The House of Favourite Newspapers

Nuh Mziwanda: Sina Mpango wa Kumlipua Shilole

0

Nipeleke kwa muganga na mimi nataka wanga…

Mana mapenzi yamenikoroga kinoma …….

Kanichanja chale mwili mzima…..

Mi simkumbuki hata jina …

Yule gaidi hasidi wa moyo wangu……

Haya mapenzi basi nimeyavulia shati…

Kupendwa ni ajira na mimi sina vyeti…

Ni vipande vya mashairi kwenye bonge moja la ngoma inayokwenda kwa jina la Jike Shupa kutoka kwa kijana machachari kwenye ramani ya muziki wa Bongo Fleva Nuh Mziwanda.

Jike Shupa ni bonge moja la kolabo ambalo alimshirikisha mfalme wa muziki wa Bongo Fleva Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.

Jina halisi ni Naftar Mlawa japo wengi wamezoea kumuita Nuh Mziwanda Baby.

Amefanya poa na ngoma zingine kama Hadithi, Sandakalawe, Anameremeta, Mama Ntilie, Natapatapa na nyingine kibao.

Na kwa sasa ameachia mkwaju mkali unaokwenda kwa jina la Busy Body akiwa na rapa mkali hapa Bongo Ibrahimu Mandingo ‘Country Boy’.

MIKITO limepiga stori konki na Nuh Mziwanda na amefunguka mengi ikiwemo ishu ya kipigo cha aliyekuwa mpenzi wake mwanamuziki na mjasiriamali Zuwena Mohamed ‘Shilole’. Ungana naye hapa chini.

MIKITO: Hongera kwa kazi nzuri unazoendelea kuzifanya kwenye muziki

MZIWANDA: Ahsante sana

MIKITO: Umekuwa na staili ya kuchelewesha kutoa nyimbo labda tatizo liko wapi?

MZIWANDA: Ni kweli, ila kwa sasa sitakuwa nachelewesha kutoa nyimbo kama ilivyokuwa hapo awali, nitawapa mashabiki zangu Back to Back(ngoma kwa ngoma)

MIKITO: Mipango yako iko vipi kwa sasa hasa kuzidi kulikuza jina lako?

MZIWANDA: Kikubwa ni kufanya kazi nzuri ambayo itapendwa na mashabiki zako, kuwa na heshima kwa kile unachokifanya  hilo tu.

MIKITO: Siku chache zilizopita ulionesha kumkingia kifua Shilole baada ya kupositi picha akiwa amepigwa na mumewe, unalizungumziaje hili?

MZIWANDA: Unajua kila mtu ana mawazo yake, mimi ni kioo cha jamii watu wananiangalia. Siwezi kukaa nikateta ujinga, ili kuwafurahisha watu wengine, kile nilichokiandika ndicho nilichokiona, siwezi kukoment vibaya kabisa.

MIKITO: Kwa upande wako unadhani ni sawa kwa kile alichofanyiwa Shilole na mumewe?

MZIWANDA: Unajua mimi ni baba nina mtoto wa kike, nawaza siku mwanangu anafanyiwa vile na mumewe. Si sawa inasikitisha na inauma, maana kile kitendo si kizuri.

MIKITO: Je wewe uliwahi kumpiga Shilole kwa kipindi chote cha uhusiano wenu?

MZIWANDA: Hapana sikuwahi kumpiga hata siku moja. Kwanza si sawa mwanaume kugombana na mtoto wa kike. Tumekuwa kwenye uhusiano takribani miaka minne nilikuwa nalinda heshima yangu kama mwanaume ndani ya nyumba.

MIKITO: Je kwa hilo unamshauri nini Shilole?

MZIWANDA: Kashakuwa mtu mzima aangalie cha kufanya maana kubadili wanaume ni kujitia aibu kila mtu ana mapungufu. Aka echini na mumewe wayaongee yaishe.

MIKITO: Je unazungumziaje kipigo cha Shilole kipindi mko kwenye uhusiano?

MZIWANDA: Hayo mambo yameshapita,  Siwezi kuzungumzia kitu chochote tuongee mambo mengine.

MIKITO: Inasemekana kwamba na wewe unataka kutoa picha ambazo alikuwa akikupiga wakati mpo kwenye uhusiano je ni kweli?

MZIWANDA: Hakuna kitu kama hicho, hayo ni maneno ya watu wameamua kusema. Sina mpango huo kabisa na wala sijawaza kufanya hivyo.

MIKITO: Sasa hivi upo kwenye mahusiano vipi kuhusiana na mipango ya ndoa.

MZIWANDA: Bado sijajipanga kufunga ndoa.

MIKITO: Tukirudi kwenye muziki unaonaje ushindani uliopo sasa?

MZIWANDA: Kwa sasa lazima ushindani uwe mkali kwa sababu kila mtu amekuwa mjanja tofauti na hapo awali, ubunifu umekuwa mwingi sana.

MIKITO: Kwenye gemu hili unajiona na kitu gani cha kitofauti? MZIWANDA: Mimi niko tofauti sana na wengine ndiyo maana nikaitwa Nuh Mziwanda. Si jina tu na kingine huwa sipendi kujichanganya na watu wengine. Napenda kufanya vitu vyangu mimi kama mimi, ili kufika pale ambapo mashabiki zangu wanahitaji nifike

MIKITO: Mipango ya kuachia album imekaa vipi kwa upande wako?

MZIWANDA: Ni kitu kizuri sana msanii kuachia album kwa sababu kinafanya watu waamini kipaji chako. Msanii ukitaka kujua umekamilika kwenye sanaa lazima utoe album.

MIKITO: Wasanii wengi wamekuwa wakilalamika soko la album linasumbua kwa upande wako unaizungumziaje?

MZIWANDA: Kutoa album siyo kitu kidogo, unatakiwa kutoa kitu ambacho watu watakubali na siyo kuvurunda hivyo hata mimi nitakuja kulifanya, ila nisiliweke wazi sana.

MIKITO: Je mipango yako iko vipi kupasua kimataifa zaidi?

MZIWANDA: Ndiyo hivyo tunakomaa, unajua kufikia levo za kimataifa ni jinsi ambavyo wewe unatengeneza muziki wako hadi kufikia levo hizo. Nadhani ni msanii kujiongeza kwa kufanya muziki mzuri, naamini ukifanya hivyo utaona tu mambo yanaenda kiuepesi.

MIKITO: Unadhani ni kitu gani kinachowakwamisha wasanii kufika mbele zaidi?

MZIWANDA: Naweza kusema wasanii hatupendani na ubinafsi umekuwa mwingi. Kitu kingine  hatupeani madili na roho mbaya zimetawala.

MIKITO: Changamoto unazozipitia kwenye kazi yako ya muziki ni zipi?

MZIWANDA: Changamoto ni nyingi, lakini mimi naamini tukiweza kuepukana nazo kila kitu kitakuwa sawa, wasanii tusisaidiane kwa sababu eti tunafahamiana, tusifanyiane kitu kwa kukomoana na hata maprodyuza wanasumbua sana.

MIKITO: Unajivunia nini kwenye muziki wako?

MZIWANDA: Mafanikio ambayo najivunia sasa hivi ni mengi ila ninajisikia furaha sana kujulikana na watu wa aina tofauti tofauti, hili ndilo ninaweza kusema ni moja kati ya mafanikio yangu, mengine ni mambo ya kawaida tu.

Makala: Khadija Bakari

Leave A Reply