The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-37

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Anatujua, sisi ni wenzake. Tulikuwa tukifukua makaburi pamoja. Ana deni letu la mtoto. Alituambia akizaa mtoto wa kwanza atatupa sisi tumle!”
“He! Mume wangu…vipi?”
SASA ENDELEA…

Nikajifanya kama nashangaa.
“Naona hao ni wendawazimu mke wangu, achana nao,” nikamwambia kisha nikainuka na kushuka kitandani. Nilikwenda kwenye dirisha nikafungua pazia na kuchungulia nje.
“Ninyi wendawazimu…mmetokea wapi? Hebu ondokeni hapa! Kwanza mmeingilia kwa wapi?”

“Unajua jinsi tulivyofika hapa kwako, sisi si wendawazimu, tuko timamu kama ulivyo wewe. Shida yetu ni mtoto wetu. Wewe pia umeshakula nyama za watoto wa wenzako. Tulikusaidia ukapata ubunge hadi leo umekuwa waziri. Usijaribu kutugeuka.” Maneno yakawa yanasikika nje ya dirisha.

Nikamtazama mke wangu kuona jinsi alivyoyapokea. Yalikuwa yamemchanganya akili. Nilimuona waziwazi alikuwa amechanganyikiwa.
Maneno yaliendelea kumiminika nje ya dirisha.

“Shida yetu ni huyo mtoto. Huyo mtoto si wako ni wetu. Tutamchukua tu, huna ujanja wa kumzuia.”

“Ninyi ni vichaa kwelikweli. Mimi sielewi mnachoongea na sijui mlifikaje humu ndani. Huyu mlinzi sijui anafanya kazi gani? Anaacha vichaa wanaingia ndani! Pumbavu kabisa!” nikajidai kufoka.

Niliziba pazia nikaenda kuchukua simu yangu harakaharaka. Nikampigia yule mlinzi.
Simu iliita kwa karibu nusu dakika kabla ya kupokelewa.
“Wewe unalala siyo?” nikamuuliza mlinzi alipopokea simu.
“Sijalala mheshimiwa, niko macho.”

“Mbona watu wanaingia humu ndani wanatufanyia fujo, wewe uko wapi?”
Mlinzi akashtuka.
“Watu? Watu gani hao?”
“Unauliza watu gani wakati nyumba imezingirwa kabisa, hebu njoo hapa kwenye dirisha langu uone.”

Mlinzi akakata simu. Bila shaka alikuwa akija upande ule uliokuwa na dirisha.
Nikasogea karibu na dirisha na kupiga kelele za kutishia.
“Piga! Piga risasi watu wote hao!”

Niliyasikia mabuti ya yule mlinzi wakati akiizunguka nyumba. Nikatoka mle chumbani na kufungua mlango wa nje.
Mlinzi alizunguka nyumba nzima na kutokea tena kwenye mlango.
“Mheshimiwa nilikuwa naangazaangaza lakini sijaona mtu yeyote,” akaniambia.
Ikabidi nizunguke naye tena lakini hatukuona mtu yeyote.
“Nilisikia kama kuna watu,” nikamwambia.

“Hapana mheshimiwa. Hao watu wangeingia kwa wapi wakati mimi niko kwenye geti?”
Nilikuwa nimetahayari kidogo lakini nilijikaza.
“Sawa. Basi jaribu kuwa makini. Usilale!” nikajidai kumwambia.
“Sawa mheshimiwa, siwezi kulala.”

Nikarudi ndani. Mke wangu alikuwa akinisubiri chumbani. Alikuwa amemkumbatia mtoto wake kitandani. Yale maneno ya wale wachawi yalikuwa yamemtisha.
Aliponiona naingia mle chumbani alinikazia macho.

“Wamekwenda wapi hao watu?” akaniuliza.
“Tumezunguka nyumba yote hatukuona watu,” nikamjibu.
“Sasa wale walikuwa akina nani?”

“Ndiyo nimeshindwa kuelewa, sijui walikuwa akina nani!”
“Mbona walikuwa wakisema wametoka Nzega na kwamba wewe ni mwenzao mlikubaliana uwape mtoto wako?”

“Walikuwa wakijiropokea tu maneno yasiyoeleweka. Mtoto gani tulikubaliana niwape!”
“Sasa wewe katika akili yako unataka uniambie wale walikuwa akina nani na kwa nini walitoweka ghafla?”

“Mke wangu hata mimi najiuliza kama unavyojiuliza wewe, bado sijawaelewa wale watu.”
“Yatakuwa ni maajabu ya mwaka. Mimi sijawahi kuona hali kama hii maishani mwangu!”

Mke wangu aliposema hivyo hakuzungumza tena. Bila shaka alikuwa akizungumza na moyo wake.
Japokuwa hatukuzungumza tena habari ile hakukuwa na aliyelala tena, si mimi wala yeye.

Asubuhi alinikumbushia tena yaliyotokea usiku uliopita.
Akaniuliza tena wale watu walikuwa akina nani. Majibu yangu yalikuwa yaleyale niliyompa jana usiku.

Muda wetu wa kwenda kazini ulipowadia tukatoka. Niliuona uso wa mke wangu haukuwa wa kawaida. Ulikuwa na kitu kama tuhuma dhidi yangu lakini hakutaka kuniambia yaliyokuwa moyoni mwake.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

Leave A Reply