The House of Favourite Newspapers

SBL YASHAURI MFUMO WA KODI UARAKISHWE

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Mark Ocitti, ameshauri kuharakishwa kwa utaratibu wa kuoanisha mfumo wa kodi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ocitti amesema, pamoja na kwamba hatua nzuri na kubwa zimefikiwa, lakini vikwazo vya kibiashara vilivyopo havina budi kushughulikiwa ili kuongeza kasi ya uwekezaji na kurahisisha biashara ya bidhaa na huduma.

Akizungumza katika mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Wakuu wa Nchi za EAC uliofanyika jijini Arusha, Ocitti amesema tafsiri tofauti za vipengele vya kisheria kama ‘bidhaa za nje’ imesabisha kuwepo kwa kodi kubwa kwa bidhaa zinazotoka ndani ya nchi wanachama, jambo ambalo limepunguza kasi ya ukuaji wa biashara.

“Utekelezaji wa kuoanisha mfumo wa kodi miongoni mwa nchi wanachama umekuwa hauendi vizuri kwa sababu mbalimbali ikiwemo utofauti ya kiuchumi pamoja na kufikiria mapato, viwanda vya ndani, ushindani na nyinginezo,” amesema.

Akizungumzia athari zake kwenye sekta ya uzalishaji wa bia, alisema utofauti wa kodi za ndani miongoni mwa nchi wanachama, umesababisha kuongezeka kwa pombe haramu na kuongeza kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa kanuni itayoweka mfumo wa kodi unaofanana kutokana na utofauti wa maendeleo ya kiuchumi na pia hakuna msukumo wa kisheria unatoa msisitizo kwa jambo hilo.


“Kasi ndogo ya upitiaji wa Itifaki ya Ushuru wa Forodha kwa nchi wanachama wa EAC unaathiri baadhi ya shughuli na kuzifanya bajeti za nchi hizi kutegemea kwa kiasi kikubwa ushuru wa forodha. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2018 kumekuwa na mfumo mzuri kati ya nchi wanachama kwa kukuliana muundo wa 0%, 10%, 25% na 35,” amesema.

Akizungumzia namna kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL) ambayo ni kampuni mama ya SBL ilivyoathirika amesema imekuwa ni bahati nzuri kuwa makampuni yaliyo chini ya EABL yamesajiliwa kama makapuni ya ndani kwa nchi wanachama na hivyo hayajaathirika kwa kuwa bidhaa zake zinazalishwa ndani ya nchi hizo.

Na Neema Adrian

Leave A Reply