The House of Favourite Newspapers

Ndugu Watano wa Hamza Waendelea Kushikiliwa

0

WATU watano wanaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi nchini kufuatia shambulio lililofanywa na Hamza Mohamed na kusababisha mauaji ya askari polisi watatu na askari mmoja wa kampuni binafsi.

 

Msemaji wa familia ya marehemu Hamza, Abdulrahman Hassan amesema kuwa ni siku ya pili sasa (jana) watu watano wa familia yao kushikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya taratibu za kiuchunguzi na kwamba amekuwa akifuatilia taratibu ili waweze kuachiwa.

 

Hata hivyo Hassan ambaye ni mume wa dada yake Hamza amesema kuwa kama familia nao walishtushwa na kitendo cha mauaji kilichofanywa na Hamza na kwamba walijua kuwa anamiliki silaha lakini wahawakuwahi kuona kasoro yoyote kwake iliyopelekea kufanya alichokifanya.

 

Amesema, “Tulikuwa hatujui kama angeweza kutumia silaha kwa kile alichokifanya, Hamza alikuwa akiishi muda mwingi mkoani Mbeya na kazi zake ni migodini hivyo tulijua kutokana na kazi zake alikuwa anamiliki silaha na anajua jinsi ya kuitumia.”

 

Mama na dada wa marehemu Hamza Mohammed wameachiliwa baada ya mahojiano, ambapo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.

 

Hamza aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, jirani na ulipo Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

 

Mwishoni mwa juma lililopita Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

Leave A Reply