The House of Favourite Newspapers

Sasa Ndiyo Mtamjua Asante Kwasi Akiwa Simba

Asante Kwasi (kulia) enzi akiwa timu ya Lipuli.

KWA muda mrefu, kikosi cha Simba kilikuwa kikihitaji mchezaji mmoja mwenye uwezo wa kufanya majukumu zaidi ya matatu uwanjani.

Mwanzoni mwa msimu huu, wakamchukua Erasto Nyoni na Shomari Kapombe ambao ndiyo wachezaji wanaoonekana kuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani. Wawili hao wote wametokea Azam FC.

 

Kapombe ambaye tangu ajiunge na Simba ameshindwa kucheza hata mechi moja mpaka sasa kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyonga, ana uwezo wa kucheza beki wa kulia, kushoto na katikati.

Asante Kwasi akijiandaa kumkaba mchezaji wa Yanga.

 

Kwa upande wa Nyoni, nafasi hizo anazocheza Kapombe anaziweza, lakini pia anaweza kucheza kiungo mkabaji.

Licha ya wawili hao kusajiliwa kwa wakati mmoja, lakini Simba ikahitaji mchezaji mwingine wa ziada. Katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Desemba, mwaka jana, ikaingia sokoni na kuinasa saini ya Mghana, Asante Kwasi.

 

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza imekuwaje Mghana huyo atue Simba kwani ana nini cha ziada kulinganisha na mabeki lukuki ambao wamejaza kwenye kikosi hicho ambao nao wanacheza nafasi sawa na yeye!

 

Ujio kwa Kwasi ndani ya Simba una maana nyingi. Kwanza ni kuziba pengo la Mzimbabwe, Method Mwanjale, lakini pia kufanya majukumu ya wachezaji wengine uwanjani inapotokea kuna uhitaji huo.

 

Spoti Xtra linakuletea mambo hayo adimu ambayo Kwasi anayo na yanaweza kuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Simba ambacho Februari, mwaka huu kitaanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kucheza dhidi ya Gendarmerie Nationale FC ya Djibout.

 

KUIMARISHA SAFU YA ULINZI

Kabla ya ujio wa Kwasi, walinzi wa kati waliokuwa wakiiunda safu ya ulinzi ya Simba walikuwa ni Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Method Mwanjale na Salim Mbonde.

Mwanjale akaachwa katika usajili wa dirisha dogo, Mbonde akapata majeraha, Kwasi akasajiliwa, huku pia Paul Bukaba naye akiruhusiwa kuitumikia timu hiyo.

Kusajiliwa kwa Kwasi inamaanisha kwamba safu hiyo ya ulinzi itakuwa imara zaidi kutokana na Mghana huyo kujituma zaidi huku akiwa mhamasishaji kwa wenzake.

 

Hilo litaisaidia Simba kwenye harakati zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini hata kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Kwasi ambaye aliwahi kucheza soka Mbabane Swallows ya Swaziland kabla ya kutua Tanzania, ni wazi atakuwa na uzoefu na mechi za kimataifa. Simba hapa itakuwa imepata mtu sahihi wa kuijenga safu yao ya ulinzi.

 

MIPIRA ILIYOKUFA NI YAKE

Kikosi cha Simba mara kadhaa kinapokuwa uwanjani, Shiza Kichuya ndiye amekuwa akipambana sana na mipira iliyokufa ambayo ni faulo, kona na penalti. Katika faulo amekuwa hana kawaida ya kuzipiga moja kwa moja langoni.

Lakini kutokana na ujio wa Kwasi, ni wazi zile faulo zitakazotokea kwenye eneo la hatari la timu pinzani atakabidhiwa Mghana huyo kutokana na umahiri wake kwenye anga hizo. Lakini pia hata penalti anajua sana kupiga.

 

Kwasi tangu akiwa Mbao alikuwa hatari kwa mipira hiyo, lakini hakuwahi kufunga kwa faulo wala penalti, lakini amekuja kuwa hatari zaidi alipotua Lipuli.

Mpaka anaondoka Lipuli, amefunga mabao manne ambayo mawili kwa penalti na mawili kwa faulo.

Mabao aliyofunga kwa penalti ni dhidi ya Mbao waliposhinda 2-1, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Mwadui.

Na yale aliyofunga kwa faulo ni dhidi ya Ndanda ambapo timu yake ilifungwa 2-1, pia dhidi ya Simba wakati timu hizo zilipotoka sare ya 1-1.

MABAO YAKE YATAWAAMSHA WASHAMBULIAJI

Inafahamika Kwasi ni beki, lakini ana uwezo mzuri wa kufunga mabao na kuipa timu yake ushindi.

Simba kwa muda mrefu imekuwa ikimtumia zaidi Emmanuel Okwi katika ufungaji, alipokuja kupata majeraha, timu hiyo ikawa na shida ya ufungaji.

Hivi sasa John Bocco anajitahidi kuokoa jahazi kwa kufunga mabao. Lakini Kwasi pia anaweza kuwa msaada wa hilo akishazoeana na wenzake.

Kitendo cha Kwasi kufunga mabao manne akiwa beki tena katika timu zilizokuwa zimefanya usajili wa kawaida kabisa, ni jambo la kuvutia na dalili kwamba ni fundi.

Hata siku ikitokea washambuliaji wa Simba wamebanwa, yeye anachukua majukumu yake.

Jambo hilo litawafanya washambuliaji wa timu hiyo kuamka na kutimiza majukumu yao ipasavyo bila ya kusubiri beki awasaidie, wataonekana hawana kazi, mwisho wa siku wataambulia kukaa benchi.

 

Spoti Xtra baada ya kuyaona hayo, ikazungumza na kocha wake wa sasa, Masoud Djuma raia wa Burundi; “Sijawahi kumuona akicheza, lakini nimepata taarifa zake kwamba ni beki mzuri na atatusaidia ndiyo maana amesajiliwa hapa.”

“Tuna michuano mingi mbele yetu ikiwemo ile ya kimataifa, ni wazi tunatakiwa kuwa na kikosi kipana ambacho kila idara kiwe kamili. Ujio wake utasaidia hilo,” alisema Djuma.

Kwa upande wa Selemani Matola ambaye ndiye kocha wake wa zamani alipokuwa Lipuli, anasema: “Kwasi ni mchezaji mzuri sana na kuondoka kwake kikosini kwetu ni pigo kubwa, lakini hatuna jinsi tunapambana kuhakikisha pengo lake tunaliziba haraka.

“Wapo mabeki wengi ambao wataziba pengo lake, lakini kuwa na mchezaji kama yeye kikosini kunamaanisha kwamba mna zaidi ya mchezaji, ataisaidia sana timu yake ya sasa.”

MAKALA NA OMARY MDOSE | SPOTI XTRA

Comments are closed.