The House of Favourite Newspapers

Samia awatwisha zigo la mauaji viongozi wa Dini

0

RASI Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa kidini na kimila kuwa chanzo cha kudhibiti mauaji yanayotokea mara kwa mara nchini, kwa kutoa mafunzo ya maadili yatakayosaidia kurejesha utu na hofu ya Mungu.

 

Ameyasema hayo leo Februari 22 alipohutunia katika maadhimisho ya miaka 25 ya Jubilee ya Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi yaliyofanyika wilayani Ngara Mkoa wa Kagera.

 

Amesema wilaya ya Ngara kwa mwaka 2022 kulikuwa na matukio ya kuuawa na kujiua 22 huku mwaka 2021 kukiwa na matukio 21, akisema visababishi ni pamoja na wivu wa mapenzi, tamaa ya mali, imani za kishirikina, msongo wa mawazo na ugomvi wa kifamilia.

 

“Anayetia uhai na kutoa uhai ni Mungu pekee sasa sina uhakika wanaojiua au kuua wenzao kuwa ni kazi ya Mungu, hivyo viongozi wa dini na mila mna kazi ya kufanya kama ulivyosema Baba Askofu (Niwemugizi) kuwa umeshaianza kuwa kuitisha kikao kati ya viongozi wa dini, mila na serikali katika wilaya yenu,” amesema Samia.

 

Rais Samia amesema serikali itatumia somo la uraia kupandikiza hofu ya Mungu na uzalendo kwa wanafunzi ili wawe mstari wa mbele kupambana na mauaji hayo.

 

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Askofu Niwemugizi amesema licha ya kuwepo kwa juhudi za kupambana na mauaji hayo, lakini zimejikita kwenye matokeo ya tatizo badala ya kutafuta chanzo.

 

Amewataka viongozi wa dini kulaani matukio ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu huku akiwatahadharisha viongozi wa dini kutonyamaza kwani kufanya hivyo kutaifanya ghazabu ya Mungu kunyanyuka.

 

Amesema matukio hayo yanatia doa katika taifa hivyo yanatakiwa kulaaniwa na kila mtanzania. “Viongozi wa dini tukinyamaza, ghadhabu ya Mungu itaamka, mambo ya hovyo yanatendeka na sisi hatusemi, wanaotenda mabaya lazima tuwashauri na tuwaonye ili waishi vizuri,” amesema Niwemugizi.

Leave A Reply