The House of Favourite Newspapers

Quick Rocka, Mbona Unajishusha?

0

 

QUICK Rocka ni mmoja wa wanamuziki ambao waliingia kwa kishindo kikubwa katika anga la Muziki wa Kizazi Kipya, enzi zile wakija na kundi lao la Rockaz, ambalo liliundwa na wanamuziki ambao ni Chief Rocka na Mo Rocka.

Kibao chao, Bullet kilipenya vizuri na kukamata masikio ya mashabiki kwa kiwango cha juu sana, kiasi kwamba kundi lao likazoeleka haraka na kuonekana kama la siku nyingi na tangu wakati huo, jina la Quick Rocka likajichomoza.

Ni kijana ambaye amekaa kisanii hasa, kwa namna anavyofanya kazi yake kiasi kwamba tayari ni figa muhimu miongoni mwa wasanii mastaa wa Bongo kwa sasa.

Baada ya Bullet, nilipata bahati ya kusikiliza kazi yake nyingine aliyofanya na Mfalme wa Freestyle Bongo, Ngwea iliyoitwa My Baby. Hakika ni kazi ambayo inamfanya shabiki kutambua uwezo wa mtu anayemsikiliza, kama alivyofanya vizuri pia katika Wimbo wa Down, aliofanya pamoja na Mimi Mars.

Ni msanii mwenye uwezo na anayejua namna ya kucheza na mic katika wakati ambao mashabiki wana kiu ya kutaka kusikia kazi mpya.

Hivi majuzi Quick Rocka amefanya kazi yake mpya iitwayo Watasema, akiwa amewashirikisha vijana wa OMG. Mara tu baada ya kuachiwa hewani kwa wimbo huo, mkongwe TID, ameibuka na kulalamika juu ya kuchukuliwa sehemu ya wimbo wake uliompatia mashabiki wengi, Watasema.

TID analalamika kuwa Rocka na wenzake hawakumshirikisha katika wazo la wimbo huo, hivyo anataka kulipwa.

Sijamsikia Quick Rocka anasema nini kuhusu suala hili, lakini vyovyote iwavyo, anatakiwa kumuomba radhi TID kwa aliyoyafanya. Kuingiza verse ya mwimbaji mwingine katika wimbo wako siyo jambo geni, ni utamaduni wa miaka nenda rudi.

Lakini alichojaribu kukikwepa Quick Rocka, ni ukweli kuwa haiwezekani kuingia maneno au beat ya mtu kwenye kazi yako pasipo mwenyewe kufahamu. Huu ni wizi kama wizi mwingine.

Ndiyo maana haishangazi kumuona TID akitoa povu, si kwamba ameishiwa kama wengine wanavyojaribu kutengeneza mazingira, bali anafanya hivyo kwa sababu ni haki yake ya msingi kabisa. Hata angekuwa ni milionea kiasi gani, mtu hawezi kutumia jasho lake pasipo mwenyewe kushirikishwa.

Huu ndiyo utamaduni wa muziki, wasanii wengi walishaweka vipande vya wanamuziki wenzao wa zamani au wa enzi moja, kutegemea na uchaguzi wao. Alifanya hivyo Mr Paul aliporudia Wimbo wa Jabali la Muziki, Marijani Rajabu wa Zuwena au hata Lady Jaydee alipofanya Muhongo wa Jang’ombe wa Bi Kidude.

Kwa nini Quick Rocka hakuzungumza na TID kuhusu kipande hicho cha maneno? Lakini pia kulikuwa na tabu gani kwake kuchagua jina lingine tofauti na hilo la Watasema ambalo tayari alishalitumia mwenzake?

Yote kwa yote, huu siyo aina ya muziki ambao tungependa wasanii wetu wafanye, kwa sababu kwanza kunapunguza ubunifu, lakini pia ni kuzalisha malumbano na bifu zisizo na kichwa wala miguu. Katika hili, TID anayo haki ya kuuzuia wimbo huu na hao jamaa wakalazimika kumlipa.

Muziki haujawahi kuzalisha mbabe wala mjuaji wa kudukua kazi za wenzie. Na siku zote mbunifu hapatwi na majanga ya kitoto kama haya ya kunakili kazi za mwenzake.

Na pengine huu uwe pia ujumbe kwa wasanii wengine wanaofikiri wanaweza kutumia kazi za mtu pasipo mazungumzo. Enzi zimebadilika, haki za wasanii zinalindwa kwa mujibu wa sheria. Na msanii mkubwa hivi, unawezaje kufanya hivi?

 

Kauli ya Sheikh Ponda Kuhusu Denti UDSM Aliyeuawa na Polisi kwa ‘Ujambazi’

Leave A Reply