The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Rais Magufuli Atua Mwanza kwa Ziara ya Siku 2, Kesho Kuzindua Mradi Sengerema

0

Rais John Magufuli ametua jijini Mwanza na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imedhamiria kuondoa kero ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi na kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama wamachinga ili wafanye biashara zao bila kusumbuliwa.

Rais Magufuli amesema hayo leo (Julai 3) baada ya kuwasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi wa mkoa huo.

Akiwa mkoani hapa, Rais Magufuli kesho (Julai 4) atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Sengerema.

Katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Rais Magufuli amekutana na kamati ya amani ya viongozi wa dini ambao aliwashukuru kwa sala na dua zao na amewataka waendelee kuwahimiza waumini kuliombea Taifa ili liepukane na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa maendeleo.

Akiwa njiani kutoka uwanjani eneo la Bwiru, akielekea Ikulu ndogo ya Mwanza, Rais alisimama kuzungumza na wananchi waliokuwa wamejipanga barabarani na kusimamisha msafara wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imepania kupambana na ufisadi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali tofauti za dini au siasa.

Akiwa eneo la Nyamagana, Rais alitembea kwa miguu na kuwasalimu wananchi waliokuwa wakimshangilia na kuzuia msafara wake.

Pia, alienda Uwanja wa Mpira wa Nyamagana na kuungana na baadhi ya wananchi waliokuwa wakiangalia mechi ya mpira wa miguu kati ya timu ya Buhongwe na Nyamwaga.

Rais Magufuli pia alisema amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi katikati ya jiji ambao gharama za ujenzi wake zilitokana na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano.

 
MAPOKEZI YA RAISI MAGUFULI JIJINI MWANZA, JULAI 03, 2017

Rais Magufuli Atua Mwanza, Kuzindua Mradi Mkubwa wa Maji Sengerema

Leave A Reply