The House of Favourite Newspapers

Nelly Muosha Magari wa Posta-23

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Nelly aliyekuwa chumbani kwa Doreen wakipiga stori baada ya kugarazana na kukabidhiwa simu, alipoanza kuitwa tena na fundi Yassin. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na utamu huu…

Sharobaro Nelly alipomsikia fundi Yassin akimwita alipaniki na kutaka kuitika lakini Doreen akamkataza kwa ishara na kumwambia atulie pale kitandani.

Kama alivyoshauriwa, alitulia ndipo Doreen akaangua kicheko cha chini na kumwambia Nelly kumbe alikuwa muoga namna ile, Nelly akaachia tabasamu.
“Ndiyo maana yake, wewe hujui kama kunguru muoga huishi miaka mingi?” Nelly alimwambia Doreen kwa sauti ya chini.

Doreen alipoambiwa hivyo, alicheka na kumweleza Nelly kwamba kumbe alikuwa mtaalam wa methali, Nelly akamwambia alikuwa zaidi ya mtaalam, mtoto wa kike akacheka.

Wakati wakiendelea kuzungumza, fundi Yassin aliendelea kumwita na alipobaini Nelly hakuwemo ndani akarudi ndani huku akicheka maana mambo ya kijana wake huyo licha ya kumsikitisha yalimchekesha pia.

“Sasa si unaona, kakuita mpaka kachoka kaamua kwenda kuendelea na kazi, ungeitika ungeharibu kila kitu,” Doreen alimwambia.

“Da! Wewe ni zaidi ya wajanja, nashukuru kwa kunizuia kuitika maana tungefanya bonge la misteki mpenzi wangu,” Nelly alimwambia Doreen.
Doreen alimwambia asijali na kumweleza kuwa muda ule ulikuwa mwafaka kumtoa mle chumbani, kauli ambayo iliungwa mkono na Nelly ambaye moyoni alisema hata kama fundi Yassin atammaindi ilikuwa poa tu!

Msichana huyo wa kishua ambaye moyo wake ulikuwa kwatu kwa kupewa raha na Nelly, alifungua mlango wa uani ambao ulikuwa haufunguliwi mara kwa mara, Nelly akatoka.
Kama alivyopewa ujanja, alipotoka alikwenda kwenye duka moja la jirani akanunua soda tatu na maji chupa moja na kurejea getini, akaanza kugonga huku akimwita Zakayo amfungulie.

Kufuatia geti kugongwa na kuitwa jina lake, Zakayo aligundua aliyekuwa akimuita alikuwa Nelly, akamwambia fundi Yassin kwamba mtu aliyewapelekea ndiye aliyekuwa akigonga geti.

“Unasema kweli?” fundi Yassin alimwuliza.
“Kaka mkubwa bwana na huyo dogo wako unachekesha, ila ni kama nilivyokwambia bila ya kumuondoa mimi naacha kazi tusije wote tukaonekana tunashabikia vitendo vyake maana kwa ninavyomfahamu bosi akibaini ujinga wake atatutimua,” Zakayo alimwambia.

Fundi Yassin alipoelezwa hivyo, alipata hasira akaamua kwenda kufungua geti na kweli alipofanya hivyo akamkuta Nelly kasimama huku akitabasamu na mkononi akiwa na mfuko.

“Nelly naona umeshindwa kazi, ingia ndani uchukue vitu vyako urudi nyumbani mambo mengine tutazungumza huko,” fundi Yassin alimwambia kwa hasira.

“Kwani bro nimefanya kosa gani, wakati naendelea na kazi nilibanwa na kiu nikaamua kwenda kununua maji, hata nyinyi nimewaletea soda hizi hapa,” Nelly alimwambia huku akimuonesha zile soda.

Kitendo cha dogo huyo mpenda mademu wazuri kuongea kwa upole na kumuonesha zile soda, fundi Yassin akajikuta akicheka na kumwambia alikuwa na bahati kwani alitaka kumtimua.

“Bro bwana, sasa unitimue kwa kosa gani, kwenda kununua soda?” Nelly alimwambia.
Kabla fundi Yassin hajajibu, Nelly alitoa soda moja ya kopo akampatia kisha alifunga geti na kuongozana kwenda ndani walikokuwa akina Haruni na Zakayo.

Walipofika fundi Yassin aliwafahamisha kwamba Nelly hakutegea kazi ila alikwenda kununua soda, sharobaro huyo akatoa soda zilizobaki akawapatia akina Zakayo.

“Ila wewe dogo una mambo mengi kama unga wa ngano, hii kazi haikufai, wewe ulifaa uwe mwanamuziki wa Bongo Fleva,” Haruni alimwambia Nelly, wote wakacheka.
Wakati wakizungumza, hakuna kati yao aliyejua dogo huyo kwenye mfuko wake wa nyuma kulikuwa na simu ya kisasa aliyopewa na Doreen.

“Ulichokiongea Haruni nakiunga mkono kwa asilimia mia moja, huyu alifaa awe msanii wa Bongo Fleva, huku kaja kwa bahati mbaya,” Zakayo naye alidakia.
Mafundi hao walifanya kazi hadi jioni ambapo hata hivyo Nelly hakuweza kumaliza kuhamisha mchanga, kama ilivyokuwa kawaida ya fundi Yassin kumuona Doreen kwa ajili ya malipo alimwita msichana huyo.

“Vipi fundi mnataka kuondoka?” Doreen alimwuliza fundi Yassin.
“Ndiyo, nafikiri tukija kesho tutamalizia kuweka marumaru kule vyumbani kisha tuhamie subuleni,” fundi Yassin alimwambia.

Alipoambiwa hivyo, Doreen aliyekuwa akimtupia jicho kijanja Nelly aliwapa pole ya kazi kisha alimkabidhi fundi Yassin bahasha ya khaki iliyokuwa imetuna.

Itaendelea wiki ijayo. Maoni tumia namba hiyo juu.

Leave A Reply