The House of Favourite Newspapers

‘Nisaidieni jamani, mishipa mwilini imepasuka’

0

Na Elvan Stambuli

HATARI! Kelvin Msuya (28), mkazi wa Kijiji cha Kiyungi wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro yupo katika hatari ya kupoteza maisha kufuatia mishipa ya mwilini mwake kupasuka na kuvuja damu kwa ndani.

Akizungumza na Uwazi akiwa Hospitali ya KCMC mjini Moshi, Msuya anasema ana matatizo mazito katika mwili wake kwani baadhi ya mishipa yake ya damu imethibitika kupasuka.

CHANZO CHA UGONJWA
“Mimi nilizaliwa Agosti 29, mwaka 1987. Nilisoma Shule ya Msingi Kiyungi na masomo ya sekondari niliyapata Umburi Vunjo baadaye nikahamia Sekondari ya Shighatini.
“Nikiwa kidato cha tatu, mwaka 2006 nikaanza kuugua ugonjwa usiojulikana lakini unamalizia na upungufu wa damu mwilini.

“Tatizo hilo lilikuwa likinikumba mara kwa mara na nikawa natibiwa kwa kulazwa Hospitali ya KCMC na kuongezewa damu.“Kusema kweli, nilimaliza kidato cha nne kwa shida kutokana na kusoma huku nikiuguaugua.”

KUHAMISHIWA MUHIMBILI
“Baada ya kumaliza masomo ya sekondari, tatizo la kuongezewa damu halikwisha, nikahamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

“Nilifanyiwa vipimo na kugundulika kuwa, mishipa ya njia ya chakula imepasuka na kuvujisha damu, kitaalamu walisema inaitwa esophageal varieces na mishipa iliyokuwa ikipeleka damu kwenye ini nayo ilikuwa imepasuka na kufanya kovu hivyo, ilikuwa haipeleki damu sawasawa.

“Madaktari pia katika kunipima waligundua kuwa, nina vidonda vitatu tumboni.”

TIBA
“Niliambiwa kuwa ni lazima niwe nachomwa sindano na kila sindano moja ni shilingi laki moja na nusu (150,000), fedha ambazo sina kwa hiyo sijawahi kuchomwa.

“Niliambiwa nianze kwanza kuchomwa sindano tatu, hiyo maana yake natakiwa kuwa na shilingi laki nne na nusu (450,000), gharama nyingine za matibabu niliambiwa ni shilingi milioni mbili na laki saba (2,700,000) ambazo sina.

Hapa ninapoongea na wewe, nimetoka chumba cha wagonjwa mahututi Hospitali ya KCMC, Jumatatu Novemba 30, mwaka huu na natakiwa kurudi tena Muhimbili lakini nashindwa kwenda kwa kuwa sina fedha.”

NALELEWA NA MAMA
“Nalelewa na mama tu ambaye hana kipato, baba yangu ambaye haishi na mama ni mgonjwa na sipati msaada wowote kutoka kwake kwa sababu hajiwezi kiuchumi. Kutokana na hali hiyo nawaomba Watanzania wenzangu waokoe maisha yangu kwa kunisaidia kwa hali na mali,” alisema Msuya na kuangua kilio.

Yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kuwasiliana na Kelvin kwa namba 0765 041 166, 0714 343011, 0785 454 854.

Leave A Reply