The House of Favourite Newspapers

Rich Mavoko, Diamond Mbona Freshi tu

0

RICHARD Martin Lusinga ndilo jina lake halisi lakini wengi wamezoea kumuita Rich Mavoko kutokana na kazi yake ya muziki wa Bongo Fleva anayoifanya kwa muda mrefu kiasi cha kupachikwa jina la Messi wa Bongo Fleva.

 

Rich Mavoko amewahi kutamba na anatamba na ngoma zake nyingi kama Marry Me, Silali, Uzuri wako, Roho Yangu, Kokoro, Ibaki Stori, Follow Me, Ona (na Lulu Diva) na nyingine nyingi ambazo zilifanya vizuri na bado zinafanya poa kunako platforms mbalimmbali za muziki.

 

Rich Mavoko amekuwa kimya kiasi f’lani baada ya kutoka kwenye Lebo ya Wasafi chini ya Diamond Platnumz kabla ya mwaka jana kuibuka na EP yake ya Mini Tape.

IJUMAA SHOWBIZ imemtafuta na kufanya naye mahojiano maalum (exclusively) ambapo amefunguka mambo mengi kuhusu kazi, maisha yake binafsi na matarajio yake kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva;

 

IJUMAA SHOWBIZ: Gemu la muziki kwa sasa unalionaje?

RICH MAVOKO: Kwa upande wangu naona gemu bado liko poa tu kwa sababu kazi nzuri zinazidi kutoka na maisha ya wasanii yanabadilika, wanamiliki majumba na magari ya kifahari.

IJUMAA SHOWBIZ: Mwaka jana uliachia EP na ikafanya vizuri, vipi mwaka huu tutegemee utaachia album?

 

RICH MAVOKO: Ndiyo, mashabiki wangu wakae mkao wa kusikiliza muziki mzuri, mwezi huu (wa 10) au ujao (wa 11) nitatoa album yangu mpya.

IJUMAA SHOWBIZ: Album itakwenda kwa jina gani?

RICH MAVOKO: Siku zikikaribia nitawaambia jina la album, lakini kwa sasa siwezi kulisema.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Tutegemee kuwaona mastaa gani wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi kwenye album yako?

RICH MAVOKO: Kila kitu kitakuwa ni surprise hivyo naomba mashabiki zangu wasikae mbali na kurasa zangu za mitandao ya kijamii.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa ukifanya muziki mzuri siku zote, lakini huonekani ukiwa nominated (kuteuliwa kuwania) tuzo mbalimbali, unahisi tatizo ni nini?

 

RICH MAVOKO: Ni kweli nafanya muziki mzuri, lakini huwa naamini kwenye hizi tuzo lazima mtu uwe na koneksheni nzuri ndiyo uwe nominated. Pia naona kuna baadhi ya mastaa huwa wanaomba wenyewe kuingia hivyo kila jambo na wakati wake na wakati wangu utakapofika basi nitawania siku moja.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Haikuumizi kuona wenzako wanatajwa kila siku kwenye tuzo na wewe hutajwi?

RICH MAVOKO: Kusema ukweli sijawahi kujisikia vibaya hata siku moja, kama nilivyosema mwanzo kuwa kila jambo na wakati wake na mimi najiamini, nafanya vizuri hivyo hata bila hizo tuzo mimi bado nitaendelea kuwa bora kwenye gemu.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Wasanii wakongwe wa Bongo Fleva kama King Kiba, AY, Profesa Jay na wengineo walionesha kutofurahishwa na baadhi ya mastaa ambao wameamua kuimba Amapiano ili kujiingizia kipato wakati siyo asili ya muziki wetu na badala yake wakashauri kuwa ingekuwa vizuri zaidi kama mastaa hao wangeimba Bongo Fleva ili kuzidi kuipeperusha bendera ya nchi yetu, vipi kwa upande wako wewe hili unalichukuliaje?

 

RICH MAVOKO: Jambo ambalo watu wengi hawaelewi ni kitu kimoja kwamba Amapiano ni kama Kwaito tu au Niger Music; hii ni aina ya muziki wa kuzuka, muziki ambao unakuja na kuondoka kwa hiyo haiwezi kuathiri chochote kwenye Bongo Fleva. Binafsi siwezi kuwalaumu hao wasanii walioimba Amapiano kwa sababu kila mtu anaimba kitu ambacho anakiona kwenye maono yake.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa maana hiyo tutegemee kukuona na wewe unaimba Amapiano kwenye album yako ijayo?

RICH MAVOKO: Kuhusu hilo pia nitazungumza muda ukifika kama kwenye album yangu kutakuwa na Amapiano au la, lakini pia hata kama ikiwepo, basi haiwezi kuwa Amapiano kama ile ambayo watu wameizoea; yaani itakuwa Amapiano, lakini itakuwa na Bongo Fleva kwa sababu ndiyo asili yetu.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mara ya mwisho kuwasiliana na Diamond Platnumz ilikuwa ni lini na mliongea kuhusu nini?

RICH MAVOKO: (anacheka) sikumbuki kwa kweli, nadhani hata mwaka utakuwa umepita hatujawasiliana

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi lakini umefikiria labda kumshirikisha kwenye album yako?

RICH MAVOKO: Inategemea, ikitokea mbona freshi tu.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Lakini unatamani ashiriki?

RICH MAVOKO: Ni msanii ambaye anafanya vizuri kwa hiyo kama menejimenti itaona anastahili kuwepo kwenye album yangu ni sawa, sina tatizo kwenye hilo.

IJUMAA SHOWBIZ: Uhusiano wako na Harmonize kwa sasa katika kazi ukoje?

 

RICH MAVOKO: Hapana, kwa sasa bado hatujapata nafasi ya kukaa na kuzungumza kuhusu kazi.

IJUMAA: Lulu Diva anaendeleaje?

RICH MAVOKO: Sifahamu kwa sababu huwa siwasiliani naye kabisa.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini hamuwasiliani wakati kuna kipindi ilikuwa inasemekana kuwa mpo kwenye uhusiano wa kimapenzi?

 

RICH MAVOKO: Mimi na Lulu hatujawahi kuwa karibu wala kuwa na uhusiano wa kimapenzi, ukaribu wangu mimi na yeye ulikuwa ni kwa ajili ya kazi tu na siyo vinginevyo.

IJUMAA SHOWBIZ: Asante kwa muda wako.

 

RICH MAVOKO: Shukrani, karibu tena na tena.

 

MAKALA; MEMORISE RICHARD, BONGO

Leave A Reply