The House of Favourite Newspapers

NDUGAI: “Huyu Kijana Hajitambui, HAJIELEWI, Anamdanganya RAIS Hadharani” – Video

Spika wa Bunge, Job Ndugai, amemjibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufuatia kauli aliyoitoa leo mbele ya Rais Dkt. John Magufuli, akiwalalamikia Wabunge kuwa wameidhihaki timu ya Taifa ya Tanzania (TAIFA STARS) baada ya kupigwa bao 2-0 na Senegal juzi kwnye michuano ya AFCON.

 

Spika amesema kauli ile ni sawa na kumdanganya Rais hadharani kwani wabunge wanaiunga mkono Taifa Stars kwa asilimia mia moja na kauli aliyoitoa ya kusema Taifa Stars wanahitaji lishe hakuwa na maana ya kuwatusi ama kuwabeza.

 

Awali, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliomba mwongozo wa spika kuhusu suala hilo; “Mmoja ya viongozi amewabagaza wabunge tena mbele ya Mkuu wa nchi, tunapaswa tupate mwongozo wako Spika, kwa sababu anaweza kutokea mwingine akalisema bunge na asifanywe chochote, tunakufahamu hupendi bunge hili kuchezewa, kutomaswatomaswa wala kudharauliwa, nini kimekupata leo unajitetea? Tunaomba usimame utoe kauli kama spika wa bunge na mkuu wa mhimili huu.”

 

Akizungumzia suala hilo, Spika Ndugai amesema; “Tusilikuze sana jambo hili, kama wabunge wangekuwa na mawazo ya kuidhihaki timu yetu je, kungekuwa na wabunge wengine 30, wanaondoka kesho kwenda kwenye mchezo mwingine wa Taifa Stars?

 

“Haya ni mawazo ya mtu mmoja ambaye bahati mbaya ndo hivyo, kuna viongozi wa Serikali ambao wana diriki kumdanganya Rais hadharani, kiongozi wa Serikali unapoongea mbele ya Rais jipangee, sio unawasingizia wabunge wamekukosea nini?

 

“Natamani ningefunguka kidogo kuhusu…. lakini inatosha. Nasema wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, bahati mbaya  kijana wetu huyu hajitambui, hajielewi, na kwa sababu ana nguvu aliyo nayo na makundi kwenye mitandao ya kijamii, anaweza kumtukana Spika, si vizuri kufanya hivyo. Kama kuna mtu ana deni la kufanya kwa Taifa Stars ni yeye, akitaka niseme nitasema, kwa leo imetosha,” amesema Spika Ndugai.

 

“Leo mchana, RC Paul Makonda wakati akizungumza mbele ya Rais Magufuli wakati akizindua Ghala na Mitambo ya Kuchakata Gesi ya LPG ya Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited katika eneo la Vijibweni Kigamboni jijini Dar es Salaam alisema;

 

“Mimi ni mpenzi mkubwa wa Taifa Stars na nimeumizwa sana na matokeo ya Senegal, lakini kilichoniuma kikubwa zaidi ni watu kuwabeza wachezaji wa Taifa Stars ambao wameipa heshima nchi hii kwa miaka 39 kuingia AFCON 2019, leo wameonekana hawana afya njema, hawana chochote, hawana uongozi mzuri, hatuwezi kuwa na taifa la namna hii.

 

“Mheshimiwa Rais, kama itakupendeza ninaomba unipe ruhusa niende Misri kuwapa hamasa vijana wetu, nina uhakika watashinda mechi ijayo dhidi ya ndugu zetu Kenya. Vijana wetu wana ari kubwa ya ushindi, hata leo asubuhi nimeongea na nahodha Mbwana Samatta, amenihakikishia wapo vizuri na watashinda mechi ijayo,” alisema Makonda.

 

MSIKIE NDUGAI HAPA AKIFUNGUKA

Comments are closed.