaruhusu kurudi Tanzania lakini wamekataa na watu wote wamenyang’anywa hati zao za kusafiria (passport).

 

Taarifa zaidi zitafuata.

 

Leave A Reply