The House of Favourite Newspapers

Safari ya Mwisho ya Rais Moi Yaanza Kabarak Nakuru

0

MWILI wa aliyekuwa rais mstaafu wa Kenya, Daniel Toroitich Arap Moi,  umesafirishwa kwa ndege ya kijeshi kutoka Nairobi ukipelekwa nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru, ambako anazikwa leo Jumatano.

 

Ndege hiyo imewasili uwanja mdogo wa Kabarak dakika chache kabla ya saa tatu za asubuhi. Awali, ndege iliyobeba mwili wa Rais huyo mstaafu na aliyetawala Kenya kwa miaka 24 iliondoka katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi, mwendo wa saa moja na dakika arubaini na tano asubuhi.

 

Baada ya zaidi ya miaka 96 duniani hatimaye safari ya hayati rais mtaafu Daniel Toroitich Arap Moi inafika tamati hivi leo.

 

Maombi ya mazishi yanaandaliwa katika shule ya msingi ya Kabarak kabla ya mwili wake kusafirishwa takriban kilomita nne hadi nyumbani kwake atakapozikwa mkabala na marehemu mkewe Lena Moi aliyefariki mwaka 2004.

Mamia ya watu walianza kufika katika shule ya msingi ya Kabarak kuanzia mwendo saa kumi asubuhi tayari kumpa mkono wa buriani mwenda zake rais mutaafu. Kila alipowasili alipokezwa mkate na maji. Mwili wa hayati Moi umeondolewa kutoka hifadhi ya maiti ya Lee hadi uwanja wa ndege wa Wilson na kusafirishwa kwa ndege hadi Kabarak.

 

Familia ya marehemu ikiongozwa na mwanawe Gedion Moi, imeshuhudia mwili wa marehemu ukiwekwa kwenye ndege ya kikosi cha wanajeshi wa nchi kavu, ndicho Kenya Army.

Kwa mujibu wa itikadi na desturi za hafla ya mazishi, familia na waombolozaji kwa jumla huvalia mavazi meusi, na kipande cha kitambaa hususan cheupe kwenye mfupo wa shati au blauzi. Kipande hicho pia hutundikwa begani.

 

Mwanawe marehemu, kitinda mimba na pia seneta wa Baringo Gedion Moi na familia yake, wote wamevalia mavazi meusi, kwa mujibu wa picha na video zilizonaswa uwanjani Wilson akishuhudia mwili wa Mzee Moi ukiwekwa kwenye ndege.

 

Ni taswira ambayo pia inaonekana kwa wengi wa waombolezaji ambao tayari wamefika nyumbani kwake (Mzee Moi) Kabarak. “Mavazi meusi ni ishara ya heshima kwa marehemu,” anasema Dennis Mugambi. Nyingi ya hafla za mazishi, waombolezaji huvalia mavazi meusi.

Mzee Moi aliaga dunia Februari 4, 2020, akiwa na anapewa mazishi ya hadhi ya heshima ya juu kitaifa na kama kiongozi aliyewahi kuwa Amiri Jeshi Mkuu, atasindikizwa na ufyatuaji wa mizinga 19.

 

Rais Uhuru Kenyatta ataongoza taifa katika kumpungia mkono wa buriani Mzee Moi, hafla ambayo itahudhuriwa na marais kadha wa kigeni pamoja na viongozi na wageni mashuri kutoka serikalini na nchi za kigeni. Kwa mujibu wa waandalizi wa mazishi hayo, yanatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya watu 30,000.

 

Vikosi vya jeshi tayari vimeandaa gwaride katika uwanja mdogo wa ndege wa Kabaraka tayari kupokea mwili wa aliyekuwa amiri mkuu wa majeshi. Mazishi yake yataongozwa na idara jeshi kuashiria kwamba marehemu alikuwa amiri mkuu wa majeshi kabla ya kustaafu. Mizinga 19 ya kijeshi itapigwa kwa heshima yake.

 

Maombi rasmi ya kumwombea hayati Moi yaliandaliwa siku ya Jumanne katika uwanja wa kimaaifa wa Nyayo na kuhudhuria marais na viongozi kadhaa wa nchi mbali mbali.

Na SAMMY WAWERU

Leave A Reply