The House of Favourite Newspapers

Hospitali Ya Kigamboni Yapatiwa Vifaa Tiba Na Puma Energy Wakiadhimisha Siku Ya Wanawake

0
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Bi Fatma Abdallah (wapili kulia) akimkabidhi sehemu ya vifaa tiba Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Dk. Lucas Ngamtwa anayemfuatia ni Matroni wa hospitali hiyo, Eva Sambai na mwisho ni Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. James Mbapila. Kulia anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Wanawake wa Puma, Dativa Showe.

Dar es Salaam 8 Machi 2024: Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania leo imekabidhi msaada wa vifaa tiba mbalimbali ikiwemo viti mwendo na mashine za kupimia presha vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 6.5 ambavyo vitatumika katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Bi Fatma Abdallah amesema katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kampuni hiyo imeona ina kila sababu ya kuwagusa wanawake kupitia vifaa tiba hivyo ambavyo wamekabidhi.

Picha ya pamoja Wanawake wa Puma na uongozi wa hospitali hiyo baada ya tukio la ugawaji wa msaada huo.

“Kila Machi 8 ya kila mwaka imekuwa ikiadhimishwa Siku ya Wanawake Duniani, hivi nasi mwaka huu tumeona tusikae nyuma na kuamua kujumuika na wenzetu kwa kuadhimisha siku hii kitofauti. Tumeona tuguse jamii na jamii yenyewe yetu inayotuzunguka.

“Puma tumekuja kukabidhi vifaa tiba hivi katika wodi ya wanawake katika Hospitali hii ya Wilaya ya Kigamboni, tumejitahidi kukusanya vifaa tiba kadhaa vyenye thamani ya Sh.milioni 6.5. Tunavyo vifaa tiba vya aina mbalimbali ikiwemo viti mwendo, mashine za kupima presha na vinginevyo, tunaamini vitasaidia wodi ya wanawake. Tunafahamu wodi ya akinamama ni eneo lenye changamoto nyingi na wagonjwa wengi.

“Hivyo inahitaji uangalizi tofauti, sio kwamba tunajipendelea sisi wanawake lakini wodi ya wanawake inahitaji uangalizi wa tofauti kidogo,” amesema Bi. Fatma huku akielezea kuwa katika kampuni yao wameendelea kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake ikiwemo katika ngazi za juu akiwemo yeye mwenyewe.

Amefafanua zaidi kuwa Puma kuna wanawake zaidi ya 48 na hatua kubwa imepigwa kuanzia mwaka 2023 kwani wakati anaingia Puma mwaka jana kulikuwa na wafanyakazi wanawake asilimia 9 lakini sasa hivi imefika asilimia 16 na kuongeza kuwa wanawake wengi wameingizwa kwenye nafasi za juu.

Hata hivyo amesema wanaendelea kutengeneza mazingira kuwawezesha, kuwathaminisha na kuwaleta pamoja wanawake ili waweze kuleta maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

“Puma tutaendelea kusaidia sekta ya afya kama tulivyosema, tunaangalia sekta ya afya na sekta ya elimu,” amesema huku akikumbusha kuhusu Puma ni kwamba ni kampuni kubwa inayojuhusisha na sekta ya mafuta, ni kampuni ambayo inawabia wawili.

“Sisi tunaongoza katika soko la mafuta lakini bado tunaendelea kukua, tunaimani maono yetu ni kuhakikisha tunafikia wananchi wengi ambao hawapati huduma ya mafuta kwa ukaribu.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk. James Mbapila na Matroni Eva Sambai kila mmoja kwa wakati wake wameshukuru kwa msaada huo na kusema Puma imeonesha kuwathamini na kuwajali zaidi wao kwenye hospitali hiyo kwani ziko hospitali nyingi katika jiji la Dar es Salaam lakini wamewachagua wao kuwapelekea msaada huo.

“Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani Puma mmeona haja ya kuja kwetu na kutushika mkono, vifaa hivi kwetu vitasaidia katika kutoa huduma katika wodi ya wanawake tunawashukuru sana. na Mungu awabariki.” Alimaliza kusema Kaimu Mganga Mfawidhi huyo.

Wakati huo huo Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni (DMO) Dk. Lucas Ngamtwa amesema wanatoa shukrani za dhati kwa kampuni ya Puma kwa namna ambavyo wameguswa na kuamua kuwashika mkono katika hospitali hiyo.

“Hospitali yetu ni mpya bado tunachangamoto nyingi ikiwemo ya watalaam na vifaa tiba lakini kwa kutambua hilo Kampuni ya Puma mmeona mje mtushike mkono kwa kuhakikisha akina mama wanaokuja kupata huduma katika hospitali yetu wanakuwa salama na wanajifungua katika mazingira mazuri.”

Leave A Reply