The House of Favourite Newspapers

Nandy, Zuchu Ilikuwa Patashika 2021

0

WAKATI zikiwa zimebaki saa kadhaa kuingia mwaka 2022, inasemekana kwamba, mwaka 2021 ulikuwa ni mwaka wa patashika nguo kuchanika kati ya wanadada wawili wanaokiamsha kunako Bongo Fleva, Faustina Charles almaarufu Nandy na Zuhura Othman au Zuchu.

 

Nandy na Zuchu walifanya kufanya makubwa; kila mmoja kupitia mlango wake.

Mwaka 2021 unatajwa kuchagisha ushindani wa mstaa hao kiasi cha mashabiki wao kuwapima katika ngazi ya kimataifa kufuatia wote kutajwa kuwania tuzo mbili kubwa na kuwekwa katika vipengele viwili tofauti na kingine cha pamoja.

 

Wawili hao walipambanishwa kwenye Tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA) 2021 ambazo zilitolewa Novemba 19 na 21, 2021 huko jijini Lagos, Nigeria.

Nandy na Zuchu walishindanishwa katika kipengele kimoja cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.

 

Nandy alishawahi kushinda tuzo hiyo katika kipengele hicho mwaka 2017 hivyo ilitarajiwa kwamba Zuchu angeshinda au kupindua meza au Nandy akaendeleza ubabe, lakini wote walishindwa.

 

Wawili wao walitajwa tena kuwania Tuzo za African Music Magazine Awards (AFRIMMA) 2021 ambazo hutolewa nchini Marekani, huko nako waliwekwa tena pamoja kwenye Kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki japokuwa walishindwa.

 

Wasanii hao wawili mwaka 2020 walishinda tuzo hiyo, Nandy akishinda katika Kipengele cha Msanii Bora Afrika Mashariki huku Zuchu akishinda Kipengele cha Msanii Bora Anayechipukia.

 

Zuchu amekuwa akifanya vizuri kwenye muziki tangu Aprili, 2020 alipotangazwa kuwa chini ya Wasafi huku Nandy aking’aa tangu mwaka 2016 baada kufanya vizuri Shindano la Tecno Own The Stage nchini Nigeria.

 

Maeneo ambayo yameshuhudiwa ushindani wa Nandy na Zuchu ni kama ifuatavyo;

Zuchu ndiye msanii wa kike wa kwanza kufikisha watazamaji milioni 100 kwenye Mtandao wa YouTube Tanzania na Afrika Mashariki ambapo sasa wamefikia zaidi ua milioni 240.3 huku Nandy naye akafanya hivyo na sasa amefikisha zaidi ya milioni 130.2.

 

Nandy alifanya vizuri katika shindano la kwanza la Karaoke barani Afrika, Tecno Own The Stage nchini Nigeria, aliposhika nafasi ya pili na kuondoka na shilingi milioni 36 huku Zuchu akishindwa kufua dafu kwenye shindano hilo.

 

Zuchu ndiye msanii wa kike anayeongoza kwa wafuatiliaji kwenye YouTube Tanzania akiwanao zaidi ya milioni 1.5 huku Nandy akishika nafasi ya pili akiwa nao zaidi ya 914,000.

Hadi sasa Nandy tayari ana albam moja ya The African Princess iliyotoka Novemba 2018 na ana Extended Playlist (EP) mbili za Wanibariki (2020) na Taste (2021) ilihali Zuchu hana albam ila ana EP moja ya I Am Zuchu iliyotoka Aprili, 2020.

 

Mama mzazi wa Zuchu ni Khadija Kopa ambaye ni Malkia wa Taarab huku baba mzazi wa Nandy, Charles Mfinanga amewahi kuwa DJ maarufu.

Zuchu ni shabiki wa Simba na mwaka juzi alitumbuiza kwenye Tamasha Simba Day huku Nandy akiwa ni shabiki wa Yanga na mwaka 2021 alitumbuiza kwenye Tamasha la Siku ya Mwananchi.

Nandy anajisimamia mwenyewe kimuziki chini ya lebo yake ya The African Princess huku Zuchu akisimamiwa na Wasafi chini ya Diamond Platnumz.

 

Mwaka 2021, Nandy alifanya tamasha lake la Nandy Festival katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Dodoma, Arusha, Dar na visiwani Zanzibar huku Zuchu akifanya tamasha kubwa la Home Coming nyumbani kwao, Zanzibar.

Nandy amefanya kolabo na wasanii wa kimataifa na nchi zao kwenye mabano kama Willy Paul (Kenya,) Joeboy (Nigeria) na Koffi Olomide (DR Congo) huku Zuchu akifanya na Joeboy (Nigeria), Olakira (Nigeria) na Spice Diana (Uganda).

 

Hadi sasa, Nandy na Zuchu ndiyo wasanii waliobahatika kupigiwa simu na Rais Samia Suluhu Hassan wakiwa katika shoo zao. Nandy aliipokea simu ya Rais akiwa Dodoma katika tamasha lake la Nandy Festival huku Zuchu akiipokea akiwa Zanzibar katika tamasha lake la Home Coming.

 

Baada ya Zuchu kumzidi namba upande wa YouTube, Nandy naye alikuja kupindua meza upande wa Instagram na Facebook ambako huko ana wafuasi zaidi ya milioni 5.6 (Instagram), na Facebook ana zaidi ya milioni 2.1 huku Zuchu akiwa na zaidi ya milioni 3.5 kwenye Instagram na Facebook zaidi ya milioni 1.2.

 

Nandy ana tuzo nne kubwa; mbili kutoka AFRIMMA (2017 na 2020) -Nigeria, nyingine kutoka AFRIMMA (2020) -Marekani na Maranatha Awards (2018) -Kenya huku Zuchu akiwa na moja tu; Afrimma 2020 kutoka Marekani.

STORI; ELVAN STAMBULI, DAR

Leave A Reply