The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-3

0

Ilipoishia wiki iliyopita

Baada ya kumuachia maelekezo yote muhimu juu ya namna ya kuendesha biashara kipindi nikiwa sipo, nikapanda basi kuelekea Songea, alfajiri ya siku hiyo, miaka mingi iliyopita.

Songa nayo sasa…

Nikiwa ndani ya basi lililoitwa Chesangoma, mawazo yangu yalikuwa ni juu ya simulizi za machimbo, nilitamani sana kufika na kuona jinsi gani vijana wengi wanatoka kutokana na kazi hiyo. Mfukoni mwangu nilikuwa na kiasi cha shilingi milioni moja, niliamini hizo zingetosha kunifanya nielewe mazingira na kujua sehemu ya kuanzia.

Safari ilikuwa ndefu sana, kwani hadi tunafika katika mlima Kitonga, ilikuwa mchana na tukasimama hapo kula katika hoteli iliyokuwa mwanzo tu wa mlima. Baada ya kula safari ikaendelea na nikapitiwa na usingizi hadi wakati flani niliposhtuka baada ya kuona kama ninamwagiwa maji baridi.

Niliposhtuka na kuamka, ilikuwa ni jionijioni. Nikashtuka kuona nimeloa sehemu ya bega niliyoegemea basi, kumbe kulikuwa na umande ndani ya gari, nilipouliza hapo ni wapi, nikaambiwa tupo Njombe, sehemu yenye baridi kali katika ukanda wa Nyanda za juu kusini.

Nikalazimika kulifuata begi langu, nikatoa koti maana tanguo awali nilidokezwa kuwa huko ninakoenda kuna baridi sana. Tulifika Songea mjini majira kama ya saa mbili usiku, nikatafuta sehemu ya kulala, lakini kabla ya kwenda kulala, nikajiunga na wenzangu waliokuwa wakipata moja moto moja baridi, ili angalau kuuandaa mwili kwa baridi kali ya usiku. Majira ya saa tano za usiku ndipo nilipopanda kitandani kulala.

Asubuhi na mapema, nilipanda basi la kuelekea Mbinga, ambako baada ya saa tatu, nikafika eneo hilo la Kitai, nikateremka kwa mujibu wa maelekezo, nikaulizia magari ya kuelekea Masuguru, nikaonyeshwa Land Rover 109 zilizokuwa zimejipanga foleni, nikasogea na kuingia katika lile lililokuwa mbele zaidi. Nilipoulizia kuhusu nauli, nikaambiwa ni shilingi elfu 30, mara mbili ya ile ya kutoka Dar es Salaam hadi Songea!

Saa moja baadaye tukaanza safari ya kuelekea machimbo, njia ilikuwa ni mbovu sana, ingawa kwa wakati ule wa kiangazi, kidogo ilikuwa nafuu, kwani kama ingekuwa wakati wa masika, nadhani tungepata taabu sana kufika tulikokuwa tunataka kwenda. Ingawa wenyeji walisema ni umbali mfupi tu, lakini hadi jua linazama, ndipo tuliingia katika ‘mji’ wa machimbo.

Pilikapilika zilikuwa ni nyingi katika kamji hako, watu wakiingia huku na kutokea kule, baa karibu kila banda na maduka. Watu wengi wanaume, wanawake na vijana ndiyo usiseme. Nikiwa bado mgeni, nikaenda kwenye baa moja iliyoonekana imetulia kidogo, nikajisogeza na kuagiza kinywaji huku nikiusoma mji huo.

Baada ya kunywa bia kama tatu hivi, nikagundua hata wale niliokuwa nimekaa nao, walikuwa wageni. Muuzaji aliniambia kuwa katika mji huo, kila siku wanakuja watu wapya na kwamba hakuna mwenyeji wa eneo hilo. Ingawa lipo mkoani Ruvuma, lakini vijana wengi wametoka mikoa ya mbali kama Arusha, Mtwara, Mbeya na Dodoma.

Sikutaka kulala, hivyo nilikunywa polepole na baadaye kula vizuri ili nisije kuibiwa fedha nilizokuwa nazo. Niliambiwa eneo la machimbo liko umbali wa kama kilometa mbili kutoka pale na watu huanza kwenda huko kuanzia saa kumi na moja alfajiri.

Asubuhi siku iliyofuata, niliondoka pale kambini kama saa mbili hivi, nikapanda bodaboda hadi eneo la machimbo. Nikaenda kule wanakochimba, nikafika hadi mtoni wanakosafisha madini, nikaambiwa madini yanayopatikana pale ni Ruby, Green Tomaline na mengine yasiyo maarufu, lakini yenye soko sana huko Ulaya.

Nikazunguka pia eneo hilo nikaona watu wakiwa na maeneo ya kuuzia vyakula, pombe, sigara, bangi, nguo na kila aina ya biashara. Baada ya kushuhudia sehemu zote, nikajikuta nikivutiwa na kufanya biashara zaidi kuliko kuchimba madini.

Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.

Leave A Reply