The House of Favourite Newspapers

Ndugai Apongezwa, Wasema Ilitarajiwa

0

WATU wa kada mbalimbali wamesema hatua ya Spika Job Ndugai (pichani) kujiuzulu ni jambo lililotarajiwa huku wengine wakisema amechukua uamuzi wa busara kwa maslahi ya taifa na chama chake, CCM.

 

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Goodluck Ng’ingo alisema kitendo cha spika huyo kujiuzulu kilitegemewa kwa sababu endapo asingejiuzulu, kulikuwa na uwezekano wa wabunge kupiga kura ya kumng’oa.

 

Alisema zipo sababu kubwa za kiongozi huyo kuchukua hatua hiyo kutokana na kauli yake kuhusu mikopo na kudai nchi itapigwa mnada, ambazo zimeonesha kuwa hata Bunge alilokuwa analiongoza limeshindwa kufanya kazi yake.

 

“Masuala yote kukopa na hata kama kweli nchi ingekuwa iko hatarini kama spika alikuwa na nafasi kama mhimili wa Bunge kuishauri serikali ndani ya Bunge,” alisema Ng’ingo.

 

Aidha, alisema kwa nafasi yake ya uspika pia alikuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambayo ndio inasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na serikali, hivyo pia tamko lake limeonesha kuwa kama hiyo nayo imeshindwa kusimamia serikali.

 

Alisema kanuni za uongozi za CCM zinabainisha wazi kuwa mwanachama yeyote anayepinga maamuzi yanayotokana na kikao halali, ni sawa na usaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.

“Kwa hiyo amefanya maamuzi ya busara kwa sababu asingejiuzulu angeweza kufukuzwa uanachama na kupoteza nafasi ya uspika na ubunge pia,” alisisitiza.

 

Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya CCM na pia Mjumbe wa Kamati Kuu, Abdallah Bulembo alisema Ndugai anastahili pongezi kwa uamuzi aliouchukua.

Alisema ametumia busara kujiuzulu kwa sababu katika nchi kuna mihimili mitatu na ikitokea mhimili mmoja unasigana na mwingine, mambo hayaendi.

 

“Nampongeza Ndugai kwa ujasiri wake wa mara mbili. Mara ya kwanza ni kujitokeza hadharani na kuomba samahani, hili si jambo rahisi kama watu wengi wanavyolichukulia. Pili, ni uamuzi wake wa kutangaza kujiuzulu kwa sababu ameona kutatokea msigano kati ya mhimili mmoja na mwingine na hii itazuia wananchi kupata maendeleo,” alisema Bulembo.

 

Aliongeza kuwa Ndugai amefanya uamuzi wa busara kwa maslahi ya nchi yake, CCM na kumpongeza kwa hilo, akisema “anaipenda nchi yake.”

Naye Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (CCM) alipongeza hatua ya Ndugai kujiuzulu, akisema itamfanya kuwa huru na kuondoa mgongano kati ya mihimili hiyo miwili.

 

“Nampongeza sana kwa uamuzi wake huo hasa ukizingatia kuwa amefikia maamuzi hayo kwa hiari yake mwenyewe na ndio kitu tulichokuwa tunamshauri,” alisema Lusinde maarufu Kibajaji.

Aliongeza: “Uamuzi wake ni mzuri, kwanza utamweka kuwa huru (Ndugai), lakini pia itaondoa mgongano wa mihimili hii miwili.”

 

Awali, Lusinde alisema endapo Ndugai asingechukua hatua ya kujiuzulu mpaka leo, basi angewakusanya wazee maarufu wa Mkoa wa Dodoma kwenda nyumbani kwa spika kumuomba ajiuzulu.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema kwa sasa nchi inapita katika kukua mokrasia.

 

Alisema kujiuzulu kwa Ndugai ni utashi na maamuzi yake kikatiba na hata katika barua yake imejionesha kuwa hajashurutishwa na mtu.

“Ametekeleza haki zake katika suala zima katika suala zima la kutekeleza demokrasia,” alisema Padri Kitima.

 

Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu wa ACT-Wazalendo, Mbarara Maharagande alisema ni hatua sahihi kiuongozi kwani mwenendo wake kwa siku za hivi karibuni haukuwa sahihi.

“Alikuwa na mambo ya kidikteta, lugha alizokuwa akitumia hazikuwa sahihi kama kiongozi, lakini fedha zilizokopwa katika awamu hii ya uongozi shilingi trilioni 1.3 ni fedha kidogo sana ukilinganisha na mikopo ya wakati uliopita. Mbona hakuwahi kuisema hiyo?” alihoji Maharagande.

 

Alisema pamoja na Spika Ndugai kuchukua hatua hiyo, CCM inahitaji utulivu kwa sasa kwa sababu malumbano ndani ya chama kwa sasa yanaweza kuleta athari kwa wananchi.

 

MWANZO MWISHO

“CCM inahitaji utulivu, malumbano ya sasa yanaweza kuwa na athari kwa wananchi, lakini pia malumbano hayo yanaweza kuwa faida kwa vyama vya upinzani katika medali za siasa,” alisema.

Leave A Reply