The House of Favourite Newspapers

Nay wa Mitego: Nyumba Yangu Ikiwaka Moto Nakimbia na Sanamu tu

0
Mkali wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego akiwa mbele ya Sanamu analolipenda zaidi nyumbani kwake, mwenyewe anasema ukitokea moto ataondoka na sanamu hilo.

Na Boniphace Ngumije | Risasi Jumamosi | Mpaka Home

MAMBO vipi mpenzi msomaji wa Mpaka Home? Kama kawaida ya kolamu hii kukutembeza kila Siku za Jumamosi katika nyumba za mastaa, leo inakupeleka moja kwa moja Kimara- Resorts nyumbani kwa mkali wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego.’ Katika safu hii staa huyo wa Wimbo wa Wapo amefunguka mambo mengi anayofanya akiwa nyumbani kwake hapo, msikie anavyotiririka mwenyewe;

MPAKA HOME: Nyumbani kwako pametulia sana, unapenda kufanya
nini hasa ukiwa nyumbani?

Nay wa Mitego akipanga vitu vyake vizuri.

NAY: Inategemea na siku zenyewe. Sifanyi vitu kwa utaratibu kwamba kila siku nitakuwa nafanya jambo moja. Unajua muda mwingi nakuwa kwenye shoo usiku kwa hiyo nikirudi asubuhi nakuwa nimechoka nalala tu.

Lakini ninapopata nafasi, huwa nafanya usafi wa mazingira na mambo mengine.

Nay wa Mitego akiweka sawa mkate wake.

MPAKA HOME: Mambo mengine ukimaanisha nini?

NAY: Nikimaanisha kutunza mifugo yangu. Napenda kufuga kuku, kwa hiyo kila ninapokuwa na nafasi nawahudumia chakula na kusafisha maeneo wanapolala.

…Akiwa jikoni.

MPAKA HOME: Je, unaishi na mwanamke hapa?

NAY: Hapana. Hapo nyuma kidogo nilikuwa naishi na mama yangu, lakini kama unavyojua baada ya sekeseke la Wimbo wa Wapo kuwa kubwa kwa usalama zaidi niliamua kuihamisha familia yangu.

MPAKA HOME: Kwa sasa unaishi na nani?

NAY: Naishi na kijana wangu mmoja anaitwa Atlanta. Huyu ni miongoni mwa vijana wanaonisaidia kuweka kazi zangu kwenye mitandao ya kijamii.

MPAKA HOME: Mai sha umeyapatia yako vizuri, kwa nini mpaka sasa hujaoa?

NAY: Maisha si kwamba nimeyapatia, bado natafuta. Kwa hiyo kuoa ni suala la kutulia na mimi ninafikiri wakati wangu bado. Nahitaji kufanya mambo yangu zaidi na kutunza watoto wangu.

MPAKA HOME: Una watoto wangapi?

NAY: Watatu.

MPAKA HOME: Huwa wanakuja hapa nyumbani?

NAY: Ndiyo tena mara kwa mara. Kama mtoto wa kiume ambaye ndiye mdogo wa wote aitwaye Cultis nimeishi naye sana, tangu akiwa na miezi mitatu, mpaka juzijuzi alipochukuliwa na mama yangu.

MPAKA HOME: Katika nyumba yako unapenda zaidi kitu gani?

NAY: Mazingira ya nyumba tu yalivyo. Lakini pia sanamu langu hilo unaloliona hapo sebuleni nalipenda sana. Yaani nipo radhi nyumba ikiwaka moto niache kila kitu lakini nikimbie nalo.

MPAKA HOME: Aisee, inaonekana lina siri nzito?

NAY: Hapana, ninalipenda tu.

MPAKA HOME: Vipi kuhusu chakula, anakuandalia nani?

NAY: Atlanta au wakati mwingine mimi mwenyewe.

Leave A Reply