The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukuwa Msukule

0

MSIMULIAJI: Obedi Masanja

MWANDISHI: Shani Ramadhani

NAITWA Obedi Masanja, ni mkazi wa Gongo la Mboto hapa Dar. Nimekuwa nikisoma na kufuatilia mikasa mingi ya watu kupitia magazeti ya Global Publishers na kutokana na kusoma mikasa hiyo na mimi nimeona si vibaya nikatoa mkasa wangu ili watu wajue na wajifunze kupitia kwangu.

Huu mkasa ulinitokea nikiwa nyumbani kwetu Mara katika Kijiji cha Kigada ambapo ndipo nilipozaliwa na kukulia hapo miaka 37 iliyopita.

AMALIZA MSINGI, AFELI

Baada kumaliza elimu yangu ya msingi mwaka 1991 katika Shule ya Msingi Kigada na matokeo yalitoka mabaya sikufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na wakati huo hali ya maisha ilikuwa ngumu mtu kupata bahati ya kusomeshwa na wazazi hasa kwa familia kama ya kwetu kwani tulikuwa na maisha duni.

AINGIA KWENYE UVUVI

Kwa kuwa mimi binafsi nilitamani nisome sana ili baadaye nije kuiinua familia kwa sababu wakati huo pale nyumbani walikuwa wanategemea kilimo cha mkono ambacho kilikuwa hakina mafanikio yoyote hivyo nikajikita katika uvuvi kwa lengo la kutafuta pesa itakayoniwezesha kurudi tena shuleni kurudia darasa la saba.

Nilianza kujishughulisha na uvuvi nyakati za usiku kwa kutumia taa aina ya chemli. Nikiwa huko nilishanusurika kuzama mara kadhaa lakini kwa kuwa Mungu alikuwa bado anataka niendelee kuishi sikufa, niliendelea kutafuta riziki na pesa niliyokuwa naipata kupitia kazi ile nilikuwa nikiihifadhi nyumbani japo kuna wakati hali ilizidi kuwa mbaya nyumbani nikawa nalazimika kuchukua kiasi na kumpa mama kwa ajili ya chakula.

Nilifanya kazi ya uvuvi kwa miaka mitatu na pesa niliyokuwa naipata ilikuwa imetosha kuniwezesha kurudi tena shuleni na angalau kuiinua familia yangu kiuchumi kwa kupitia kilimo cha zao la chai na kuajiri vibarua (vijana ambao walikuwa wanalima na tunawalipa pesa) huku mimi nikiwa msimamizi.

BABA ATAKA KUMPA SAPOTI, AKATAA

Baba yangu alikuwa na eneo kubwa la mashamba aliponiona nina kiu ya kusoma akataka auze baadhi ya mashamba lakini ikabidi nimweleweshe sana ndipo akakubaliana na ushauri wangu wa kujikita katika kilimo.

Mwaka 1995, mwezi wa kwanza ndiyo nilikwenda kuanza darasa la saba katika Shule ya Msingi Mgata ambayo ilikuwa palepale kijijini kwa kusoma elimu ile ya watu wazima ambapo nilikuwa nikienda jioni na tayari nilikuwa nimeshanunua vitabu vya masomo yote ili nisiwe napata shida kujisomea hata nikiwa nyumbani.

AANZA MASOMO KWA TABU

Asubuhi nikawa nakwenda shambani, mchana narudi nyumbani kujiandaa kiwenda shule japo kuna wakati mwingine nilikuwa nashindwa kwenda kutokana na uchovu na kuishia kujisomea nyumbani kwa kutumia mbalamwezi au kama mbalamwezi hakuna siku hiyo nilikuwa nikijisomea kwa kutumia moto wa kuni.

Nilikuwa nakoka moto jikoni na kisha najisomea nikiona sehemu siielewi nilikuwa nikiweka kiporo lakini ajabu ya Mungu, kwenye mitihani nilikuwa nikishika nafasi ya kwanza.

Nilisoma katika mazingira hayo na kuhakikisha nimebadili kwa kiasi fulani pale nyumbani palikuwa pameimarika kiasi kwamba kwa wakati ule kijiji kizima ni kwetu tu ndiyo kulikuwa na maendeleo kwa kujenga nyumba ya matofali na kuweka bati.

AFANYA MTIHANI WA TAIFA

Mwaka 1995 nilifanya mtihani wa taifa na baadaye majibu yalitoka nikachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 1996 katika Shule ya Sekondari Ivungo ambayo ni ya bweni. Iko Bukoba, Kagera. Nakumbuka Januari Mosi ndiyo nilitakiwa kuripoti shuleni hapo. Wakati huo nilikuwa nina umri wa miaka 20.

AENDA SHULE, AKUTANA NA MAUZAUZA NJIANI

Nilijiandaa kwenda shule kwa vitu mbalimbli vilivyokuwa vinatakiwa lakini siku niliyokuwa nakwenda kuripoti ndipo nikaanza kukutana na mauzauza njiani naelekea kituoni kupanda basi lililokuwa linakwenda Bukoba.

Itaendelea wiki ijayo

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Ndugu Zangu Walinichukuwa Msukule.

Leave A Reply