The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani 21

0

ILIPOISHIA:

“Yaani mimi, kumbe alijua analala na mimi lakini bosi wao katumia madaraka kunimiliki mimi.”
“Na kweli jana ilikuwa ajabu, yule bosi wao huwa hashughuliki na sisi zaidi ya vijana wake au wageni wake lakini jana tumeshangaa kukuchukua wewe.”
SAA ENDELEA…
“Kaona mzigo unalipa,” nilijishebedua mtoto wa kike kwa kujigeuza kuonesha umbile langu.
“Kweli kabisa upo kimauzo,” Bahati alisema.
“Basi wakati tunakwenda si ndiyo akataka leo iwe zamu yake.”
“Duh! Shoga unatisha umeshapata booking kabisa leo mbu hawakujui.”
“Dada wee, basi si akaniuliza kama nina simu nikamjibu sina, mwanaume kaingiza mkono mfukoni na kutoa kitita eti nikitoka pale ninunue simu kisha nimjulishe kwa kumpigia baada ya kuniandikia namba kwenye karatasi ili jioni ya leo abebe mzigo.”
“Sasa Konso kwa nini umenunua simu ya gharama hivyo, kwani ungekuja kutuuliza panapouzwa simu tungekuelekeza ungepata simu nzuri kwa bei nafuu na pesa kibao ingebakia,” Doi alinilaumu.
“Jamani simu hii sijanunua ametumwa mtu aniletee.”
“Duh! Kweli kapagawa kabla hajapewa mchezo katoa pesa, bado kakuletea simu ya gharama, akipewa si atakununulia gari?”
“Jamani simu hajaninunulia yeye.”
“Sasa kakununulia nani?”
“Papaa.”
“He! Makubwa, ili iweje?”
“Akiwa na shida na mimi ananipigia,” sikutaka kuweka kila kitu wazi.
“Kwa hiyo pesa ya simu unayo?”
“Ninayo.”
“Sasa Jose utampigia?” Sipe aliniuliza.
“Nitampigia, lakini lazima niwasiliane kwanza na Papaa kama hana shida na mimi basi nitampa nafasi hiyo Jose.”
“Sasa itakuwaje si lazima mwende pale?”
“Alisema hanipeleki tena pale baada ya kufanya kosa lile bila kujua.”
“Hapo sawa.”
Sikutaka kuyasema yote niliyozungumza na Papaa kwa vile sikuwajua vizuri mashoga zetu zaidi ya Doi ambaye ndiye aliyekuwa ndugu yangu. Kwa vile nilirudi nimechoka na kifungua kinywa nilikuwa nimepata, nilioga na kupanda kitandani ambako usingizi mzito ulinichukua.
Niliamshwa saa kumi na mbili jioni kwa ajili ya chakula na kujiandaa na kazi ya usiku. Kwa vile nilikuwa na donge moyoni la kutaka kujua kule tulipokwenda ni wapi na wale watu ni kina nani na wanajishughulisha na kitu gani.

Japokuwa nilipata pesa nyingi bila kutegemea lakini nilitakiwa kuijua historia yao kabla

ya kuingia kichwakichwa siku zote tamaa mbele mauti nyuma. Nilipanga kuzungumza na Doi ambaye niliamini anajua kila kitu juu ya wale watu.
Sikutaka kutoka siku ile pia nilipanga kumuomba Doi naye asiende ili tuweze kuzungumza kwa kituo kabla sijapokea simu ya Papaa.
Baada ya kuamka ili tujiandae kuingia kazini kwa kuoga na kupata chakula. Mimi nilikuwa wa mwisho kuoga kutokana na uchovu wa kazi ya usiku.
Wakati natoka kuoga nilimuona Doi akielekea msalani na kopo mkononi, niliitumia nafasi ile kumjulisha, nilimsimamisha:
“Shoga nina mazungumzo muhimu sana na wewe.”
“Mazungumzo! Ya nini tena mbona unanitisha?” Doi alishtuka.
“Wala usishtuke ni ya kawaida ila ni muhimu sana kwetu.”
“Mmh! Sawa.”
“Lakini naomba kitu kimoja.”
“He! Mbona leo unanishangaza.”
“Walaa, ni jambo kuhusu kazi yetu hasa safari yangu ya kwanza jana usiku imeniacha na maswali mengi kuliko majibu.”
“Sawa, lakini si unajua muda si rafiki kwetu?”

“Ni kweli, nataka mi na wewe tuchelewe kidogo ili tuweze kuzungumza.”
“Konso, wenzetu watajisikia vibaya na kuonesha kuja kwako nimeanza kuwatenga, nami sitaki kuonesha tofauti yoyote kitu hicho kinaweza kufanya wakuchukie nami sitaki kuona kinatokea zaidi ya kutengeneza umoja hata kama nitakuwa sipo pengo langu kati yako na rafiki zetu lisionekane.”
“Ni kweli kuna kitu muhimu sana nataka tuzungumze wawili tu.”
“Mmh!” Doi aliguna.
“Kuna kitu nataka unisaidie kabla sijafanya kitu chochote, kumbuka wewe ndiye mwenyeji wangu, kila kitu cha hapa unakijua hivyo basi nahitaji muongozo wako kuna kitu kinataka ufafanuzi wa kina.”
“Nimekuelewa basi fanya hivi singizia ugonjwa wa tumbo ili nibaki na wewe tuzungumze vizuri.”
“Sawa, hapo umenena kitu.”
Tulikubaliana kitu cha kufanya ili tusiwashtue shoga zetu wasifikirie vibaya. Nilimwacha Doi aende msalani na mimi kuingia ndani, nilikuta chakula kimeshaandaliwa.
Itaendelea jumamosi

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply